Dar es Salaam. Askari wanne wa Jeshi la Polisi Kitengo cha Intelijensia mkoani Kilimanjaro, wanaokabiliwa na kesi ya uporaji wa pikipiki ya abiria maarufu bodaboda, kwa kutumia silaha, leo Jumatano, Septemba 3, 2025 tena wanapandishwa kizimbani.
Askari hao wanaokabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Moshi, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ally Mkama ni G.2478 Ramadhan Jumanne, F.7340 Goodluck Richard, G.654 Zakayo Sanga na Victor Shelukindo, wote wakiwa na cheo cha Sajini.
Maofisa hao wenye dhamana ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo, Agosti 22, 2025.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 20614/2025, wanakabiliwa na shtaka moja la wizi wa pikipiki kwa kutumia silaha, kinyume na kifungu cha 287A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code – PC) kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Katika maelezo ya shitaka hilo kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyoko katika mfumo wa mashauri wa Mahakama, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 22, 2025.
Wanadaiwa siku hiyo katika eneo la Police Line ndani ya wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakiwa na silaha aina ya pingu, waliiba pikipiki aina ya Sinoray yenye namba za usajili MC 406 ERU, mali ya Ramadhan Joseph Singe
Wanadaiwa kabla na baada ya kuiba pikipiki hiyo, washtakiwa hao walimtisha na kutumia pingu hizo kwa kumfunga Ramadhan ili kujipatia pikipiki hiyo.
Kifungu cha sheria wanachostakiwa nacho askari hao kinasema mtu anayeiba kitu chochote na kabla au baada ya kuiba anakuwa na silaha au chombo chochote cha hatari au cha kukera na atakitumia kupata au kuhifadhi kitu hicho anakuwa anatenda kosa la wizi wa kutumia silaha.
Endapo atatiwa hatiani, atawajibika kwa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 jela kwa kosa hilo la wizi au pamoja na adhabu ya viboko.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Mkama aliahirisha kesi hiyo mpaka leo Jumatano itakapotajwa tena na aliamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu gerezani.
Kwa mujibu wa sheria, shitaka hilo halina dhamana hivyo washitakiwa wataendelea kuhifadhiwa mahabusu kwa kipindi chote cha kesi hiyo.
Kabla ya maofisa hao wanne wa polisi kupandishwa kizimbani na kusomewa shtaka la wizi wa bodaboda hiyo mali ya Ramadhani, askari Polisi sita mkoani Kilimanjaro walitiwa mbaroni kuhusiana na tukio la kutoweka kwa dereva bodaboda maarufu Moshi, Deogratius Shirima (35).
Mwendesha bodaboda huyo alitoweka Julai 21, 2025 lakini pikipiki aliyokuwa akiiendesha ilidaiwa kuwa ilibainika ilikuwa ndani ya nyumba kwa mmoja wa askari hao ndani ya kambi hiyo ya Polisi. Hata hivyo, mpaka leo bodaboda huyo hajapatikana na hajulikani alipo.
Jumanne ya Agosti 5, 2025, Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kwa simu na alipoulizwa juu ya tukio hilo na ni askari wangapi wa Jeshi la Polisi wa mkoani kwake wanashikiliwa alijibu:-
“Kama tulivyosema, uchunguzi unaendelea, viongozi wakubwa tupo nao hapa.”
Ingawa Kamanda Maigwa hakufafanua zaidi viongozi hao ni akina nani, lakini taarifa za uhakika ambazo Mwananchi lilizipata zilibainisha kulikuwa na timu ya maofisa wa Polisi iliyotoka makao makuu Dodoma ikiongozwa na ofisa mwenye cheo cha kamishna.
Taarifa ambazo Mwananchi lilizipata kutoka kwa vyanzo vya upande wa mwendesha bodaboda aliyetoweka baada ya kutoweka, mmiliki wa pikipiki hiyo aliitafuta kupitia mfumo wa Global Positioning System (GPS) iliyofungwa katika pikipiki hiyo.
GPS hiyo iliwaelekeza hadi nyumbani kwa askari polisi mmoja ndani ya kambi hiyo ya Polisi.
Ramadhani ambaye pikipiki yake ndio inahusika katika kesi hiyo, aliachwa eneo hilo kambi hiyo ya Polisi kuangalia nyumba ilimokuwa pikipiki hiyo kama kungekuwa na hatua yoyote ingechukuliwa na watuhumiwa kuhusiana na bodaboda hiyo.
Hata hivyo, Ramadhani alijikuta matatani baada ya polisi wawili kufika mahali hapo alipokuwa ambao walimkamata, wakamfunga pingu na kumuondoa na baadae pikipiki ya bodaboda aliyetoweka, ikahamishwa kutoka ndani ya nyumba hiyo.
Pikipiki hiyo aliyokuwa akiiendesha Deogratius kabla ya kutoweka ilikutwa imetelekezwa mtoni umbali wa kati ya kilometa tatu na saba.
Kwa mujibu wa mkewe, Mariam Abdi, siku mumewe anatoweka, waliachana saa 11 jioni ambapo alimtaka ampigie baadae ili ampe pesa kwa ajili ya chakula cha jioni na, muda huo ulipofika, alipiga simu yake lakini ikawa haipatikani tena.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kitakachojiri mahakamani hapo.