Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amewaagiza maofisa mazingira, ardhi na mipango miji kuweka utaratibu mzuri utunzaji wa mazingira na kutoruhusu mtu kujenga pasipo kupanda miti 20 katika maeneo yao.
Hatua hiyo imetajwa kuwa sehemu ya kuhamasisha jamii katika utunzaji wa mazingira kwa kutambua ni jukumu la kila mmoja na sio kwa vikundi wala Serikali.
Malisa ametoa agizo hilo wakati akikabidhi hundi ya Sh40.5 milioni kwa vikundi 18 vya kuweka na kukosa na utunzaji wa mazingira Mkoa wa Mbeya.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Beno Malisa(kulia) aliwa ameshika hundi ya Sh 40.5 milio ambayo alikabidhi kwa vikundi vya kuweka na kukopa na utunzaji wa Mazingira Mkoa wa Mbeya(katika) Meneja mradi wa Shirika la Likolto, Shukuru Tweve
Hundi hiyo imekabidhiwa kwenye mkutano maalumu ulioandaliwa Shirika la Likolto na kufanyika katika Ukumbi wa Beaco jijini na kuhusisha baadhi ya halmashauri.
“Mtu asipewe kibali cha ujenzi mpaka apande miti 20 katika eneo lake, lakini maofisa mazingira, ardhi na mipango miji wekeni utaratibu mzuri wa utunzaji wa mazingira,”amesema Malisa.
Malisa amesisitiza jukumu la kutunza mazingira ni la kila mmoja na sio vikundi wala Serikali na kwamba anayehitaji kuishi lazima ajikite kutunza mazingira.
“Maofisa wa Serikali msitoe vibali wala kuruhusu mtu kujenga pasipo kupanda miti, lakini pia wekeni utaratibu mzuri wa kutoa elimu kwa jamii na kujua umujimu wa utunzaji wa mazingira,” amesema Malisa.
Kuhusu hundi iliyotolewa, Malisa ameagiza Shirika la Likolto na wanufaika kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyo kusudiwa na sio vingine.

“Niwaombe zingatieni matumizi ya fedha mlizopata katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika suala la utunzaji wa mazingira ili kuifanya Tanzania hususani Mkoa wa Mbeya kuwa kijani,”amesema.
Msimamizi wa Mradi kutoka Shirika la Likolto, Shukuru Tweve amesema lengo la kutoa ruzuku hiyo ni kuwekeza utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ya matunda, mbogamboga na kuboresha makorongo ya mito yaliyo athirika na mmonyoko wa udongo.
“Vikundi vilivyo nufaika mikoa ya Mbeya na Songwe vitakwenda kuongeza nguvu utunzaji wa mazingira, upandaji wa miti rafiki ya matunda na mbogamboga na kuhifadhi maeneo yenye makorongo,”amesema Tweve.
Amesema kupitia mradi huo vikundi 18 kutoka Mkoa wa Mbeya vimenufaika na ruzuku ya Sh40.2 milioni na Mkoa wa Songwe vikundi 10 vitanufaika na ruzuku ya Sh22.5 milioni.