Safari ya chuo kikuu yaanza kwa wanafunzi 116,596 kwa mwaka 2025/2026

Dar es Salaam. Wakati awamu ya kwanza ya udahili wa Shahada ya Kwanza ikifungwa leo, jumla ya waombaji  116, 596 wamedahiliwa katika taasisi 88 za elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Kati ya hao 67,576 wamechaguliwa katika chuo zaidi ya kimoja au programu zaidi ya moja, hivyo wametakiwa kujithibitisha katika programu na chuo kimoja ili kutoa nafasi kwa wengine.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa amesema waombaji hao wametakiwa kujithibitisha katika chuo na programu moja ndani ya siku 19 kuanzia leo Septemba 3 hadi Septemba 21, 2025.

Amesema hatua hiyo itatoa nafasi kwa ambao hawajapata nafasi katika awamu ya kwanza kuwania nafasi hizo kwenye awamu ya pili ya udahili, ambayo inaanza Septemba 3 hadi 21, 2025.

Profesa Kihampa amesema katika mwaka wa masomo 2025/2026 taasisi za elimu ya juu zina nafasi za masomo 205,652 ikiwa ni ongezeko la nafasi 6,666 ikilinganishwa na mwaka wa masomo uliopita uliokuwa na nafasi 198,986.

“Mwaka huu nafasi zimeongezeka na hata programu za masomo zimeongezeka kufikia 894 kutoka 856 za mwaka wa masomo 2024/2025, hii ni sawa na ongezeko la programu 38,” amesema Profesa Kihampa.

Katika awamu ya kwanza ya udahili jumla ya waombaji 146,879 walituma maombi na asilimia 79.4 kati yao ndiyo waliochaguliwa kuacha nafasi 89,056.

“Hizi nafasi 89,056 ziko wazi kwa ajili ya awamu ya pili ya udahili na zitaongezeka kadiri wale waombaji waliochaguliwa katika chuo au programu zaidi ya moja watakakapojithibitisha kwenye chuo kimoja na kutoa nafasi kwa waombaji wengine.

“Hii ndiyo sababu tunasisitiza waombaji hawa kujithibitisha kwenye chuo kimoja. Tunapofungua awamu ya pili tunawasisitiza wale ambao hawakupata nafasi na wale ambao hawakutuma maombi wafanye hivyo katika muda uliopangwa,”

Pia, amevitaka vyuo vya elimu ya juu kutangaza programu ambazo bado zina nafasi, ili kutoa fursa kwa waombaji kuzichagua.

Akizungumzia hilo Mchambuzi wa masuala ya elimu, Dk Rehema Mhando amesema idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa katika chuo zaidi ya kimoja ni kielelezo cha changamoto za mfumo wa udahili.

“Ni muhimu kuendelea kuboresha mfumo ili kuepusha urundikaji wa nafasi na kuchelewesha wanafunzi wengine kupata fursa,” ameshauri.

Amina Mussa ambaye ni mwalimu wa sekondari, amesema ongezeko la nafasi na programu za masomo ni hatua nzuri, kwani linaonyesha jitihada za Serikali na vyuo vikuu katika kupanua fursa za elimu ya juu.

Hata hivyo, ameongeza kuwa changamoto kubwa inabaki kuwa ubora wa elimu unaotolewa.

Mwanafunzi aliyemaliza kidato cha sita, Kelvin Jonas, amesema hatua ya TCU kutoa siku 19 kwa waliochaguliwa kujithibitisha ni jambo zuri kwa sababu linatoa nafasi kwa wengine.

“Ni faraja kujua kwamba nafasi bado zipo kwa awamu ya pili. Hii inawapa matumaini wenzetu  ambao hawakuchaguliwa katika  awamu ya kwanza,” amesema.

Mkazi wa Kigamboni, Hassan Abdallah ambaye pia ni mzazi amesema ongezeko la nafasi za masomo ni ishara njema, lakini akasisitiza kuwa Serikali na vyuo vinapaswa pia kuongeza mikopo na ufadhili.

“Wanafunzi wengi wanachaguliwa, lakini changamoto ni ada na gharama za maisha chuoni,” amesema Hassan.