Dar/Dodoma. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma imepanga kusikiliza shauri la kuenguliwa katika uteuzi mgombea urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, baada ya maombi kutolewa na kujibiwa kwa maandishi.
Mahakama imetoa maelekezo hayo leo Jumatano, Septemba 3, 2025, baada ya wajibu maombi, Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuachana na mpango wa kuweka pingamizi la awali katika shauri hilo lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa ACT-Wazalendo na Mpina.
Kufunguliwa kwa shauri hilo kunatokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa Mpina kuomba kuteuliwa na INEC kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kutokana na uamuzi wa msajili, INEC ilimzuia Mpina kurejesha fomu ya kuomba kuteuliwa iliyokuwa imemkabidhi awali.
Katika shauri hilo namba 21692 la mwaka 2025 lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, waombaji wanapinga uamuzi wa INEC kumwengua Mpina katika orodha ya wagombea walioomba kuteuliwa na Tume, wakiomba mahakama iielekeze INEC ipokee fomu yake kwa ajili ya uhakiki na uteuzi.
Shauri hilo linasikilizwa na majaji Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza.
Wajibu maombi katika majibu waliyoyawasilisha jana Septemba 2, 2025, waliibua pingamizi la awali dhidi ya shauri hilo kwamba lisisikilizwe, badala yake litupiliwe mbali.
Iwapo pingamizi hilo lingeendelea, mwenendo wa shauri la msingi ungesimama kupisha usikilizwaji na uamuzi wake kwanza.
Hata hivyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa wajibu maombi, Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo leo Septemba 3, ameieleza mahakama kuwa baada ya kutafakari upya kuhusu uharaka wa shauri hilo, wameondoa pingamizi hilo ili kuendelea na usikiliziwaji wa shauri la msingi.
Baada ya uamuzi huo, Mahakama imeelekeza waombaji wawasilishe hoja zao Septemba 5 na wajibu maombi wawasilishe hoja za utetezi Septemba 7, 2025. Zote zitawasilishwa kwa maandishi kwa njia ya mtandao.
Pia, mahakama imeelekeza wadaawa wote kufika mahakamani Septemba 8, 2025 saa 8:00 mchana kwa ajili ya usikilizwaji wa ana kwa ana.
Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, Agosti 6, 2025 kugombea urais lakini uteuzi wake ulibatilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kutokana na pingamizi la Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala.
Monalisa alidai uteuzi huo ni batili kwa kuwa Mpina hana sifa kutokana na kutokutimiza vigezo vya kikanuni, akirejea Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa chama hicho, Toleo la mwaka 2015, kanuni namba 16(4) (i-iv).
Akirejea kanuni hizo, Monalisa alibainisha kuwa kanuni ya 16(4) (i) inaeleza mgombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa, anapaswa awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama.
Kanuni ya 16(4) (iv) anapaswa awe ni mtu aliyethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT-Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi.
Monalisa alibainisha kuwa Mpina anakosa sifa zote hizo, kwa kuwa alijiunga na chama hicho Agosti 5, 2025 na alipitishwa na mkutano mkuu kuwa mgombea wa chama hicho Agosti 6, siku moja baada ya kujiunga na chama hicho.
Msajili wa Vyama vya Siasa baada ya kusikiliza pande zote alikubaliana na hoja za pingamizi la Monalisa na kutengua uteuzi wa Mpina, INEC kwa upande wake baada ya kupata barua ya Msajili, ilimtaka Mpina asifike ofisi zake siku ya uteuzi wa wagombea, Agosti 27, 2025 hivyo, siku hiyohiyo alifungua kesi mahakamani.
Shauri hilo lilitajwa kwa mara ya kwanza Agosti 28, 2025.
Waombaji waliwakilishwa na jopo la mawakili John Seka, Edson Kilatu, Peter Madeleka, Mwanaisha Mdeme na Jaspar Sabuni, huku wajibu maombi wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method akishirikiana na Stanley Kalokola na Erigh Rumisha.
Mbali na nafuu zinazoombwa, pia Mpina aliiomba Mahakama iiamuru INEC isimamishe kwa muda mchakato wa uteuzi wa wagombea wa urais kusubiri shauri hilo kusikilizwa likishirikisha pande zote.
Mahakama katika amri zilizotolewa na Jaji Kagomba, ilikataa maombi ya kusimamisha mchakato wa uteuzi wa wagombea urais.
Hata hivyo, Jaji Kagomba alisema Mahakama ina wajibu wa kuangalia yote yaliyofanyika kama yamezingatia sheria na Katiba na kwamba, ikijiridhisha kuwa taratibu za kisheria na kikatiba hazikufuatwa katika kuondolewa kwake, haitasita kutoa amri zitakazomrudishia haki zake.
Wajibu maombi walipewa siku tano wawe wamewasilisha majibu na kiapo kinzani na shauri lilipangwa kutajwa leo Septemba 3.