Moshi. Mwalimu Deus John (30), anayefundisha Shule ya Sekondari Uru, iliyopo Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, amesimulia masaibu aliyopitia ya kukosa usingizi kwa miezi nane kabla ya kuondolewa uvimbe wenye uzito wa kilo mbili na maji zaidi ya lita tatu kwenye pafu lake la kushoto katika Hospitali ya KCMC.
Amesema hali hiyo ilianza polepole, kwa kikohozi cha kawaida na uchovu wa mara kwa mara, lakini kadri siku zilivyozidi kwenda alianza kuhisi maumivu upande mmoja wa kifua na kushindwa kupumua vizuri, licha ya kwenda hospitali mara kadhaa na kupewa dawa za kutuliza maumivu hayo.
Akizungumzia tatizo hilo leo Septemba 3, 2025 akiwa hospitalini hapo, amesema baada ya hali yake ya kiafya kuwa mbaya zaidi alikwenda Hospitali ya KCMC kwa matibabu zaidi na ndipo madaktari waligundua kuwa alikuwa na uvimbe mkubwa kwenye pafu la kushoto, sambamba na maji yaliyokuwa yakiziba mapafu na kushinikiza moyo kuelekea upande wa kulia.
“Nilianza kuona changamoto ya kifua kwa mara ya kwanza Februari mwaka huu, nilipoona mabadiliko hayo nilianza kufuatilia matibabu sehemu mbalimbali, lakini haikubainika shida ni nini na walikuwa wananipatia dawa za kutuliza maumivu ambayo nilikuwa nayasikia,” amesema Mwalimu John.
Amesema: “Kwa mara ya kwanza dawa zilinisaidia na ile hali ikapotea kidogo mpaka mwezi Mei hali ilivyorejea kama ilivyokuwa awali, niliendelea kufuatilia matibabu katika hospitali mbalimbali lakini sikuweza kupata suluhu, niliandikiwa vipimo vya moyo lakini majibu yalivyorudi yakaonyesha sina tatizo.”
Amesema kadri siku zilivyozidi kwenda, hali yake ya ugonjwa ilikuwa mbaya zaidi kwa kuwa kilikuwa ni kipindi cha hali ya baridi.
“Iipofika Agosti mwishoni nilienda Hospitali ya St Joseph kwa matibabu zaidi kwa kuwaelezea madaktari hali ilivyo, walinichukua kipimo cha X-Ray ambacho kilionyesha kuwa pafu moja la kushoto lina maji, wakanambia inahitajika kufanyika kipimo cha CT Scan, nikapewa Rufaa ya kwenda KCMC,”amesema Mwalimu John.
Amesema: “Nilienda KCMC wakaendelea na taratibu wakarudia X-Ray majibu yakatoka vile vile kama yalivyotoka awali, walinifanyia CT Scan ikaonyesha tatizo jingine wakasema kuna uvimbe kwenye pafu upande wa kushoto, hivyo nikaandikiwa vipimo ili kujaribu kuona shida ni nini lakini wakati huo nilikuwa na maumivu makali sana, yaani wiki mbili nilikuwa silali, nilikuwa nalala kwa kukaa kwenye kochi.”
Amesema kutokana na hali yake kuwa mbaya zaidi Madaktari wa hospitali ya KCMC waliamua kumfanyia upasuaji kutokana na hali yake kuwa ni mbaya na hivyo alitolewa uvimbe wenye uzito wa kilo mbili na maji zaidi ya lita tatu.
Mwalimu John amesema kwasasa anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu: “Sasa hivi najisikia vizuri zaidi, naweza kulala kuamkia na kutembea na kufanya mazoezi mwenyewe ni hatua nzuri, vinginevyo namshukuru Mwenyezi Mungu nimeinarika.”
Akimzungumzia mgonjwa huyo, Daktari bingwa wa upasuaji Hospitali ya KCMC, Profesa Kondo Chilonga amesema mgonjwa huyo alikuwa na uvimbe ambao ulikuwa na mkandamizo kwenye ukuta wa kushoto wa moyo uliomsababishia kushindwa kulala.
“Tatizo hili lilimfanya asumbuliwe na matatizo ya kifua ambapo alikuwa akiumwa mara kwa mara, amekuwa pia akikohoa kwa zaidi ya miezi minane na kushindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na matatizo ya kifua, lakini hali yake ya kiafya ilizidi kudorora siku za hivi karibuni ambapo maumivu yalikuwa yakiongezeka,” amesema Profesa Chilonga
Amesema baada ya mgonjwa huyo kufika KCMC walimfanyia vipimo ambavyo viliweza kuonyesha pafu lake la kushoto lilikuwa na uvimbe mkubwa ambao ulisababisha mapafu yake kushindwa kufanya kazi vizuri.
“Ni tatizo ambalo halipo kwa jamii kwa kiwango kikubwa, linapata watu wachache, lakini miongoni mwao huwa wanapaswa kufanyiwa upasuaji na tatizo lake lilikuwa ni kubwa na kumfanya eneo la kifua upande wa kushoto kubanwa,”amesema Profesa Chilonga
Profesa Chilonga amesema kutokana na tatizo lake lilikuwa ni kubwa walilazimika kufanya upasuaji kwa zaidi ya saa tano na walifanikiwa kuondoa uvimbe na maji yaliyokuwa kwenye mapafu.
“Kwa sasa tunasubiri kupata majibu ya vipimo vya kufahamu chanzo cha tatizo la kwake ni kipi kwa kutumia kipimo cha patholojia ili kuweza kujua kama ni uvimbe ambao ni saratani au la, kama vipimo vitaonyesha kama ni saratani basi hatua nyingine za matibabu zitaanza kufuata ikiwemo kuanza tiba ya saratani,” amesema Profesa Chilonga.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapoona tatizo ambalo limedumu kwa muda mrefu kuchukua hatua na kufika kwenye vituo vya afya kwa ajili ya matibabu.
“Natoa wito kwa wananchi, pale wanapoona panakuwa na matatizo ambayo yamekuwa kwa muda mrefu au kushindwa kupata matibabu ni vyema ukafika kwenye vituo au hospitalu ambayo unaweza kupata hizo huduma mapema zaidi ili kuweza kuzuia tatizo kuwa kubwa,” amesema Profesa Chilonga.
Profesa Chilonga, amesema kwa mwaka hufanya upasuaji kwa wagonjwa wenye matatizo ya kifua takribani 20 hadi 30.