Soud, Khatib kuchuana nafasi ya pili uchaguzi wa urais Zanzibar

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AAFP) Taifa, Said Soud Said amesema hakuna chama kimoja kitaweza kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM), iwapo vyama vingine havitaungana na kuwa na nguvu moja.

Soud ambaye pia ni mtiania urais kupitia chama hicho na tayari ameshachukua fomu ya kuomba uteuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) ametoa kauli hiyo leo Septemba 3, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho Mwera Unguja.

Amesema hilo linatokana na mizizi ambayo chama hicho tawala kimeshajiwekea.

Hata hivyo katika uchaguzi wa mwaka huu hakuna namna vyama hivyo vinaweza kuungana, tayari ZEC imeshatoa fomu za kuomba uteuzi watiania urais kwa vyama 17 ambapo ratiba ya kuchukua na kurejesha ilianza Agosti 28 na kukamilika Septemba 10, na Septemba 11 ni uteuzi wa wagombea watakaokuwa wamekidhi vigezo kupeperusha bendera za vyama vyao.

“Hakuna chama kitaweza kuiondoa CCM madarakani iwapo vyama hivi havitaungana, kwahiyo hiyo ndio njia pekee ya kukiangusha lakini iwapo kila mmoja akitaka kuishika madaraka itawachukua muda mrefu kufanikiwa,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu kuchukua fomu ya kuwania kiti cha urais Ilhali anajua ni ngumu bila kuungana, Soud amesema lengo lake anataka kushika nafasi ya pili ili awe Makamu wa Kwanza wa Rais.

“Kwanza tunatakiwa kujua kwamba kugombea nafasi yoyote ni haki ya kila raia wa Nchi hii kikatiba, kwahiyo ni haki yangu lakini pia lengo langu mimi ni kuwa nafasi ya Makamu wa Kwanza,” amesema Soud.

Soud anakuwa wa pili miongoni mwa watia nia 17 waliochukua fomu Zec kuwania urais lakini wao wakiweka wazi kwamba nia yao ni kushika nafasi ya pili Ili ili wawe Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mujibu wa katika ya Zanzibar.

Mwingine ambaye ameshaeleza kuitaka nafasi hiyo ni mtiania urais kupitia chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib ambaye naye wakati wa kuchukua fomu za uteuzi ZEC, alisema licha ya kushindania lakini yeye anapigania zaidi nafasi ya pili.

Akizungumza kuhusu kura ya mapema, Soud amesema chama chao kinakubaliana nayo na ndivyo sheria inavyotaka kwahiyo hawana budi kuitii na kuizingatia.
Amewasisitiza wananchi kuendelea kuwa wamoja na wasikubali kurubuni wa na wanasiasa katika kipingi hiki wanapoelekea kwenye kampeni na uchaguzi kufanya mambo yatakayoashiria uvunjifu wa amani.