ALIYEKUWA mshambuliaji wa Kagera Sugar raia wa Cameroon, Moubarack Amza amekamilisha usajili wa kujiunga na Bandari FC ya Kenya, itakayocheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Yanga katika kilele cha ‘Wiki ya Mwananchi’ Septemba 12.
Nyota huyo atacheza dhidi ya Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, katika tamasha la kikosi hicho linalofahamika kwa jina la ‘Wiki ya Mwananchi’, litakalofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Septemba 12, 2025.
Amza alijiunga na Kagera Januari 1, 2025, ikiwa ni kwa mara ya pili baada ya awali kujiunga nayo Januari 2024, kwa mkopo akitokea Singida Black Stars zamani Ihefu, kisha kuondoka msimu wa 2024-2025 na kutua kwa ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo FC.
Akizungumza na Mwanaspoti, Amza alisema ni kweli amekamilisha usajili huo wa kujiunga na Bandari ya Kenya kwa mkataba wa mwaka mmoja, akiamini anaenda kupata uzoefu mwingine baada ya kuitumikia Ligi Kuu Bara katika timu mbalimbali nchini.
“Nimeamua kutafuta changamoto nje ya Ligi ya Tanzania, nimejifunza mambo mengi sana kuanzia namna ya ushindani na jinsi watu wanavyopenda mpira, ni wakati kwangu wa kuangalia fursa upande mwingine hasa wa Ligi Kuu ya Kenya,” alisema Amza.
Amza kwa msimu wa 2024-2025 hakufunga bao lolote la Ligi Kuu Bara ingawa, msimu bora hapa nchini ambao hata yeye anakiri ulikuwa 2022-2023, akikichezea kikosi cha ‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union, ambao alimaliza msimu kwa kufunga mabao saba.
Katika kipindi chote cha miezi sita aliyoichezea Kagera Sugar alifunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara, huku mara yake ya mwisho kufunga ilikuwa kwenye ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0, dhidi ya Tabora United, mechi ikipigwa Aprili 17, 2024.
Kwa msimu wa 2024-2025, Bandari ilimaliza Ligi ya Kenya ikiwa nafasi ya nane kwa pointi 44, baada ya kushinda mechi zake 10, sare 14 na kupoteza 10 kati ya 34 ilizocheza, ikifunga mabao 26 na kuruhusu 30, huku bingwa ikiwa ni Kenya Police FC.