UONGOZI wa Tabora United umeingia sokoni kusaka kipya mpya baada ya tegemeo namba moja, Fikirini Bakari, kuvunjika taya katika mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga iliyowafunga mabao 4-0 katika Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.
Chanzo cha Mwanaspoti kimesema Bakari aliyemaliza akiwa na ‘clean sheet’ moja aliyoipata akiwa Fountain Gate kabla ya kujiunga wakati dirisha dogo kwa mkopo Tabora United msimu uliopita, itamchukua muda kuuguza taya lake aliloumia mwishoni mwa wiki iliyopita akiitumikia timu hiyo.
Na baada ya kubaini hilo, viongozi wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Bara itakapoanza Septemba 17 wameamua kwamba lazmima wawe na uhakika wa kuwa na kikosi imara na kamili.
“Viongozi kumtafuta kipa mwingine haina maana wataachana na Bakari, akipona ataendelea na majukumu yake kama kawaida. Ingawa yupo kipa wa kigeni hatuwezi kumwamini moja kwa moja peke yake,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Tumeangalia timu zingine zilivyosajili. Tunatambua ligi na michuano mingine ya msimu wa 2025/26 itakuwa migumu ndiyo maana tunajaribu kuweka sawa kila eneo ili tuanze ligi kwa kishindo.”
Mbali na hilo chanzo hicho kilisema Shaaban Chilunda aliyemaliza msimu uliopita na mabao mawili akiwa KMC, tayari amejiunga na Tabora United iliyopo Babati, Manyara katika mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yaliyoandaliwa na Fountain Gate.
“Chilunda aliingia kambini Jumatatu usiku ataendelea kufanya programu na wachezaji wenzake kujiandaa na msimu mpya. Tulichokizingatia (kumsajili) ni uzoefu wake katika ligi kapita Azam, Simba, KMC na kacheza nje, hivyo huduma yake itakuwa msaada kwa timu,” kilisema chanzo hicho.