Teknolojia ilivyopunguza udanganyifu sekta ya bima ya afya, AI yatajwa

Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji na Msimamizi Mkuu wa Jubilee Health Insurance, Dk Harold Adamson amesema mageuzi ya kidijitali ndiyo njia sahihi ya kuongeza idadi ya wananchi wanaojiunga na bima ya afya.

Vilevile, amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi umesaidia kufanikisha mabadiliko hayo.

Dk Adamson amesema ajenda ya afya kwa wote imekuwa msingi wa uamuzi kwako kuwekeza kwenye teknolojia ili kuhakikisha huduma inakuwa jumuishi na nafuu.

“Kwa muda mrefu sekta ya bima imekuwa ikitumia mbinu za jadi, lakini hivi sasa ushindani upo katika matumizi ya data. Taasisi yenye uwezo wa kutumia taarifa vizuri inaweza kutoa huduma bora kwa gharama nafuu na kuongeza ushirikiano kati ya watoa huduma na wanufaika,” amesema.

Amesema Jubilee imewekeza kwenye computational models (mifumo ya kihisabati na kitarakimu) zinazosaidia kutabiri gharama halisi za matibabu kwa kila mgonjwa kulingana na idadi ya watu katika eneo husika na aina ya huduma wanazohitaji.

Dk Adamson amesema mfumo huo unasaidia kuzuia kurudiwa kwa huduma zisizo na ulazima, hivyo kupunguza gharama kwa kampuni na wateja.

Pia, amesema matumizi ya teknolojia yamepunguza udanganyifu kwenye sekta ya bima, ikiwamo kurudia matumizi ya dawa au kudanganya kuhusu huduma zilizotolewa.

Kupitia mfumo wa akili mnemba (AI), amesema kampuni inaweza kubaini mapema maeneo yanayopoteza fedha na kuyafanyia kazi, hatua iliyosaidia kuokoa kiasi kikubwa cha rasilimali.

Amesema hayo leo Septemba 3, 2025 wakati wa mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Ltd (MCL) wenye mada isemayo: “Afya bora kwa wote: Ipi nafasi ya ubunifu wa kidijitali kuongeza wanaojiunga na bima ya afya?”

Kwa upande wake, mwanzilishi mwenza wa Kliniki ya Medikea, Desire Ruhinda amesema changamoto ya Watanzania wengi kutoshiriki kwenye mifumo ya bima ya afya imesabisha wataalamu na wabunifu wa teknolojia kutafuta suluhisho za kidijitali zinazolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Amesema waliona pengo kubwa kati ya wananchi na huduma za bima, hivyo wakabuni njia ya kidijitali itakayosaidia kuongeza uelewa na ushiriki.

“Kupitia aplikesheni ya simu, wananchi sasa wanaweza kupata huduma za afya kwa njia ya mtandaoni, ikiwamo kufanya video consultation na madaktari, kupokea dawa kupitia e-prescription, pamoja na kulipia huduma kwa awamu,” amesema.

Amesema mfumo huo pia umeunganishwa na maduka ya dawa na vituo vya afya vilivyopo jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa ukaribu zaidi.

Ruhinda amesema moja ya changamoto walizoziona ni gharama kubwa ambazo mgonjwa hulipa anapopata matatizo makubwa ya kiafya, akitoa mfano wa mgonjwa wa kisukari anayepata tatizo la figo kutokana na kuchelewa kupata huduma.

Mkurugenzi Mkazi wa PharmAccess, Dk Heri Marwa amesema ili kuchochea ongezeko la wanaojiunga na bima ya afya kidijitali, mkakati unapaswa kuwekwa katika utoaji wa taarifa kwa umma.

“Kwangu mimi naona ili kuvutia watu wengi kunufaika na ubunifu huu, kuwe na utoaji taarifa kwa umma ili watu wapate taarifa sahihi waweze kujiunga,” amesema na kuongeza:

“Usumbufu wa kuzifuata huduma unakuwa tatizo kwani huduma zinatolewa mikoani, kwa watu wa kijijini kwenda na kurudi mara kadhaa wengine huona usumbufu na kuamua kuachana nayo,” amesema.

Changamoto nyingine amesema ni gharama kubwa ambazo zinatokana na uchache wa wanaojiunga na bima ya afya, hali inayofanya gharama ziwe juu kwa wachache waliojiunga.

Amesema ikiwa zaidi ya asilimia 27 ya Watanzania watatumia intaneti, ubunifu wa kidijitali ukitumika vizuri na kuweka mazingira rafiki watu wengi wanaweza kujiandikisha na kunufaika na huduma hiyo kama ilivyo kwa nyingine za kimtandao.

Mbali ya hayo, imeelezwa uboreshaji huduma kwa wanufaika wa bima ya afya utavutia wanaojiunga na huduma hizo.

Raya Hamza Mohamed, Msimamizi Mkuu wa Mifumo katika Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) amesema uendeshaji wa mifumo ya huduma kwa wanufaika wa bima ya afya uunganishe na mingine ili isomane kuwezesha kuondoa usumbufu kwa wanufaika kwenda mara nyingi kwa mtoa huduma kwa tatizo lilelile.

“Cha msingi ni uboreshaji wa huduma kwa wanufaika kwa kuunganisha mifumo kidijitali isomane, badala ya mtu kuja mara nyingi kwa jambo moja. Apate huduma zote kwa wakati mmoja,” amesema.

Amesema ZHSF unatumia mifumo ya kidijitali katika utambuzi ukiwa umeunganishwa na mifumo ya Vitambulisho vya Taifa kurahisisha upatikanaji taarifa.

“Tayari tumeanza kusajili wanachama kwa kutumia mfumo, changamoto ni uelewa mdogo kwa jamii, ila kwa kuwezesha mfumo wetu kuunganisha na mfumo wa Vitambulisho vya Taifa inakuwa rahisi kupata taarifa zingine  na kuwaunganisha kirahisi wanaojisajili,” amesema.

Naye Waziri wa zamani wa Afya Zanzibar, Dk Seif Rashid amesema huduma ya kidijitali itarahisisha mawasiliano kati ya mtoa huduma, mpokea na mlipiaji wa huduma hizo.

Ameonyesha kutoridhishwa na idadi ya wanaopata huduma za afya kwa njia ya bima akisema ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya Watanzania na upatikanaji wa huduma za bima nchini (walipiaji).

Licha ya pongezi kwa maendeleo ya mifumo ya kidijitali aliyosema ina mchango mkubwa katika kurahisisha na kuvutia watu wengi katika utoaji huduma salama, amesisitiza kuboreshwa mifumo ili kurahisha zaidi huduma hizo.

“Kwa takribani miaka 10 tulikotoka, miongozo na mifumo imekuwa ikiwekwa na kuboreshwa ili iweze kuwasaidia wadau wote; watoa huduma, wapokea huduma na walipia huduma kuwasiliana na kutoa huduma kwa urahisi,” amesema.

Amesema ni muhimu kuendelea kuunganisha mifumo ya hospitali ngazi zote isomane ili kupunguza changamoto kwa mgonjwa kufanyiwa kipimo cha aina moja kila anapokwenda hospitali nyingine.

Pia, amepongeza juhudi zilizofanywa na Serikali kuwekeza kwenye maendeleo ya teknolojia ikiwamo malipo ya Serikali kwa njia ya namba za malipo akisema inarahisisha huduma zote kufanyika na kukamilika mtandaoni bila usumbufu.

Amesema wananchi wengi wanaoishi mbali na maeneo ya huduma za bima wamekuwa wakiikosa huduma hiyo lakini kwa kuihamishia mtandaoni wengi watajiunga na kunufaika nayo.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema changamoto inayowakabili wananchi wengi si tu ada ya bima, bali urahisi wa usajili na upatikanaji wa huduma.

Amesema matumizi ya mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali yana nafasi kubwa ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu manufaa ya bima ya afya.

“Kama tunaweza kutumia nguvu ya Instagram, TikTok, Facebook au WhatsApp kueneza taarifa za afya, basi tunaweza pia kuongeza kasi ya watu kujiunga na bima,” amesema na kuongeza:

“Teknolojia ya kidijitali inaweza kuwa nyenzo ya kipekee ya kuongeza Watanzania wanaojiunga na bima ya afya na kuboresha huduma za matibabu.”

Amesema teknolojia inaweza kuimarisha usalama wa wagonjwa kupitia ufuatiliaji wa matibabu kwa kutumia namba ya utambulisho wa afya.

“Hii itasaidia kuondoa changamoto za kupotea kwa taarifa au kudanganywa kwa huduma,” amesema.

Dk Nkoronko amesema zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanaoishi vijijini wanajihusisha na kilimo, lakini hawana kipato cha uhakika, hivyo mifumo ya bima inaweza kuunganishwa na sekta ya kilimo kupitia vyama vya ushirika na mikataba ya kilimo ili michango ya bima iwe sehemu ya shughuli zao za kila siku.

Amesema mageuzi ya kidijitali hayataishia kuongeza idadi ya watu wanaojiunga na bima pekee, bali pia yataleta uwazi, kupunguza gharama na kulinda maisha ya Watanzania.

Amesema ushirikiano wa sekta binafsi, taasisi za afya na Serikali ni muhimu ili kuhakikisha teknolojia inatumika kufanikisha lengo la Taifa la afya bora kwa wote.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Arusha, Hipoliti Lello amesema sheria ya bima ya afya kwa wote ni nyenzo ya kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma kati ya wenye nacho na wasio nacho, pia kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia.

Amesema tangu Agosti, 2024 baadhi ya vifungu vya sheria hiyo vimeanza kutekelezwa, ingawa bado ipo sehemu ya hiari, lengo ni kufikia ulazima kwa wananchi wote.

“Changamoto kubwa iliyobainika ni wananchi wengi kukosa uwezo hata wa nauli kufika ofisi za usajili, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kidijitali na uhamasishaji katika ngazi ya jamii,” amesema.

Lello amesema kwa kulinganisha na mifumo mingine ya bima, kwenye bima za vyombo vya moto ni kubwa kuliko bima ya afya, hali inayodhihirisha bado kuna kazi kubwa ya kuongeza uelewa wa wananchi.

Amesema Serikali ikikamilisha utekelezaji wa vifungu vyote vya sheria, kila mwananchi atalazimika kujiunga, hivyo kuongeza usawa wa huduma za afya nchini.

Kuhusu gharama, Lello amesema malipo ya michango yatabaki yakipangwa kwa kuzingatia makundi ya wananchi, akieleza wale wasio na uwezo watalipiwa na Serikali.

Hatua hiyo amesema inalenga kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma, huku wamiliki wa vipato vikubwa wakichangia zaidi ili kusaidia mfumo kuwa endelevu.

Amesema NHIF imebadilisha mikakati ya elimu na uhamasishaji, ikitumia zaidi mitandao ya kijamii na mbinu za kidijitali badala ya kutegemea matangazo ya kizamani.

Ameeleza kampeni nyingi tayari zimekuwa zikisambaa mtandaoni, zikivutia maelfu ya wananchi kuangalia na kupata taarifa, lakini changamoto inabaki kuwashawishi kuchukua hatua ya kujiunga rasmi.