Bukoba. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkoa Kagera wamezindua ofisi ya dawati maalumu la kuwawezesha wafanyabiashara kiuchumi.
Akizungumza katika uzinduzi wa ofisa ya dawati maalamu la TRA la kusikiliza, kutambua na kuwezesha wafanyabiashara leo Septemba 3, 2025 kwenye ofisi za mamlaka hiyo.
Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwassa ametoa wito kwa Watanzania kutumia dawati hilo akitaja kuwa ni fursa adimu ambayo italeta manufaa makubwa na tija kibiashara mkoa huu.

Mkuu wa mkoa Kagera,Fatma Mwassa akizindua Ofisi za dawati maalumu la kuwawezesha wafanyabiashara.
“Kuna watu wengi wenye biashara za kubwa na kati walikuwa wamepata changamoto za kodi ila kwa kutumia dawati hili basi changamoto ziatatuliwa,” amesema.
Aidha, Mwassa amesisitiza wafanyabiashara mkoani Kagera kuhakikisha wanatafuta pia wataalamu wa masuala ya kodi ili kuwawezesha kupukana changaamoto zinazoweza kukwamisha biashara zao pamoja na kufilisika.
Kwa upande wa Meneja wa TRA Mkoa Kagera, Castro John amesema wameanzisha dawati hili maalumu kuwanusuru wafanyabiashara wadogo ambao walikuwa wanafanya katika sekta isiyo rasmi, wa kati na wakubwa.
Amesema kwa uchunguzi na takwimu nchini zinaonyesha kuwa watu wanaofanyabiashara katika sekta isiyo rasmi ndiyo kiini cha kuzalisha ajira kwa wingi.
“Sehemu kubwa ya wafanyabiashara wadogo wadogo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuto rasmishwa kwa biashara zao na kutotambuliwa na taasisi mbali mbali za serikali na za kifedha,” amesema.
John, ameongeza kuwa changamoto hizo ndiyo zimesababisha Serikali kuiagiza TRA kuanzisha dawati hilo la kuwasaidia.

Amesema hayo yote yatafanyika kupitia utoaji wa huduma za karibu kwa wafanyabiashara wote kuwapatia elimu bure na msaada sitahiki juu ya biashara wanazofanya kuwaunganisha na taasisi nyingine za kiserikali pamoja na kuwasogezea huduma karibu kwenye maeneo ya biashara zao.
“Tunategemea kuwa tutaendelea kujenga mahusiano bora na sekta binafsi ikiwemo kuhakikisha kuwa tunashiriki kikamilifu katika kuwalea na kuwahudumia ili kuona kama biashara zao zinakuwa, tumejipanga pia kufikia vikundi vyote vya wakina mama na vijana vinavyojihusisha na biashara,” amesema.
Mkazi wa Manispaa ya Bukoba na mfanyabiashara mdogo wa nafaka, Lucas Kalyamtima amesema yeye amefurahi kuona TRA wameanzisha chombo cha kuwafikia kilahisi kwa kuwapatia elimu bure na kuwawezesha kibiashara, hivyo atahakikisha anakitumia vyema kukua kibiashara na kiuchumi.