Dar es Salaam. Ili kukabiliana na ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi ambacho kimekuwa kilio cha muda mrefu, Chama cha Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Tanzania (Tucasa) kimependekeza kutungwa kwa sheria ya malipo (Sopa) itakayozibana taasisi kulipa madeni kwa mujibu wa mkataba.
Mbali na kulipa madeni pia sheria hiyo imetajwa kuwa kichocheo chai mchango wa sekta ya ujenzi katika pato la Taifa, kufungua fursa za ajira na kuvuta wawekezaji.
Hayo yamesemwa leo Septemba 3, 2025 katika mkutano wa makandarasi ulioandaliwa na Tucasa uliofanyika jijini hapa.
Mwenyekiti wa Tucasa, Samwel Marwa amesema tafiti zinaonyesha kuwa uwepo wa Sopa utapunguza bei za utekelezaji miradi katika soko hali itakayowezesha Serikali kufanya kazi nyingi zaidi kuliko.
“Kwa sasa Serikali inatumia fedha nyingi kulipa fidia ya ucheleweshaji wa malipo, fedha ambayo ingeweza kutumika kujenga miradi mingine. Pia, mkandarasi anapokupa bei inakuwa ya ushindani hali itakayoshusha gharama za utekelezaji wa miradi,” amesema.
Hilo pia itachangia kuleta ufanisi katika sekta nyingine kwani malipo yanapotolewa kwa wakati yatachochea ongezeko la malipo ya kodi, kusisimua manunuzi, kukuza ajira na kusaidia kupunguza ombwe lililopo la vijana kukaa mtaani baada ya kumaliza chuo.
“Kwa hali iliyopo sasa makampuni yanashindwa kuhudumia wafanyakazi wake na kuwapunguza wengine, lakini wakiwa wanalipwa kwa wakati wataajiri zaidi. Hii pia itasaidia kuona thamani ya fedha miradi inapotekelezwa,” amesema.
Uwepo wa sheria hiyo pia utasaidia kupunguza migogoro kati ya wakandarasi na taasisi mbalimbali ambayo kwa sasa inabeba asilimia kubwa ya mashauri yote.
Sheria hiyo pia itasaidia kuvutia uwekezaji wa ndani na nje kwani watakuwa na imani ya soko hali itakayofanya nchi kusonga mbele hali itakayoondoa ulazima wa nchi kuendelea kukopa kutokana na kuwa na uwezo wa kutengeneza fedha nyingi.
Amesema ulipaji wa madeni kwa wakati itasaidia pia wakandarasi kufanya kazi kwa moyo tofauti na wale wanaotekeleza miradi mbalimbali huku wakiwa hawana uhakika wa lini watalipwa.
Pia, ili kukabiliana na changamoto za wakandarasi wazawa kupata mitaji waliitaka Serikali kuja na benki maalumu ya wakandarasi ambayo baadaye itakapokuwa inaweza kuachwa chini ya watu binafsi.
Awali, alipokiwa akizitaja changamoto wanazokabiliana nazo Marwa amesema mbali na kuchelewa kwa malipo pia uwepo kodi zisizo rafiki ikiwemo ile ya Ongezeko la Thamani (VAT) pia ni changamoto.
Amesema kodi hiyo inamtaka mtu kulipa VAT anapotoa ‘invoice’ ambayo hata yeye hana uhakika italipwa lini na inaweza kuchukua miezi sita au mwaka.
Pia, alilia na ukosefu wa mitaji kwa makandarasi wa chini na kati hali inayowafanya wanakosa fedha za kununua vifaa vya kisasa hivyo wanashindwa kushindana katika soko.
“Pia, miradi mingi inatekelezwa nchini lakini mingi wanapewa wageni hali inayofanya wakandarasi wa ndani washindwe kupata uzoefu na mapato ya biashara,” amesema.
Amesema hilo limasababishwa na ushindani usiokuwa wa haki kati ya wageni na wazawa hali inayofanya asilimia 70 ya thamani ya kazi zote nchini kufanywa na wageni wakati ambao takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia mbili pekee ya makandarasi wote waliosajiliwa nchini ndiyo wageni.
“Kuna jambo linalopaswa kufanyiwa mabadiliko kwani haiwezekani kuwa wageni ndiyo walizaliwa kuweza kuliko wenyeji. Lazima kuwepo juhudi za makusudi kuangalia tatizo ni lifanyiwe utatuzi ili makandarasi wa ndani waweze kushiriki katkka ujenzi wa nchi,” amesema Marwa.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema wanatambua uwepo wa madeni ya makandarasi waliotekeleza miradi katika maeneo mbalimbali na wameanza kuchukua hatua za kuyalipa hasa yale ya muda mrefu.
“Kati ya Julai na Agosti mwaka huu tumeshalipa zaidi ya Sh100 bilioni za Tanzania na kati ya Sh60 hadi Sh50 zimekwenda kwenye mikoa kwa ajili ya kulipa wakandarasi wa ndani,” amesema.
Lengo la kifanya hivyo ni kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali inayojitokeza ili kuongexa ushiriki wao katika sekta.
Ulega pia amesema wamepokea mapendekezo ya kuundwa kwa sheria ya ulipaji wa madeni na watakwenda kukaa na wataalamu ili kushauriana juu ya namna suala hilo linavyoweza kutekelezwa.
Serikali itaendelea kuhakikisha wakandarasi wa ndani wanashiriki kikamilifu katika miradi mikubwa kama ilivyo azma yake sambamba na kuhakikisha sheria inayotaka wakandarasi wa ndani kupewa tenda ya miradi isiyozidi Sh50 bilioni inasimamiwa kikamilifu.
“Na hii itasaidia kuhakikisha wakandarasi wetu wa ndani wanasimama, wanashindana na kushiriki kikamlifu katika utekelezaji wa miradi hii,” amesema Ulega.