Hata hivyo, mwaka huu kuna tofauti kubwa: Chama tawala CCM kinatarajiwa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu bila kukutana uso kwa uso na Chadema, mpinzani wake wa jadi. Ni kama Simba kucheza fainali na Yanga, halafu mmoja wao asitokeze uwanjani kwa sababu ya kutoridhishwa na kanuni za mchezo au kumkataa refa. Inafanana kidogo na “Dabi” ya Kariakoo iliyowahi kutokea hivi karibuni.
Kwa wafuasi wa siasa, hili ni tukio la kusikitisha na la kuchekesha kwa wakati mmoja. Kwanza, unaona jinsi mchakato unavyogeuka kuwa kama filamu ya Nollywood; kila siku kuna visa vipya. Chadema, chama kikuu cha upinzani, kipo pembeni kutokana na madai ya kushikilia “No Retreat No Surrender”. Mungu wangu! Nilitaka kusema “No Reform No Election”. Sawa na timu kudai wabadilishe refa kabla hajatia kwato uwanjani.
Lakini bado kuna kiini cha mchezo. Staa wa Chadema, Tundu Lissu anayeitaka nyumba ya Magogoni, bado yuko Mahakamani akikabiliana na kesi ya uhaini. Kesi yenyewe imekuwa kama mfululizo wa tamthilia vya runinga ambapo kila siku mfuatiliaji hukatizwa na tukio la kusisimua kwenye kila kipande kinachotangulia. Hivyo analazimika kusubiri kipande kinachofuata apate mwendelezo.
Kwa upande mwingine ACT Wazalendo, chama kilichojitokeza kama kimbilio jipya la wapinzani waliokata tamaa na Chadema nacho kimegonga kisiki kikiwa safarini. Tume Huru ya Uchaguzi imebainisha kwamba mgombea wao wa urais hakujiunga na chama mapema kama kanuni zinavyotaka. Hapa unaweza kujiuliza, hivi kweli mtu anataka kugombea urais halafu anasahau sharti dogo kama la siku saba?
Historia inatufundisha kwamba vyama vidogo vya upinzani mara kwa mara vimekuwa kama vijiti vidogo vinavyonasa kwenye tairi la baiskeli ya CCM. NCCR Mageuzi ilishawahi kuwa mwiba mchungu, CUF nayo iliwahi kutingisha, TLP nayo ikatikisa. Kila chama kilipata muda wake kwenye hadhira na kikaacha alama. Lakini sasa, vyama hivi vinabaki kama magwiji waliostaafu ambao wanaanza kila stori na neno “enzi zetu”.
Kwa macho ya haraka, unaweza kuona uchaguzi wa mwaka huu utakuwa rahisi sana kwa chama tawala. Vyama vya upinzani vimevurugika, wagombea wao wameshikwa shati na kanuni, na wengine wapo kwenye foleni ya Mahakama. Ni kama mchezo wa soka ambapo timu pinzani imeingia na kikosi cha pili, huku wachezaji nyota wakiwa benchi kwa sababu ya kadi nyekundu.
Lakini tusije tukadanganyika. Hata kama upinzani haumo rasmi kwenye majukwaa ya kampeni, sauti zao bado zipo mitaani, kwenye mitandao ya kijamii, na kwenye vijiwe vya kahawa. Stori kubwa ni “tumenyimwa haki”, “kanuni zimegeuzwa” na “mizani haiko sawa”. Hapa ndipo upinzani wa kweli unapoibuka nje ya karatasi za kura, ndani mioyo ya wananchi wanaohisi wamenyimwa nafasi ya kushuhudia pambano la haki.
Kwa hiyo, uchaguzi huu unaweza kuonekana rahisi kwa CCM. Lakini kiuhalisia unaweza kuwa mgumu zaidi. Mgumu si kwa sababu kuna mpinzani wa nguvu anayeinua mikono hadharani, bali kwa sababu kuna mzuka wa upinzani usioonekana unaotembea mitaani. Hali hii ni hatari zaidi kuliko kupambana na mpinzani anayeonekana, kwa sababu inaleta swali la msingi: Je, wananchi wataendelea kuwa watazamaji au wataanza kuhoji mfumo wenyewe?
Na hapa ndipo mzaha unageuka kuwa jambo la kushtua. Ni rahisi kucheka kwamba chama kimoja kimeshindwa kufuata kanuni za siku saba, au kwamba kingine kipo mahakamani badala ya uwanjani. Lakini ukweli mchungu ni kwamba uchaguzi bila washindani halisi unageuka kuwa kama shindano la muziki lenye bendi moja. Unaweza kuimba na kucheza mwanzo, lakini mwisho wa siku mashabiki wanachoka kusikia sauti ile ile.
Kila mtu na kila asasi inayoguswa na uchaguzi ipo roho juu kwa sasa. Mbilinge za uchaguzi zimewagawa watu kwenye makundi tofauti. Hawa wanawaona wale kuwa madikteta wasiothamini haki za mtu, wakati wale wanawaona wenzao kuwa wakaidi na watukutu. Makundi haya hayawezi kuketi jamvi moja na kusuluhisha tofauti zao, bali kila kundi linafanya mikakati ya ushindi.
Sisi yetu macho, lakini wakati hauwezi kutazama bila kuongea. Hatuusubiri wakati uongee kwa kuogopa uchungu wa maneno yake, lakini tunalazimika kuusubiri uongee kwa kuwa hatuna jinsi. Tutafanyaje wakati tunajua kuwa mafahali wawili wanapopambana, sisi manyasi ndio tutakaopondeka. Fahali ana tofauti gani na tajiri aliyeamua “bora punda afe lakini mzigo wangu ufike”.
Kaulimbiu za vyama vya siasa, wanachama wake, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla zinasisitiza amani kuelekea na katika Uchaguzi Mkuu. Lakini wote wanaanza na maombi ya uchaguzi huru na wa haki. Hili ndilo jambo muhimu kuliko kitu chochote kwa sasa, na kwa wakati ujao. Kila kisiki king’olewe na kila shimo lisawazishwe; kwa maana ya pande zote zitende na kutendewa haki.