UCHAMBUZI WA MALOTO: CUF 2025 inamtoa chozi Seif kaburini, Profesa Lipumba akishika tama

Agosti 31, 2025, Viwanja vya Furahisha, Mwanza, ulifanyika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo. Hali ya mkutano inatafakarisha. Inasikitisha.

Mahudhurio ya watu yalikuwa kidogo. Hadhira ilitosha hema moja. Kila kitu kilidhihirisha jinsi chama hicho kilivyo na uhaba wa rasilimali. Mtu mgeni na asiyejua historia, angeadhani CUF ni chama kidogo au ni kipya kinachojaribu kujenga msuli.

Naukumbuka mwaka 2000. Uwanja wa Nyamagana, Mwanza. Mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba. Maelfu walifurika uwanjani ilikuwa CUF katika nyakati zake za kutikisa siasa za nchi.

Wakati huo, Mwenyekiti alikuwa Profesa Lipumba na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, chama kilibeba matumaini ya Watanzania. Hakuhitaji matangazo mengi, habari za mikutano ya CUF, zilitembea kama upepo. Watu walihudhuria kwa mafuriko.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin alipata kusema: “Yeyote asiyeukumbuka Umoja wa Soviet huyo hana moyo. Yeyote anayefikiria Soviet itaweza kurejea tena, huyo hana ubongo.”

Kwa nukuu hiyo, nami naeleza kuwa yeyote ambaye hakumbuki nyakati nzuri za Lipumba na Seif kufanya kazi pamoja kuijenga CUF huyo hana moyo.

Kilikuwa chama kikuu cha upinzani, kilichopelekana puta na dola. Tambo za ngangari na sera za utajirisho. Chama kilikuwa na wimbo wake (party anthem) na wafuasi wake waliimba kwa fahari kubwa.

Hotuba za Profesa Lipumba, zilichapwa kwenye magazeti. Watu walimpenda, walimtukuza na kumpamba kwa sifa kemkemu. Lipumba alikuwa kinara wa upinzani, chama kilibeba matumaini ya wapinzani.

Mwaka 2000, Profesa Lipumba alikuwa na umri wa miaka 47 tu. Ushawishi, haiba yenye nguvu na mtaji wa wafuasi ambao kwa pamoja, Lipumba na CUF walikuwa nao, ilikuwa sababu ya vyama kujiegemeza ili kupambana na CCM.

Chadema, kama mfano unaojitosheleza, walijiegemeza kwa CUF mwaka 2000. Wakati huo, hakuna ambaye aliwaza kwamba ingefika siku, chama hicho kingefanya mkutano wa kitaifa na mahudhurio ya watu yangeishia idadi ya watu wasioweza kujaza hata basi moja dogo.

Lile songombingo la aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema dhidi ya Katibu Mkuu wake, Mabere Marando, lilikuwa sababu ya chama hicho kugeuka dhaifu. Walidhani wanagombea chama, kumbe walikuwa wanakichimbia kaburi. Ndivyo kwa CUF, Profesa Lipumba alipokuwa akivutana na Maalim Seif, walijidanganya kwamba walikuwa wanagombea umiliki wa chama.

Ama kwa kujua na kulazimisha kwa makusudi, au kwa kutokujua na kupigwa upofu, hivyo kuenenda bila maarifa. Matokeo ya jumla, ndiyo CUF ilivyo sasa. Haina tena ushawishi. Imefilisika mtaji wake wa wafuasi, haina rasilimali za kutosha. Nani wa kulaumiwa?

Oktoba 16, 1953, Fidel Castro katika utetezi wake mahakamani kuhusu mashitaka ya kuishambulia kambi ya jeshi ya Moncada iliyopo Santiago de Cuba, Cuba, alitoa maelezo ya saa nne ambayo yanaitwa: “History Will Absolve Me”, “Historia Itaniweka Huru.”

Pamoja na kwamba huo ulikuwa utetezi mahakamani, lakini ndiyo hutambulika kama hotuba maarufu zaidi ya Castro wakati na baada ya kumpindua aliyekuwa Rais wa Cuba, Fulgencio Batista. Maneno hayo matatu; “Historia Itaniweka Huru” ndiyo ambayo naguswa kuyatumia katika kuwajasili wabeba lawama wa anguko la CUF je, ni nani kati ya Profesa Lipumba na Maalim Seif?

Kwa vyovyote, Profesa Lipumba na Seif wote watahukumiwa na historia kwa sababu ya kushindwa kutanguliza busara mbele.

Watu wazima waliofanya kazi kwa miaka 20, walishindwa vipi kuchukua hatua ya kukiokoa chama chao? Historia itawahukumu.

Chanzo cha kila kitu ni Uchaguzi Mkuu 2015. Cuf iliingia kwenye uchaguzi ikiwa mwanachama wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Vyama vingine vya Ukawa vilikuwa ni Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD. Chadema walimpokea aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kisha wakampa tiketi ya kuwa mgombea urais. Profesa Lipumba, hakukubali kumuunga mkono Lowassa. Seif alikubali. Mgombea wa Ukawa akawa Lowassa. Ni kwa sababu hiyo, Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF, akatimkia Rwanda. Baada ya Uchaguzi Mkuu 2020, Lipumba alirejea CUF, akidai bado ni mwenyekiti, kwani barua yake ya kujiuzulu haikuthibitishwa na Baraza Kuu CUF, kama ilivyotakiwa kikatiba.

Ukafuata mvutano mkubwa. Seif na timu yake walipinga Profesa Lipumba kurejea kuongoza chama chao. Profesa Lipumba aling’ang’aniza. Msajili wa Vyama vya Siasa alimtambua Lipumba. Maalim Seif na wenzake, walikwenda mahakamani.

Hukumu ilitoka ya Mahakama Kuu, ikamtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti halali. Seif na timu yake, ambao ndiyo upande uliokuwa na nguvu iliyokuwa inaibeba CUF, walihamia ACT-Wazalendo. CUF ikageuka chama mahame. Kikapoteza nuru na ushawishi kijamii.

Kuna ile hadithi inayohusu mama wawili waliokuwa wanagombea mtoto. Kila mmoja akisisitiza ni wake. Kesi ilipofika kwa mfalme, aliamuru yule mtoto akatwe katikati ili kila mmoja achukue nusu.

Mama halisi wa yule mtoto kusikia hivyo, alimwomba mfalme mtoto asikatwe katikati, kwani yupo tayari kumkosa, lakini awe hai na mzima kisha alelewe na mwanamke mwenzake aliyekuwa akidai kuwa naye ni mama halali wa mtoto.

Mama ambaye hakuwa halisi alikubali mtoto akatwe katikati ili kila mmoja abebe kipande chake. Basi mfalme akatambua kuwa mama aliyekataa mtoto asikatwe vipande viwili ndiye mama mzazi, hivyo akaamuru apewe mwanawe.

Sababu ya mama halisi kukataa mtoto asikatwe vipande ni ule uchungu wa uzazi. Uchungu wa mwana. Mama mzazi anaweza vipi kuruhusu mtoto wake akatwe vipande viwili? Heri alelewe na mwingine, lakini abaki hai na salama.

Profesa Lipumba na Maalim Seif, hakuna aliyewaza sawa na mama mzazi wa CUF. Wote walipambana na kukubali, bora chama hicho kipasuka pande mbili, kipoteze uhai, kuliko kujitazama wao wenyewe na kukubali kukosa. Walisema “tukose wote.”

Maalim Seif aliijua nguvu yake, kwamba endapo angeondoka CUF, chama hicho kisingebaki hai, na akakubali kife, akaondoka na timu yake kubwa, kisha wakatimkia ACT-Wazalendo kwa mbwembwe na tambo za “Shusha Tanga, Anua Tanga.”

Profesa Lipumba alitambua msuli wa Maalim Seif. Alijua fika kuwa endapo mwanasiasa huyo gwiji Zanzibar angeondoka, CUF isingebaki imara tena. Alitambua kuwa chama kilimhitaji sana Maalim Seif. Pamoja na hivyo, alikubali wagombane, na aliona sawa Seif kutimka, ACT-Wazalendo ikanufaika.

Maalim Seif alipokea wito wa kifo Februari 17, 2021. Bila shaka, akiwa kaburini, kama Mwenyezi Mungu anampa uoni na kuyaona yanayoendelea kwenye siasa za Tanzania kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, atakuwa anatoa chozi, kuiona hali ya CUF, akikubuka nyakati chama hicho kilipokuwa jukwaa lao la makabiliano ya dola kisiasa.

Upande wa Profesa Lipumba, yeye yupo hai. Bado ni Mwenyekiti wa CUF. Hata hivyo, anaporejea zama hizo CUF kikiwa chama tishio, yeye akiwa mwenyekiti na mgombea urais, anapokumbuka mvutano wake na Seif ulivyodidimiza chama, bila shaka, hasemi, ila anashika tama. Inaumiza kuiona CUF ile tishio katika hali ya sasa.