“Kigoomaaa aeeh Kigoma weeeyaa, leka dutigite wishava meneke, tunayo furaha kuwa wazawa wa Kigoma, leka dutigite wishava meneke,” ni kiitikio cha wimbo “Leka Dutigite.”
Ulikuwa mradi wa mahaba ya Mkoa wa Kigoma, ulioasisiwa na Zitto Kabwe, ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kwa tiketi ya Chadema. Mradi ulishirikisha wanamuziki wenye asili ya Mkoa wa Kigoma.
Linex mpaka Mwasiti. Diamond Platnumz hadi Rachel. Ommy Dimpoz na Makomando. Baba Levo kisha Queen Darleen. Wamo pia Banana Zoro, Chege, Peter Msechu na Abdu Kiba. Waliitwa (walijiita), Kigoma All Stars.
Aliongezeka pia Alikiba na Maunda Zoro. Kigoma All Stars walifanya nyimbo mbili, halafu wakapewa mradi wa kuimba wimbo wa “NSSF”, kuhamasisha hifadhi ya jamii. Kisha, hakuna tena mradi ulioendelea wa Kigoma All Stars.
Moja ya mambo ya kukumbuka, katika video ya Leka Dutigite, Baba Levo alikuwa amevaa fulana yenye picha kubwa ya Zitto, ikiwa na maandishi “Leka Dutigite.” Lingine ni tamasha kubwa la Kigoma All Stars, lililofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Mafuriko ya watu ni rekodi ambayo itachukua miaka mingi kuvunjwa. Wabunge wa majimbo mbalimbali, hata wasiokuwa wa Kigoma, walihudhuria tamasha hilo.
Lilikuwa tamasha lililodhihirisha taswira ya nguvu ya Zitto, kisiasa, kijamii, kimipango, kimikakati na kiuratibu.
Ungeweza kudhani kuwa endapo ungemgusa Zitto, basi ungekutana na hasira za wasanii wa Kigoma All Stars. Inawezekana ungeamini kuwa kwa ushawishi aliokuwa nao, ingechukua dahari na dahari, kumkabili Zitto na kumshinda.
Ulikuwa wakati ambao jina la Zitto lilijadiliwa katika ngazi ya urais. Shida ilikuwa umri. Nakumbuka mwaka 2013, nikiwa kiongozi kwenye taasisi moja ya habari, tulialika kura za maoni, Watanzania wao wenyewe bila kupewa majina ya kuwaongoza, waseme nani angefaa kuwa Rais wao.
Majumuisho ya kura za tovuti pamoja na SMS, Zitto aliongoza mbele ya wanasiasa na watu wengine mashuhuri Tanzania. Tena kwa kura nyingi. Ilikuwa wazi kuwa Zitto, alikuwa anakwamishwa na umri tu.
Alikuwa mdogo, hivyo Katiba haikuwa ikimpa fursa ya kuwania urais. Nazungumzia nyakati ambazo Zitto alikuwa moto wa kuotea mbali.
Nakumbuka andiko la Profesa Kitila Mkumbo, “Zitto Kabwe mgombea ambaye hatagombea, mhanga wa mafanikio yake”. Profesa Kitila alichambua wasifu wa Zitto, jinsi alivyo na sifa nyingi nzuri kuwa Rais wa Tanzania, lakini hakuwa na uwezo wa kugombea Uchaguzi Mkuu 2015 kwa sababu ya kuwa chini ya umri.
Mwaka 2015, Zitto alifukuzwa Chadema na kupanda basi jipya, chama kipya, ACT-Wazalendo. Ni hapo Zitto akaanza kukumbana na upweke. Zitto wa ACT-Wazalendo kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, hakuwa yule aliyekusanya halaiki Lake Tanganyika Stadium.
Ooh, Baba Levo ni mgombea udiwani, Kata ya Mwanga Kaskazini, Kigoma. Kata ambayo mimi nimezaliwa na kukulia. Kata ya nyumbani. Zitto alimshika mkono Baba Levo, akaaminika, akachaguliwa kuwa diwani. Tiketi ni ACT-Wazalendo.
Nakumbuka siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015, nilikutana na Baba Levo. Akaniambia: “Watu wote wamemkimbia kaka (Zitto). Mimi peke yangu ndiye nimeamua kusimama naye.” Ilikuwa kweli, hakuna mwana Kigoma All Stars aliyejiweka karibu na Zitto aliyefukuzwa Chadema. Baba Levo peke yake.
Kipindi chote cha udiwani wake, ungemsikia mara kwa mara Baba Levo akimsifu Zitto kwa kila aina ya mapambio. Hata udiwani uliposhindikana baada ya Uchaguzi Mkuu 2020, Baba Levo alionekana kuwa mtiifu wa Zitto.
Ghafla, Uchaguzi Mkuu 2025, unaleta tamthiliya tofauti. Baba Levo, kijana wa Zitto, vitani na Zitto, wanawania ubunge wa Kigoma Mjini. Ukimsikiliza Baba Levo, unamwelewa dhahiri kwamba hatanii. Ni kweli haivi kabisa na Zitto.
Mwaka mmoja nyuma, ungeniuliza kama Baba Levo angeweza kuingia ulingoni dhidi ya Zitto, ningekataa mpaka mwisho. Na ningeweza kula yamini kwa kujiamini kwamba kama dunia yote ingechagua kumgeuka Zitto, basi Baba Levo angekuwa miongoni mwa wale wa mwisho kabisa.
Tumeaswa kutowatumainia binadamu. Inafundishwa pia kwamba, binadamu anaweza kubadilika na kuwa tofauti kabisa kila baada ya wiki mbili.
Hivyo, haishangazi. Dunia ya ushuhuda wa Thomas Sankara kuuawa na rafiki yake chanda na pete, Blaise Compaore, Burkina Faso. Francisco Nguema kupinduliwa na mpwa wake, Teodoro Nguema.
Sasa, unasikiliza tambo za Baba Levo kuwa Diamond Platnumz, atakwenda Kigoma kumsaidia kampeni.
Maana yake ni mapambano dhidi ya Zitto. Yaani, waliomwacha mpweke Zitto mwaka 2015, mwaka 2025, wanajipiga kifua kumnyoosha asipate ubunge.
Kutoka kwa Baba Levo, Diamond hadi maswahiba wa zamani wa Zitto, nataka nichokonoe mjadala.
Je, ni Zitto ndiye anasalitiwa au ni yeye hajui kulinda uhusiano? Kuna mahali huwa anakosea au kujisahau, kwa hiyo analipa gharama?
Zilishapita nyakati, muda wote Zitto na David Kafulila (Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia baina ya Sekta Binafsi na Umma), walionekana kuchangia misimamo. Ungemsoma Kafulila katika maandiko akimkingia kifua Zitto. Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, waliachana njia.
Wakati Kafulila alionekana angejiunga na ACT-Wazalendo, kuunda timu moja na Zitto, hakuhama. Uchaguzi Mkuu 2015 ulipomalizika, Zitto na Kafulila wakawa mithili ya paka na chui. Hawakutazamana vema, hawakuzungumziana mema.
Orodha yako mwongeze Habibu Mchange. Mwanasiasa aliyechipukia Chadema, kisha akaungana na ACT-Wazalendo.
Baada ya Uchaguzi Mkuu 2015, Mchange alitangaza kujiondoa kwenye chama hicho. Halafu, gazeti la Mchange, lililokuwa linatetea agenda za ACT-Wazalendo, likageuka na kumshughulikia Zitto.
Tafakari, nguvu kubwa ambayo Zitto alikuwa nayo Chadema, ule uungwaji mkono, ulipotelea wapi? Mitandaoni, ulishakuwepo wakati, ukiandika chochote kibaya dhidi ya Zitto, kuna vijana wangekushughulikia na kukushughulisha kisawa.
Mbona siku zinakwenda haraka? Leo hii Zitto anaweza kubabuliwa mitandaoni, watu wa kumtetea hakuna. Mpweke kabisa. Je, amepoteza ufuasi au wafuasi wake wamechoka kumpigania? Vipi, wafuasi bado wapo ila wanadharau mashambulizi?
Tatizo ni lipi? Zitto ana damu ya kusalitiwa na kila mtu au ni yeye ndiye hajui jinsi ya kulea na kulinda uhusiano? Zitto anayo nafasi ya kufanya mapitio ya watu wake wa karibu alioachana nao njiani; Samson Mwigamba, kutoka mtiifu na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, hadi kuwa mpinga Zitto. Shida ni nini?
