Dar es Salaam. Katika kuelekea maendeleo ya elimu kwa kutumia teknolojia ya kidijitali, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) kwa kushirikina na Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal cha nchini China, wamefungua Kituo cha ushirikiano wa elimu ya kidijitali mahususi kwa ajili ya kuwapatia mafunzo walimu.
Kituo hicho kitakachoitwa ‘China-Africa Regional Centre for Digital Education Cooperation’, kimezinduliwa, uzinduzi ulioenda sambamba na ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo walimu katika masuala ya digitali kutoka Wilaya ya Kinondoni na Ubungo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Makamu Mkuu wa Udsm anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface amesema kuanzisha kituo hicho chuoni hapo kwao ni heshima kubwa na kueleza kuwa ni hatua muhimu kuelekea maendeleo ya kitekolojia.
Profesa Boniface amebainisha kuwa kuanzishwa kwake kumelenga kuimarisha ujuzi wa walimu katika mikoa mbalimbali kwa kutumia teknolojia katika kufundisha masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).
“Kituo hiki kitakuwa mfano wa mafanikio yanayoweza kupatikana pale taasisi zinaposhirikiana kushughulikia changamoto za elimu bora na yenye usawa na katika zama hizi za mabadiliko ya haraka ya teknolojia, walimu wanapaswa kuwa na uwezo wa kutumia zana za kidijitali ili kuboresha ubora wa elimu,” amesema Profesa Boniface.
Akizungumza kwa niaba ya chuo cha Zhejiang Normal University, Profesa Huang Xiao amesema kuanzishwa kwa kituo hicho kumetokana na ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi za China na Tanzania katika nyanja za elimu ya kidijitali na sayansi na sasa wameona pia wawatazame na walimu.
“Walimu ndio msingi wa maendeleo ya jamii, na kuwa ujuzi wa kidijitali sasa ni hitaji la lazima na sio hiari,”amesema mwakilishi huyo.
Akizungumzia kuhusu mafunzo watakaopatiwa walimu kwa siku hizo tano, Profesa Xiao amesema itahusu teknolojia ya AI, elimu ya sayansi na mbinu za ubunifu za kufundisha kutoka China huku malengo yakiwa sio tu kushiriki maarifa bali pia kukuza uwezo wa kujifunza kwa walimu wa Tanzania.
Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius upande wa China, ambao ni waratibu wa shughuli hiyo, Profesa Xiaozhen Zhang, amesema katika mafunzo hayo ya awali jumla ya walimu 90 wameshiriki huku malengo yao ni kuwafikia walimu wa kila Wilaya.
Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kinondoni, Mtundi Nyamuhanga , amesema kuanzishwa kwa kituo hicho kuna umuhimu sio tu kwa walimu wao bali na wanafunzi.
“Kama unavyojua sasa hivi kila kitu ni teknolojia na hata ufundishaji mashuleni tunakwenda kubadilisha kwa kutumia tekonolojia zaidi ikiwemo matumizi ya projekta, clip board na vifaa vingine.

“Hii inasaidia katika ufundishaji ambapo mwalimu mmoja anaweza kufundisha shule hata tano kwa wakati mmoja na hivyo kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu na nina imani itakapoenda wilaya zote italeta mabadiliko makubwa katika elimu yetu,” amesema Nyamuhanga.
Kwa upande wao walimu akiwemo Nabuzayo Ntamuti kutoka shule ya msingi Luguruni Wilaya ya Ubungo, amesema katika mafunzo hayo wana matumaini yataenda kufanya mapinduzi makubwa kwao na kwa wanafunzi wanapokuwa darasani.
“Tunashukuru mafaunzo haya yamekuja wakati sahihi kwani jinsi teknolojia inavyokuwa haraka nasi walimu hatuwezi kuikataa ni lazima twende nayo sambamba na mafunzo haya kwetu ni nyenzo ya kukimbia nayo na tuna imani hata wanafunzi watapokea vizuri kile tutachokuwa tumefundishwa,” amesema Nabuzayo.
Mwalimu Revocatus Gratian kutoka Shule ya Mbweni Manispaa ya Kinondoni amesema licha ya shule nyingi kuanza kufundisha kwa kutumia teknolojia ya kidigitali, bado wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo vifaa, miundombinu ya umeme na upatikanaji wa intaneti ya uhakika.
Hata hivyo amesema mafunzo hayo ana imani yanaenda kumsaidia kuweza si tu kufundisha bali pia kuwasiliana kwa urahisi na wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo maofisa elimu na wadau wengine wa elimu ili kuweza kuwatembelea kuona changamoto wanazokumbana nazo na kuweza kuwasaidia.