Upelelezi bado kesi ya polisi kupora bodaboda ‎

‎‎Moshi. Jamhuri imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro bado linaendelea na upelelezi wa kesi ya wizi wa pikipiki kwa kutumia silaha inayowakabili askari wanne wa Kitengo cha Intelijensia.

‎‎Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, Septemba 3, 2025 na mwendesha mashtaka katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali Jackson Matowo, wakati kesi ilipotajwa kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya upelelezi.

‎‎Askari hao wanaoshtakiwa kwa kosa hilo katika kesi  inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ally Mkama ni G.2478 Ramadhan Jumanne, F.7340 Goodluck Richard, G.654 Zakayo Sanga na Victor Shelukindo, wote wakiwa na cheo cha Sajini.

‎‎Maofisa hao wenye dhamana ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo, Agosti 22, 2025.

‎‎Katika kesi hiyo ya jinai namba 20614/2025, wanakabiliwa na shtaka moja la wizi wa pikipiki kwa kutumia silaha, kinyume cha kifungu cha 287A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (PC) kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

‎‎Katika maelezo ya shtaka hilo kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyoko katika mfumo wa mashauri wa Mahakama, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 22, 2025.

‎‎Wanadaiwa kuwa siku hiyo katika eneo la Police Line ndani ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakiwa na silaha aina ya pingu, waliiba pikipiki aina ya Sinoray yenye namba za usajili MC 406 ERU, mali ya Ramadhan Singe.

‎‎Wanadaiwa kabla na baada ya kuiba pikipiki hiyo, washtakiwa walimtisha na kutumia pingu kumfunga Ramadhan ili kujipatia pikipiki hiyo.

‎‎Baada ya kusomewa shtaka, Hakimu Mkama aliahirisha kesi hiyo mpaka leo Septemba 3, 2025 na aliamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu gerezani.

‎‎Washtakiwa hao leo Septemba 3, 2025 hawakufikishwa mahakamani bali kesi imeendeshwa kwa njia ya mtandao.

‎‎Kutokana na upelelezi kutokukamilika, Wakili Matowo ameiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya upelelezi huo.

‎‎Hakimu Mkama ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 17, 2025 itakapotajwa kuona kama upelelezi utakuwa umekamilika ili kuendelea na hatua nyingine za kisheria na kuwezesha usikilizwaji kamili kuanza.

‎‎Kwa mujibu wa sheria, shtaka hilo halina dhamana, hivyo washitakiwa wataendelea kuhifadhiwa mahabusu kwa kipindi chote cha kesi hiyo.

‎‎Kabla ya maofisa hao wanne wa polisi kupandishwa kizimbani na kusomewa shtaka la wizi wa bodaboda hiyo mali ya Ramadhan, askari polisi sita mkoani Kilimanjaro walitiwa mbaroni kuhusu tukio la kutoweka dereva wa bodaboda maarufu Moshi, Deogratius Shirima (35).

‎‎Mwendesha bodaboda huyo alitoweka Julai 21, 2025 lakini pikipiki aliyokuwa akiiendesha ilidaiwa kuwa ndani ya nyumba ya mmoja wa askari hao iliyopo katika kambi ya polisi.

 Hata hivyo, mpaka leo bodaboda huyo hajapatikana na hajulikani alipo.

‎‎Jumanne Agosti 5, 2025, Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kwa simu na alipoulizwa juu ya tukio hilo na ni askari wangapi wa jeshi hilo wanashikiliwa alijibu: ‎‎“Kama tulivyosema, uchunguzi unaendelea, viongozi wakubwa tupo nao hapa.”

‎‎Ingawa Kamanda Maigwa hakufafanua zaidi viongozi hao ni kina nani, lakini taarifa za uhakika ambazo Mwananchi lilizipata zilibainisha kulikuwa na timu ya maofisa wa polisi iliyotoka makao makuu Dodoma ikiongozwa na ofisa mwenye cheo cha Kamishna.

‎‎Taarifa ambazo Mwananchi lilizipata kutoka kwa vyanzo vya upande wa mwendesha bodaboda aliyetoweka, baada ya kutoweka kwake, mmiliki wa pikipiki aliitafuta kupitia mfumo wa Global Positioning System (GPS) iliyofungwa katika pikipiki hiyo.

‎‎GPS hiyo iliwaelekeza hadi nyumbani kwa askari ndani ya kambi hiyo ya polisi.

Ramadhan ambaye pikipiki yake ndiyo inahusika katika kesi hiyo aliachwa eneo la kambi ya polisi kuangalia nyumba ilimokuwa pikipiki na kama kungekuwa na hatua yoyote ingechukuliwa dhidi ya watuhumiwa waliohusika.

‎Hata hivyo, Ramadhan alijikuta matatani baada ya polisi wawili kufika mahali alipokuwa wakamkamata, wakamfunga pingu na kumuondoa. Baadaye pikipiki ya bodaboda aliyetoweka ikahamishwa kutoka ndani ya nyumba hiyo.

‎‎Pikipiki hiyo ilikutwa imetelekezwa mtoni umbali wa kati ya kilomita tatu na saba.

‎‎Kwa mujibu wa Mariam Abdi, mke wa bodaboda aliyetoweka siku mumewe anatoweka waliachana saa 11:00 jioni na alimtaka ampigie baadaye ili ampe fedha kwa ajili ya chakula cha jioni. Muda ulipofika alipiga simu yake lakini haikupatikana tena.