Dar es Salaam. Wafugaji wa nguruwe nchini wameitwa kujadili ufugaji wa kisasa kwa kutumia teknolojia sambamba na mbinu mpya kutoka mataifa ya nje ili kuongeza uzalishaji wa nyama.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Tanzania kuna nguruwe zaidi ya milioni 4.1 hadi mwaka 2024/25 kutoka nguruwe milioni 3.9 mwaka 2023/24 ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.1.
Wito huo umetolewa na Chama cha Wafugaji Nguruwe Tanzania (Tapifa) leo Septemba 3, 2025 kwenye mkutano na waandishi wa habari kuelekea Kongamano la Kimataifa la Wafuga Nguruwe litakalofanyika kwa mara ya kwanza Tanzania kuanzia Septamba 11 hadi 13 jijini hapa.
Kiujumla sekta ya mifugo hadi mwaka 2023 inachangia takribani asilimia 6.2 ya Pato la Taifa (GDP). Pia, inatoa ajira kwa Watanzania milioni 4.6 katika mnyororo wake wa thamani na inapanuka kwa kasi ya mwaka ya asilimia tano.
Pia, katika kuuza mauzo nje ya nchi kwa ajili ya kuongeza fedha za kigeni, hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya tani 9,863.41 za nyama zimeuzwa sawa na asilimia 89.9 ya lengo la kuuza tani 10,971 ambapo kiasi hicho kinajumuisha tani 27.83 za nguruwe zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 44.07 zimeuzwa katika masoko ya nje ya nchi.
Masoko ya mauzo ya nyama ya Tanzania nje ya nchi yameendelea kupanuka na kufikia sasa nchi 11 zikiwemo Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE) na Vietnam.
Akizungumza Mwenyekiti wa Tapifa, Doreen Maro amesema kongamano hilo la kihistoria lilianza kama wazo mwaka 2022 nchini Afrika Kusini huku utekelezaji ukaanza rasmi mwaka 2023 nchini Nigeria.
Amesema zitaangaliwa, kujifunza pamoja na fursa za kupata faida kwa wafugaji ili kuongeza uzalishaji wa nyama hiyo ikiwemo mbegu mpya na mbinu za kiteknolojia.
“Mwaka huu Tanzania tumepata nafasi ya kongamano hili ambalo linazungumzia mnyororo wa thamani wa sekta ya nguruwe. Watakuwa wageni zaidi ya 250 kutoka nje ya nchi kutakuwa jumla ya washiriki 1000. Tutazungumza tafiti mbalimbali ziizofanywa.
“Vyama vya wafugaji tisa kutoka nchi za nje vimekubali kushiriki. Tunapaswa kuangalia sekta hii kwa jicho la pili maana inakua kwa kasi na faida zake ni nyingi,” amesema.
Amesema ili watu wafuge vizuri lazima wakutane wajadiliane maana kuna wazalishaji wakubwa wa mbegu kutoka Ulaya watakuwepo.
“Kuleta teknolojia mpya ya ufugaji pia na mbegu na malisho hili ndio lengo la kongamano hili,” amebainisha.
Ofisa Mfawidhi Bodi ya Nyama Kanda ya Mashariki, Joseph Kulwa amesema watu wanapaswa kujihusisha katika mnyororo mzima wa nguruwe endapo wasipofungwa na miiko ya kiimani.
Akinukuu Shirika la Chakula Duniani, amezema binadamu kwa mwaka anapaswa kula nyama kilo 50 ikiwa ni mchanganyiko wa nyama nyeupe na nyekundu lakini takwimu nchini zikionesha Watanzania wanakula kilo 15 hivyo mkutano huo utajadili namna ya kuongeza uzalishaji wa nyama hiyo.
“Nahimiza watu tule nyama kwa wingi ikiwa ni wastani wa kilo moja kwa wiki,” amesema Ofsa huyo.