Waliokuwa watumishi Kigamboni wapandishwa kizimbani

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Fedha na Mhasibu wa Manispaa ya Kigamboni, Jonathan Manguli (38) na wenzake 12, wakiwamo wafanyabiashara wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 10, yakiwamo ya kuchepusha fedha na kuisababishia Wizara ya Tamisemi hasara ya Sh165 milioni.

Washtakiwa wengine waliokuwa watumishi wa manispaa hiyo ni mhasibu Godfrey Martiny (44), mkuu wa kitengo cha udhibiti taka na usafi wa mazingira, Juvenalis Mauna (53), mhandisi Josephat Mutembei (39) na ofisa ugavi msaidizi, Bibiana Mdete (53).

Wengine ni ofisa ugavi, Henry Rugayi (38), mhasibu, Annie Maugo (43), ofisa hesabu kutoka Tamisemi Dodoma, Tumsifu Christopher (46) na ofisa hesabu, Aidan Mpozi (61) wote kutoka Manispaa ya Kigamboni.

Washtakiwa wengine ambao ni wafanyabiashara ni Hamis Manfred (40), Paulo Mwakyusa (43), Godwin Cheyo (33) na Jennifer Manguli (30).

Washtakiwa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Septemba 3, 2025 wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 21510/2025. Wamesomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Erick Shija akishirikiana na Cathbert Mbiling’i, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.

Kabla ya washtakiwa kusomewa mashtaka, Hakimu Makube aliwaeleza hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.

Baadaye wakili Shija aliieleza Mahakama kuwa, washtakiwa wapo mbele ya Mahakama isipokuwa wanane na wa tisa (Kachira na Mpozi) ambao wana kesi nyingine mkoani, hivyo anaomba watarejeshwa Dar es Salaam kusomewa mashtaka na kuunganishwa na wenzao.

Makube alikubali ombi la upande mashtaka na kuelekeza washtakiwa waliopo mahakamani wasomewa mashtaka.

Kati ya mashtaka 10 yanayowakabili, matatu ni ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumpotosha mwajiri wao, mawili ya kuongoza genge la uhalifu, mawili ya ubadhirifu wa fedha, moja la kuchepusha fedha, kutakatisha fedha na kuisababishia hasara Tamisemi.

Katika shtaka la kwanza la kuongoza genge la uhalifu, Manguli, Martiny, Mauna, Mutembei, Rugayi, Maugo na Kachira, wanadaiwa kati ya Julai mosi, 2022 na Desemba 30, 2023 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na Dodoma, wakiwa watumishi wa umma kwa kuvunja sheria na kushindwa kutimiza majukumu yao, walifanya ubadhirifu wa Sh165 milioni.

Shtaka la pili la kuongoza genge la uhalifu Manifred, Mwankyusa, Cheyo na Manguli wanadaiwa kati ya Julai mosi, 2022 na Desemba 30, 2023 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kushirikiana na watumishi wa umma walifanya ubadhirifu wa Sh165 milioni.

Shtaka la tatu ni la kuchepusha fedha Maugo, Kachira na Mpozi, wakidaiwa kati ya Julai mosi, 2022 na Septemba 5, 2023 katika ofisi za Tamisemi Dodoma, wakiwa wahasibu, kwa masilahi binafsi walichapisha na kuhamisha Sh169 milioni, zilizokuwa zitumike kwenye miradi ya Tamisemi.

Katika shtaka la nne la ubadhirifu Manguli, Martiny na Mauna wanadaiwa kati ya Septemba 5, 2022 na Desemba 30, 2023 kwenye ofisi za Manispaa ya Kigamboni, wakiwa watumishi wa manispaa hiyo, kwa nyadhifa zao za uhasibu, mkuu wa idara ya fedha na mkuu wa idara ya udhibiti taka na usafi wa mazingira, walibadilisha matumizi ya Sh128 milioni kwa masilahi yao binafsi.

Pia, katika shtaka la tano wanadaiwa kati ya Septemba 5, 2022 na Desemba 30, 2023 katika ofisi za Manispaa ya Kigamboni, walifanya ubadhirifu kwa kubadilisha matumizi ya Sh36.8 milioni.

Shtaka la sita ni la matumizi ya nyaraka kwa nia ya kumpotosha mwajiri wao (Manispaa ya Kigamboni), ambalo Manguli na Mutembei wanadaiwa Februari 2, 2023 katika ofisi za manispaa hiyo, kwa nyadhifa zao kwa nia ovu na kwa makusudi walimdanganya mwajiri wakitumia nyaraka yenye taarifa zisizo sahihi za ukaguzi wa vifaa, kuonesha mkandarasi ameshusha tripu 220 za moramu na kukodi greda kutoka Kampuni ya Konya Investment Co Ltd, wakijua wanampotosha mwajiri wao.

Wakili Shija katika shtaka la saba amedai ni la matumizi ya nyaraka kwa nia ya kumposha mwajiri, ambalo Mdete anadaiwa Februari 2, 2023 katika ofisi za Manispaa ya Kigamboni, akiwa ofisa ugavi msaidizi, kwa nia ovu dhidi ya mwajiri wake, alitumia nyaraka yenye taarifa potofu ya vifaa kuonesha mkandarasi ameshusha tripu 220 za moramu na kukodi greda kutoka Kampuni ya Konya Investment Co Ltd, wakati akijua anampotosha mwajiri wake.

Vilevile, Rugayi katika shtaka la nane anadaiwa Machi 27, 2023 katika ofisi za manispaa hiyo, akiwa ofisa ugavi aliwasilisha nyaraka na taarifa potofu ya vifaa, akionesha Kampuni ya Mbogholo Investment imepeleka tripu ya moramu kwenye lori moja la futi 12 na kukodi greda.

Shtaka la tisa ni la kutakatisha fedha linalowakabili wengine isipokuwa mshtakiwa wa tano (Mdete), wakidaiwa kati ya Julai mosi, 2022 na Desemba 30, 2025 jijini Dar es Salaam na Dodoma, walijihusisha na muamala wa Sh165 milioni, wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la uchepushaji fedha.

Katika shtaka la 10 wote wanadaiwa kuwa, wakifahamu na kwa nia ovu waliisababishia hasara Tamisemi ya Sh165 milioni.

Upande wa mashtaka ulidai upelelezi umekamilika na kuomba tarehe kwa ajili ya kusajili taarifa muhimu Mahakama Kuu.

Mdete, kupitia wakili wake aliiomba Mahakama impe dhamana kutokana na mashtaka yanayomkabili kudhaminika kisheria.

Hakimu Makube alikubali ombi la Mdete na kutoa masharti ya dhamana, akitaka wawe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh20 milioni.

Pia, wawe na vitambulisho kutoka Serikali ya mtaa.

Hata hivyo, Mdete ameshindwa kutimiza masharti hayo, hivyo amepelekwa rumande pamoja na washtakiwa wengine.

Kesi imeahirishwa hadi Septemba 9, 2025 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo upande wa mashtaka utakuwa umeshasajili nyaraka Mahakama Kuu.

Washtakiwa wameomba Mahakama iruhusu wapelekwe mahabusu Gereza la Keko kwa kuwa huko ndiko wameacha vitu vyao.

Awali, washtakiwa hao walikuwa na kesi ya jinai Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, ambayo jana Septemba 2, 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliifuta, kisha walikamatwa na kufikishwa Mahakama ya Kisutu.