Wananchi Tunduma waeleza matumaini yao kwa Samia, wamtaka ayafanye haya

Tunduma. Wananchi wa Tunduma wameeleza matumaini yao kwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan huku wakimtaja mambo ambayo wangependa ayafanyie katika katika mji huo endapo atafanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuwajengea barabara za ndani za lami ili kupunguza vumbi, kupunguza utitiri wa kodi pamoja na kuwapatia vitambulisho vya Taifa.

Wananchi hao wameeleza hayo leo Septemba 3, 2025 kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CCM, Samia, unaofanyika mjini Tunduma ikiwa ni mkutano wake wa kwanza katika Mkoa wa Songwe.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo wameeleza matumaini yao kwa mgombea huyo huku wakimtaka afanyie kazi baadhi ya changamoto zinazowakabili.

Mkazi wa Tunduma, Eliud Mwashitete amesema wameona kazi kubwa ambayo Serikali umefanya kwenye elimu na afya, hata hivyo ameomba wajengewe barabara za lami ndani ya mji huo ili kuupendezesha na kupunguza vumbi lililopo.

“Tunaomba pia barabara yetu kuu ya Tunduma – Mbeya ipanuliwe kwa sababu imekuwa ikisababisha msongamano wa magari hasa malori yanayokwenda Zambia,” ameongeza mkazi huyo wa Tunduma.

Kwa upande wake, Bosco Zakaria amesema amekuwa akifuafulia kitambulisho cha Taifa lakini mpaka leo hajapewa, anamuomba mgombea huyo awasaidie katika changamoto hiyo akichaguliwa kwa mara nyingine.

“Nimekuwa nikifuatilia kitambulisho changu kwa miaka miwili sasa lakini sijakipata, namuomba mama (Samia) atusaidie tupate hivyo vitambulisho kwani kuna maeneo tunakwama.

Mwananchi huyo ambaye ni kada wa CCM, amempongeza mgombea huyo kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka minne iliyopita kwani wamejengewa madarasa, zahanati na vituo vya afya.

Mfanyabiashara katika mji wa Tunduma, Nolasco Kaduma amemtaka mgombea wa CCM kuhakikisha kwamba suala la kodi linasimamiwa vizuri na zile zisizo za msingi ziondolewe ili wafanye biashara kwa amani na furaha kama Watanzania.

“Kodi tunazolipa ni nyingi, tunaomba zipunguzwe ili nasi tupate faida. Pia, maofisa wa TRA (Mamlaka ya Mapato) wawe waungwana wanapokuja kufuatilia hizo kodi, baadhi yao ni wasumbufu, wanatengeneza mazingira ya rushwa,” amesema mfanyabiashara huyo.

Mkulima, Consolata Mamboleo amempongeza Rais Samia kwa kuwapelekea miradi ya madarasa na vituo vya afya kwani sasa watoto wao wanakaa kwenye madawati na wanapata huduma bora za afya.

“Sisi wakulima wa kahawa tunaomba fedha zetu kwenye vyama vya ushirika zitolewe kwa wakati ili nasi tukidhi mahitaji yetu ya kila siku. Ninaamani atalifanyia kazi na Oktoba nitatiki,” amesema mwanamke huyo.