Wanawake wagombea wapewa mbinu kukabiliana na vikwazo

Unguja. Wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea katika hatua za kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa, wanawake watakaogombea nafasi za urais, uwakilishi na udiwani kupitia vyama mbalimbali kisiwani hapa wamepewa mbinu za kuzungumza na hadhira na kutokatishwa tamaa na maneno ya kejeli na vikwazo vya kiuchumi.

Akizungumza katika mafunzo hayo leo, Jumatano, Septemba 3, 2025, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa ZNZ), Dk Mzuri Issa, amesema kuna changamoto nyingi zinazowakabili wanawake katika siasa, ikiwa ni pamoja na mitazamo hasi ya kijamii kuhusu uongozi wa mwanamke.

“Changamoto za kiuchumi, pamoja na udhalilishaji wa maneno na hata ule unaotokea mitandaoni, hayapaswi kuwa kikwazo, bali chachu ya kuthibitisha kwamba wanawake tuna nguvu, uwezo na uthubutu wa kuongoza,” amesema.

Dk Mzuri amesema utafiti unaonesha viongozi wanawake ni waadilifu, wachapakazi, na wenye kujali masuala ya jamii kwa umakini mkubwa, ambapo mara nyingi hupendelea mazungumzo na maridhiano badala ya migogoro, jambo linaloleta mshikamano na manufaa kwa jamii nzima.

“Tunaiomba jamii nzima ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kuwaunga mkono wagombea wanawake katika kipindi hiki cha uchaguzi. Tuitengeneze kwa pamoja mazingira rafiki kwa wanawake na watu wenye ulemavu, ili kila raia mwenye sifa aweze kuchagua, kuchaguliwa na kushiriki ipasavyo katika mchakato mzima wa uchaguzi,” amesisitiza Dk Mzuri.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Dk Salum Suleiman Ali, amesema mwanamke kuwa kiongozi sio jambo jepesi, kwani zipo mbinu mbalimbali zinazotumika, ikiwemo masuala ya dini, na mila, kupinga wanawake kushika nafasi hizo.

“Lazima tujiandae, sio jambo dogo kusimama mbele ya umati wa wananchi ukawashawishi wakuchague, inahitaji ujasiri na nguvu bila woga ili kufanikisha jambo hilo,” amesema Dk Salum.

Amewasihi wanawake kujiandaa kwa kuzipitia sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi ili wanapokuwa wakizungumza au kudai jambo, wajue wanasimamia katika misingi gani.

Nao baadhi ya wanawake hao, wamesema changamoto kubwa inatokea kwenye michakato ya vyama, kwani wengi ndio wanapingwa na kupata anguko la kisiasa hapo.

“Bado wanaume hawajaamini kwamba mwanamke anaweza kuongoza, kwahiyo unakuta mchakato ndani ya vyama ndipo tunapoangukia, lakini mtu akifanikiwa kupenya hapo, inakuwa rahisi hata kwenye majukwaa makubwa kupenya,” amesema Mwanakhamis Msellem Ramadhan.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Khadija Ali, kutoka chama cha ACT – Wazalendo, aliyesema vyama vyote vipo hivyo, wanawake wengine wanaungana na wanaume kuwakandamiza.

Naye mwezeshaji mwingine, Halima Msellem, amesema umefika wakati wanawake kubadilisha mitazamo yao na kuacha tabia ya kubagua na kuwa na makundi, jambo linalowafanya washindwe kuungwa mkono na wengi.

“Tubadili mitazamo, tuna kasumba ya kutengeneza makundi, unaweza kuwa unataka kura ya mtu lakini wakati huo huo unamchukia, sasa utapataje kura yake? Tubadilike na tusiwe watu wa kulalamika na kujinyong’onyeza kwenye majukwaa,” amesema.

Mafunzo hayo yametolewa na wadau wa kukuza ushiriki wa wanawake katika uongozi na siasa Zanzibar, kwa kushirikiana na ubalozi wa Norway nchini Tanzania.

Pamoja na Tamwa, wadau wengine walioshirikiana ni Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (Juwauza), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela), na Jumuiya ya Mazingira na Utetezi wa Kijinsia Pemba (Pegao).a