WACHEZAJI wanne kutoka JKT, Dar City, Tausi Royals na DB Troncatti walikuwa kivutio katika robo fainali ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) kutokana na kuwa na uwezo mzuri wa kucheza na kuchezesha timu katika nafasi zao, mambo ambayo yalizibeba na kuziwezesha kushinda.
Wachezaji hao Omary Sadick (JKT), Amin Mkosa (Dar City), Juliana Sambwe (Tausi Royals) na Jesca Lenga, ambapo Sadick anayecheza kama namba mbili maarufu shooting guard akiiwezesha JKT kuifumua timu kongwe ya Savio katika michezo 2-0.
Uwezo wa kupenya na kuchezesha timu aliouonyesha katika robo fainali hizo mbili ambapo aliongoza kumiliki mpira bila ya kupokonywa kirahisi na wapinzani wao.
Katika robo fainali ya kwanza Sadick alifunga pointi 20 na asisti 10, ilhali ile ya pili alifunga pointi 21 na kutoa asisti mara 12. Shooting guard ni mchezaji mwenye uwezo wa kufunga upande wa mitupo ya mbali, lakini kwa upande wake pia alionekana katika kukaba na kupokonya mipira.
Kwa upande wa Mkosa anayecheza namba tatu inayokwenda kimchezo wa kikapu kama small forward aliongoza kufunga pointi akitokea kwenye kona ya goli la timu pinzani wao akiinyanyasa vilivyo ngome ya wapinzani wao. Namba 3 maarufu kama small foward inachezwa na mchezaji mwenye uwezo wa kukimbia haraka na kufunga (faast break).

Sifa hiyo kwa Mkosa aliionyesha katika robo fainali, lakini mara nyingi pia alionekana akicheza kama mchezaji huru kwenye nafasi zote uwanjani.
Naye Juliana anayecheza namba moja (point guard), aliiunganisha vizuri Tausi Royals uwanjani, ambapo alikuwa mjanja kupenya mbele ya walinzi na kutoa pasi kwa wafungaji wa timu yake. Ingawa kazi hiyo ilikuwa ngumu kwake, lakini kila mara alionekana akihaha katika eneo la wapinzani kusaka ushindi.
Jesca Lenga anayecheza pia namba moja (point guard) alionyesha kiwango bora katika kuiunganisha na kuituliza timu yake ikiwa inashambuliwa na pia kushambulia upande wa wapinzani wao.
‘TURN OVER’ YAZIPONZA TIMU
Baadhi ya timu zilizoshindwa kufuzu kucheza nusu fainali ya BDL zilionyesha udhaifu kwa kupoteza mipira kirahisi, jambo ambalo linaonyesha makocha wana kazi kubwa kujenga vikosi kwa ajili ya msimu ujao.
Makosa ya timu hizo kupoteza mipira yalisababisha kutoa faida kwa wapinzani wao kufunga kwa haraka (fast break). Fast break ni neno linalotumika kwenye kikapu sawa na ‘counter attack’ (shambulizi la kushtukiza) kwenye soka.

Pia kulikuwa na makosa ya kupoteza mipira yaliyosababisha timu hizo kufanya madhambi yasiyotarajia na kuzifanya kufungwa kwa mipira ya adhabu au mchezaji kutolewa nje kwa kufanya madhambi mara tano. Kilichofanya iwe hivyo ni kutokana na mchezaji kupoteza mpira, lakini anapokwenda kupora mpira anafanya hivyo kwa kutumia nguvu inayomfanya afanye madhambi.
Timu zilizofungwa kwa kupoteza mipira ni pamoja na Srelio, Savio na UDSM Outsiders. Timu ya Srelio iliyofungwa na Dar City katika robo fainali kwa michezo 2-0 katika robo fainali ya kwanza ilifungwa pointi 90-55, na robo fainali ya pili ilifungwa kwa pointi 93-72.
Katika robo fainali ya pili Srelio ilipoteza mipira kwenye ile robo ya tatu katika dakika ya 2, 4, 6 na 9 wakati Dar City ikiongoza kwa pointi 63-60, na robo ya nne ilipoteza mipira dakika za 3, 6, 7 na 8. Katika mchezo mwingine JKT iliifumua Savio katika michezo 2-0, ambapo mchezo wa kwanza ilishinda kwa pointi 74-67 na ule wa pili ikashinda kwa pointi 83-72.
Savio iliingia uwanjani kwa lengo la kulipiza kisasi cha kufungwa katika mchezo wa kwanza kwa pointi 74-67, lakini ilishindwa kulipiza kisasi, ambapo Savio ilipoteza mipira kwenye robo ya pili dakika ya 4 na 5 na ile ya nne dakika za 5, 7, 8 na 9. Katika robo fainali ya pili JKT iliongoza kwa pointi 26-23, 14-18, 18-18 na 25-13.

Nayo Stein Warriors iliyoshiriki BDL kwa mara ya kwanza ilitinga nusu fainali baada ya kuifunga UDSM Outsiders katika michezo 2-0. Robo ya fainali ya kwanza ilishinda kwa pointi 72-65, huku ile ya pili ikishinda kwa pointi 59-46. katika robo fainali ya pili, UDSM ilipoteza mipira katika robo ya tatu dakika za 2, 4 na 7 na ile ya nne ilipoteza dakika za 3, 4, 7 na 9.
KAMA ulikuwa unajiuliza kulikoni kuhusu mashindano ya kikapu ya Ligi Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam itashirikisha timu ngapi? Basi, fahamu kwamba kuna timu 25 zimeomba kushiriki mashindano hayo kwa msimu ujao.
Kamishna wa Ufundi na Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), Haleluya Kavalambi ameliambia Mwanaspoti kwamba idadi ya timu zilizoomba kushiriki mashindano hayo ni kubwa na kwamba inaonyesha namna gani mchezo huo unazidi kupata umaarufu na kuvutia mashabiki wapya.
Kavalambi alisema lengo la Chama cha Kikapu Dar es Salaam ni kuwa na timu 20 katika ligi hiyo na utaratibu uliopo ni kwa timu zitakazoshindwa kulipa ada kabla ya tarehe ya mwisho itakayotangazwa karibuni zitakuwa zimepoteza nafasi hiyo na hiyo ni kwa zile zitakazochaguliwa.

“Tumejipanga katika ligi ya mwaka huu tunataka timu zote zilipe ada. Hatutaki kuidai timu wakati ligi hiyo ikiwa inaendelea,” alisema Kavalambi bila kutaja kiasi cha fedha kinachopaswa kulipwa.
Alizitaja kati ya timu zilizoomba kushiriki kuwa ni Jogoo, KR-one, Yellow Jacket, Christ The King, UDSM Insiders, Polisi, Mbezi Beach Spurs, Dar Kings, Veins BC, Ukonga Kings na Ukonga Warriors. Zingine ni Oilers, Kigamboni Heroes, Mgulani Heroes, Tanzania Prisons, DB Magone, Kibada Riders, Cavaliers, Kigamboni Academy, LBC, Magnets na TRA Sports.
Ligi hiyo inafanyika kwa ajili ya kutafuta timu tatu zitakazopanda daraja ili kucheza BDL mwakani. Katika Ligi Daraja la Kwanza mwaka daraja, timu za Polisi, Stein Warriors na Kurasini Heat ndizo zilizopanda.