Dar es Salaam. Baada ya kuripotiwa kwa baadhi ya kesi zinazohusu matumizi mabaya ya teknolojia ya Akili Unde (AI) ya ChatGPT kwa watoto ikiwemo kusababisha madhara kama kifo.
Kampuni ya teknolojia ya OpenAI inayomiliki Akili Unde hiyo ya ChatGPT imetangaza kuja na mfumo wa udhibiti wa wazazi utakaowapa uwezo wa kuunganisha akaunti zao na za watoto ili kuona kile wanachokifanya.
OpenAI, ambayo wiki iliyopita ilitangaza hatua hiyo ya kuongeza usalama kwa watumiaji walio katika mazingira hatarishi, imesema mabadiliko hayo yataanza kutekelezwa ndani ya mwezi mmoja kutokea sasa.
Ikumbukwe hivi karibuni kuliripotiwa kesi ya kijana aliyejulikana kwa jina moja la Adam kutoka nchini Marekani kujiua kwa maelekezo ya ChatGPT.
Baada ya tukio hilo mzazi wa kijana huyo Maria Raine na mumewe, wamefungua mashtaka wakidai kuwa ChatGPT ilihimiza mtoto wao Adam kujiua.
Imeelezwa ChatGPT ilijenga uhusiano wa karibu na kijana huyo kwa miezi kadhaa kabla ya kifo chake.
Wazazi hao wanadai katika mazungumzo yao ya mwisho, ChatGPT ilimsaidia kijana huyo mwenye umri wa miaka 16 kuiba pombe kutoka kwa wazazi wake na kumpa uchambuzi wa kiufundi namna ya kufunga kitanzi huku ikimdanganya na kumthibitishia kuwa kinaweza kumbeba binadamu.
Baada ya sakata hilo sasa OpenAI imekuja na mfumo wa udhibiti wa wazazi ambapo wataweza kuunganisha akaunti zao na za watoto wao. Hii itawapa uwezo wa kudhibiti jinsi ChatGPT inavyojibu watoto wao, kwa kufuata miongozo inayofata umri wao.
Katika hilo AI hiyo pia itatuma taarifa (notifications) kwa wazazi wakati mfumo utagundua mtoto wao yuko katika hali ya shida kubwa ya kihisia.
Matumizi ya mifano ya AI na watu wenye changamoto kubwa za afya ya akili yamezua hofu, hasa inapochukua nafasi ya mshauri au rafiki.
Utafiti uliochapishwa mwezi uliopita na Psychiatric Services uligundua kwamba ChatGPT, Gemini ya Google na Claude ya Anthropic zilikuwa zinajibu maswala ya kitabibu kwa mazoea wakati wa maswali ya hatari kubwa kuhusu kujiua, lakini zilionyesha kutokuwa thabiti katika majibu kwa maswali yenye “hatari za wastani.”
Watafiti walihitimisha: “Matokeo haya yanaonyesha haja ya maboresho zaidi ili kuhakikisha zinaweza kutumika kwa usalama na ufanisi katika kutoa taarifa za afya ya akili, hasa katika hali nyeti zinazohusisha mawazo ya kujiua.”
OpenAI imesema inaendelea kuboresha jinsi mifumo yao inavyotambua na kujibu ishara za shida ya akili na hisia. Pia, wana mpango wa kuboresha usalama wa chatbots zao ndani ya miezi mitatu, ikiwemo kuelekeza “mazungumzo nyeti kwenye mfumo wa kufikiri,” ambao utatumia nguvu zaidi ya kompyuta kuzalisha majibu salama.
Mwanasheria Melodi Dincer amesema vijana wanaweza kuamini chatbot kama rafiki au daktari kwa sababu ya muundo wake ulivyo.
Hii inaweza kuwafanya kuanza kushirikisha na maisha yao ya binafsi na kutafuta ushauri kutoka kwa mfumo ambao unaonekana kuwa na majibu yote.
Mzazi Rosemary Daud kutoka Dar es Salaam amesema hatua hiyo ni njema ikilinganishwa na matumizi ya Akili Unde yanazidi kushika kasi hasa kwa watoto wenye uwezo wa kufikia vifaa janja.
Amesema utekelezaji wa mfumo huo utasaidia hata kutambua mtoto anahisia gani kulingana na kile anachokitafuta ama kuiuliza AI.