ZEC, vyama vya siasa na mustakabali wa uchaguzi

Hivi karibuni, vyama 18 vya siasa vilitia saini hati ya makubaliano ya kuendesha uchaguzi wa Zanzibar kwa misingi ya amani, uwazi na haki. Tukio hilo lilisimamiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Kazi.

Mkataba huo unalenga kuhakikisha kwamba kampeni za uchaguzi mwaka huu zinazingatia maadili ya kisiasa kwa kutumia lugha ya staha, kuepuka uchochezi, chuki, na vitisho.

Chama pekee ambacho hakikusaini makubaliano hayo, kama ilivyokuwa pia upande wa Bara, ni Chadema.

Huu si mkataba wa kwanza wa aina hii. Katika chaguzi zilizopita, makubaliano kama haya yamesainiwa mara kadhaa, lakini utekelezaji wake haujawahi kuakisi yaliyokubaliwa. Badala yake, tumeshuhudia baadhi ya wanasiasa wakitumia majukwaa ya siasa kueneza matusi, vitisho na ukandamizaji kwa wapinzani wao kwa msaada wa baadhi ya vyombo vya dola.

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, dalili za kuvunjwa kwa maadili hayo tayari zimeanza kujitokeza.

Zipo taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa mikoa na wilaya wameanza kuwashinikiza wananchi kuwapa kadi zao za kupigia kura, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Aidha, zipo kauli za wazi za viongozi wa kisiasa wakitishia kutumia mahabusu kama chombo cha kisiasa.  Mfano wa hivi karibuni ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Kati, Unguja, Rajab Ali Rajab, aliyesikika kwenye kanda ya video inayosambaa mitandaoni akisema atakamata watu na kuwaweka mahabusu ili kuhakikisha CCM inashinda na wapinzani hawapati hata kura 100 katika kila jimbo ndani ya wilaya yake. Cha kushangaza, hadi sasa Tume ya Uchaguzi wala Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa hazijatoa tamko lolote kuhusiana na kauli hiyo inayochochea uhasama.

Tatizo jingine linaloibua maswali ni namna vyombo vya habari vya umma vinavyotumika kisiasa. Vyombo hivi, ambavyo vinaendeshwa kwa kodi za wananchi wote, vinatoa upendeleo mkubwa kwa chama tawala, huku vikipuuzia au hata kupuuza kabisa habari na shughuli za vyama vya upinzani. Hali hii si tu inakiuka misingi ya usawa wa vyama vya siasa, bali pia inadhalilisha dhana ya uchaguzi huru. Watangazaji wamekuwa wakigeuza hata vipindi vya burudani kuwa majukwaa ya kampeni za chama kimoja. Hata sifa zinazotolewa kwa baadhi ya viongozi zimevuka mipaka kiasi cha kuonekana kama kufuru kwa mtu mwenye misimamo ya kidini.

Ni wajibu wa ZEC kukumbusha uongozi wa vyombo hivi kwamba vina wajibu kwa wananchi wote bila upendeleo wowote, na havipaswi kutumiwa kisiasa na upande mmoja wa ulingo wa kisiasa. Lakini hata ZEC yenyewe haiko huru na lawama. Katika chaguzi zilizopita, tume hiyo imewahi kuwaengua wagombea zaidi ya 10 kutoka vyama vya upinzani kwa madai ya kukosa sifa, huku baadhi yao wakiwa ni watu waliowahi kuwa wawakilishi, wabunge au viongozi wa serikali. Hali hii inaacha maswali: Je, ni kweli kuwa ni wagombea wa chama tawala pekee wanaokidhi vigezo vya kugombea?

Historia inaonyesha kuwa hata viongozi wa juu wa upinzani waliowahi kushika nyadhifa kubwa serikalini, kama marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, walikutana na vikwazo visivyo vya haki kutoka kwa tume hiyo. Hali hii inapunguza imani ya umma kwa taasisi hiyo muhimu.

Hoja nyingine ya msingi ni kura za mapema, ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wapinzani kama njia inayowezesha udanganyifu. Inadaiwa kuwa mfumo huo umechangia vurugu na majeraha kwa watu wengi katika chaguzi zilizopita.

ZEC inapaswa kuwa wazi kuhusu kura hizo: ni wangapi wanaopaswa kupiga kura mapema? Kura hizo zitahesabiwa vipi? Na je, zinahesabiwa pamoja na kura za siku ya uchaguzi au peke yake?

Maswali haya yanahitaji majibu ya wazi ili kuepusha mashaka na migogoro isiyo ya lazima. Uwajibikaji wa wazi utaleta amani na kuimarisha imani ya wananchi kwa tume hiyo.

Katika hali isiyopendeza, kuna ongezeko la maandishi ya matusi na uchochezi kwenye maeneo ya wazi kama ukuta wa majiji, mitaa na vijiji. Licha ya maeneo haya kujulikana, wahusika hawachukuliwi hatua yoyote, kana kwamba matusi na vitisho ni sehemu ya uchaguzi wa kidemokrasia.

Hili ni jukumu la vyombo vya usalama kuhakikisha hali hiyo inadhibitiwa kwa mujibu wa sheria. Katika baadhi ya chaguzi zilizopita, misafara ya wapinzani ilizuiwa barabarani kwa madai kuwa wananchi hawataki kuona vyama hivyo katika maeneo yao.

Walipovuka vizuizi hivyo, walishambuliwa kwa mawe, na vyombo vya usalama vilitumia risasi za moto na mabomu ya machozi. Uhalifu huu haupaswi kurudiwa. Vyama vyote vina wajibu wa kuhakikisha kuwa wanaowapa nafasi ya kuhutubia majukwaa ya kampeni wanatumia lugha ya staha, yenye kuhimiza mshikamano na siyo mfarakano. Siasa ni uwanja wa hoja, siyo matusi wala vitisho.

Kwa ujumla, uchaguzi wa Zanzibar unaweza kuwa wa haki na amani ikiwa taasisi husika ikiwamo ZEC, vyombo vya habari, vyombo vya usalama na vyama vya siasa vitatimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria, uwajibikaji na maadili ya kisiasa.