Moshi. Mwili wa Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao (86), umezikwa leo Alhamisi Septemba 4, 2025 katika Usharika wa Lole Mwika, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Katika ibada hiyo ya maziko, Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa akihubiri amewataka waumini na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuliombea Taifa na kuwa watu wa kuleta amani, upendo na nuru kwenye jamii.
Aidha, amesisitiza kuwa kila msiba unapaswa kuwapa nafasi watu wa kutafakari maisha wanayoishi badala ya kuzoea vifo kama jambo la kawaida.
“Jambo moja ambalo ningependa kusisitiza ni kwamba, kila mwanakanisa na kila anayemjua Mungu aendelee kuliombea Taifa letu. Lakini pia tufanye kazi ya kuwa chumvi na nuru kama Yesu alivyotuagiza. Tusizoee misiba, kila msiba utufundishe na kutufanya tuweke imani yetu kwa Mungu,” amesema Dk Malasusa.
Akizungumzia utumishi wa marehemu, amesema Askofu Shao alikuwa kiongozi mwenye hekima na aliyetumikia kanisa kwa uaminifu, akipanua huduma yake ndani na nje ya nchi.
Kwa niaba ya maaskofu, Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Meru, Paulo Akyoo, amesema: “Askofu Shao amelala lakini hanuki, ananukia. Ameacha harufu njema, na hili ni somo kwa kila mmoja wetu, kuchagua kuacha harufu inayonukia au yenye kunuka.
Akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema marehemu Shao alikuwa daraja muhimu baina ya kanisa, serikali na jamii.
“Serikali itaendelea kumkumbuka Dk Shao kwa mchango wake mkubwa kwa kanisa na jamii. Alijenga mshikamano, aliheshimu na kuthamini watu, alikuwa mnyenyekevu na mzalendo. Tuliobaki tunayo mengi ya kujifunza kutoka kwake,” amesema Biteko.
Aidha, amewataka Watanzania kuishi maisha yenye alama mema ili siku ya kuondoka duniani wakumbukwe kwa matendo yao mazuri.
Miongoni mwa viongozi waliotoa pole ni mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo kupitia CCM, Enock Koola aliyesema marehemu Shao alikuwa kiungo muhimu kati ya kanisa na jamii. Naye mwanasiasa mkongwe James Mbatia alimtaja kama kiongozi mzalendo na muunganishi wa watu.
Ibada hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu na Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Freeman Mbowe, sambamba na maaskofu wa makanisa yanayounda Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na viongozi wa dini mbalimbali.
Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Zebadiah Moshi akisoma historia ya marehemu, amesema Askofu Shao atakumbukwa kwa uhodari wake katika kuhubiri Injili na kujenga mshikamano wa kanisa ndani na nje ya nchi.
Amemtaja kuwa kiongozi aliyepigania haki na usawa, aliyewajali watu kiroho na kijamii. Alieleza kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu, ikiwemo ugonjwa wa kisukari aliouhudumia kwa nidhamu kubwa.
Kwa mujibu wa historia, Dk Shao aliwahi kuwa mchungaji wa Dayosisi ya Kaskazini kati ya mwaka 1966 hadi 1974, mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki (1974-1976), msaidizi wa askofu (1976-2004) na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini kuanzia mwaka 2004 hadi alipostaafu mwaka 2014.
Marehemu ambaye alikuwa askofu wa tatu wa Dayosisi hiyo, ameacha mjane, watoto watano na wajukuu 11.