Simba imefanya mabadiliko makubwa ya Bodi ya Wakurugenzi baada ya mwekezaji Mohammed Dewji ‘MO’ akijiweka kando, huku akimteua Crescentius Magori kuchukua nafasi hiyo, ilihali CEO wa zamani wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez akirejea klabuni.
Mabadiliko hayo ambayo yametangazwa dakika chache zilizopita, MO mbali na Magori aliyewahi kuwa, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo na mshauri wa Mo Dewji ameteua sura mpya nne, huku watatu wakitoka Bodi iliyopita.
Wajumbe wapya wanne katika Bodi hiyo ni pamoja na mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji aliyekuwa Mwenyekiti wa zamani, Swedy Mkwabi, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na George Ruhango.
Barbara alitangaza kujiuzulu Simba Desemba, 2022 japo nafasi hiyo ya Mtendaji Mkuu aliiacha rasmi Januari 10, 2023 akiwa mmoja ya viongozi walioweka heshima klabuni hapo, hasa kwa mafanikio ya Simba kimataifa.
Wengine ni Zuly Chandoo, wakati Rashid Shangazi na Hussein Kitta wakiendelea kwenye Bodi hiyo.
Kwenye Uteuzi huo jina kubwa lililoshtua likikosekana ni Salim Mhene ‘Try Again’ aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo.
Taarifa hiyo haijaweka wazi sababu za kuondolewa kwa Try Again ambaye alikuwa Mjumbe aliyedumu kwa muda mrefu kabla ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji.