Cecilia Paresso alivyomnadi Samia, Daniel Awack kwa wananchi Karatu

Karatu. Aliyekuwa mbunge wa Viti Maalumu katika Bunge lililopita na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Cecilia Paresso amesema kwa kazi iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan anastahili kuenziwa kwa kupigiwa kura ya ndio ili aendelee kukamilisha ndoto yake ya kuijenga Tanzania mpya.

Paresso, ambaye awali alikuwa mwanachama na mbunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema Samia, ambaye kwa sasa ni mgombea urais wa CCM, amefanya kazi ya mfano wa kuigwa ikiwemo kukamilisha miradi yote mikubwa na ya kimkakati.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Jumatano, Septemba 3, 2025 kwenye Uwanja wa Mazingira Bora wilayani Karatu, Paresso amesema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa, Samia ndiye chaguo sahihi kutokana na uchapakazi wake na kuiendesha nchi kwa maslahi ya wananchi.

Amesema Rais Samia amesimamia vyema maridhiano ya kisiasa ambayo yameleta ustahimilivu wa kisiasa na amani ambayo ni msingi wa maendeleo. Pia, kuvutia uwekezaji na kutoa uhuru wa maoni kwa wananchi, mambo ambayo hayakupewa nafasi huko nyuma.

“Samia amevutia uwekezaji mkubwa wa kimataifa unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani 40 bilioni kwenye mradi wa gesi mkoani Lindi, hii ndio faida ya kuwa na kiongozi mwenye maono makubwa kwa nchi yetu.

“Amesimia miradi mikubwa ya nishati ya umeme vijijini ambako wananchi wengi wananufaika na huku mradi wa uzalishaji umeme wa Bwawa la Nyerere ambao, umekamilika na kutoa uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini,” amesema Paresso.

Kuhusu sekta ya afya, Paresso amesema chini ya uongozi wa Rais Samia, zaidi ya Sh1.3 trilioni zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa hospitali nchini huku Wilaya ya Karatu ikiwa miongoni mwa watakaonufaika. Kwa mujibu wa Paresso hatua hiyo inakwenda kuboresha huduma za afya ikiwemo wagonjwa kufuata huduma kwenye hospitali kubwa mbali na maeneo yao.

“Sasa ndugu zangu wana-Karatu tunataka kumpigia kura nani tena zaidi ya Samia? Huyu ndiye kiongozi wa wananchi hivyo, tumuunge mkono kuhakikisha anashinda kwa kishindo ili kumtia moyo wa kwenda kufanya makubwa zaidi,” amesema Paresso.

Mbali na kumnadi Samia, Paresso pia ametumia jukwaa hilo kuwaomba wananchi kumchagua mgombea ubunge wa Jimbo la Karatu, Daniel Awack kwa maslahi mapana ya wananchi.
Paresso, ambaye alikuwa miongoni mwa watinia kwenye nafasi ya ubunge wa jimbo hilo, amesema kwa sasa makundi yote yamevunjwa na kila mwana-CCM anapaswa kumchagua Awack.

“Naomba niseme kuwa ndani ya CCM hakuna makundi tena sasa waliokuwa watiania wote  tunamuunga mkono Awack awe mbunge wetu kwa ajili ya maendeleo yetu sote,” amesema Paresso ambaye amekuwa mbunge wa viti maalumu kuanzia mwaka 2012-2025. 

Kwa muda mrefu Jimbo la Karatu limekuwa ngome ya upinzani kwa kipindi cha miaka 25 kabla ya Daniel Awack anayegombea kwa awamu ya pili kutangazwa mshindi  katika uchaguzi wa mwaka 2020 dhidi ya Cecilia Paresso aliyekuwa akiwania kupitia Chadema.

Kwa upande wake, Awack akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano huo amesema kumekuwa na maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka mitano akiwa mbunge na kuomba ridhaa yao ili aendeleze mazuri yote aliyoanza.
“Katika kipindi cha miaka mitano tumeshirikiana kutatua changamoto za maji kwa kuchimba visima zaidi, tumejenga shule za msingi na sekondari li kuwaondolea kero watoto kutembea umbali mrefu. Nawaahidi mkinipa kura za kutosha nitaendeleza mchakamchaka wa maendeleo,” amesema Awack.