Dodoma. Mgombea mwenza Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja amesema tatizo la maji nchini litakomeshwa chini ya Serikali ya chama hicho kwa sekta hiyo kubinafsishwa.
Amesema ubinafsishaji ni sehemu ya kuondoa kero ya maji ambayo kwa muda mrefu Serikali chini ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeshindwa kuwapatia huduma ya uhakika Watanzania.
Mgombea mwenza huyo ameyaeleza hayo leo Alhamisi Septemba 4, 2025 akiwa katika Kata ya Matongoro Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma.
Mgombea huyo amefanya mkutano wake wa kwanza wa kampeni mkoani Dodoma alikoingia leo kwa lengo la kunadi sera sambamba na kuomba ridha ya kura kwa wananchi ikifika Jumatano Oktoba 29, 2025, wakiweke madarakani kwenye uchaguzi mkuu.
“Eneo la Kongwa ni tambarare tupu mnastahili kukaa na njaa kweli, kinachokosekana hapa ni maji tu tungekuwa na maji ya kutosha Kongwa ingekuwa kame hamuwezi kulima kama hakuna maji.”
“Tumezungukwa na maji na mito kila pahala, pia kimo cha maji Kongwa hakipo chini sana tungeyatoa hayo maji ardhini wananchi wakatumia kwenye umwagiliaji, tupeni ridhaa tutaipa sekta binafsi iwekeze kwenye maji ifanye vizuri,” amesema mgombea mwenza huyo.
Amesema Serikali inapaswa kutoa kipaumbele kwenye sekta ya maji na siyo kufanya maigizo kwenye huduma ambayo ni muhimu kwa wananchi.
Maigizo aliyoyataja ni kuzinduliwa kwa miradi ya maji ambayo kwa muda mfupi baada ya kuzinduliwa haitoi maji, akitafsiri ni kupoteza fedha za kodi za wananchi na kuendelea na kero ya huduma husika.
Amesema sekta binafsi ndio itakuwa na jukumu la kuhakikisha wananchi wote wamepata maji huku bili wakilipa kidogo kidogo akiwahakikishia kuwa gharama haitazidi Sh1,000 kwa mwezi.
Kwa eneo la afya, amesema kumekuwa na mzigo wa gharama ambazo zinamfanya mjamzito kutumia fedha nyingi anapojifungua kama ananunua mtoto.
Tatizo hilo amesema litatuliwa kwa kila Mtanzania kupatiwa bima ya afya ambayo itampa kipaumbele katika huduma za afya, badala ya hali ilivyo sasa mgonjwa anaweza kuwa na bima na akatakiwa kulipia fedha taslimu.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa kata ya Matongoro, Dominic Mnyawaga amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwaongoza, huduma ya maji,barabara zitapatiwa ufumbuzi kwani kwa muda mrefu wamekuwa wanyonge.