Kilimanjaro. Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amesema serikali ya chama hicho ikipewa ridhaa na wananchi kuongoza nchi, itaanzisha sera mpya na mbadala ya kuimarisha sekta ya kilimo kupitia skimu za kisasa za uzalishaji wa mazao ya parachichi na ndizi huku akisema reli ya kisasa itafika mikoa ya Kaskazini.
Amesema mpango huo utakaoenda sambamba na uanzishwaji wa viwanda vya kusindika mazao hayo, watawekeza kuanzia asilimia 10 ya bajeti ya nchi na uzalishaji wake utazingatia mahitaji ya soko la dunia.
Akizungumza leo Alhamisi Septemba 4, 2025 na wananchi wa Kijiji cha Mamsela na baadaye katika mkutano uliofanyika Tarakea, Wilaya ya Rombo, Mwalimu amesema moja ya vipaumbele vya Serikali ya Chaumma ni kutatua changamoto ya ajira kwa vijana kupitia uwekezaji mkubwa kwenye kilimo cha kisasa, kinachozingatia viwango vya kimataifa vya uzalishaji na usindikaji wa mazao.
“Nasema nikiingia madarakani, tutaanzisha sera madhubuti za kuendeleza skimu za kisasa za kilimo cha ndizi na parachichi ili yazalishwe kwa ubora unaokubalika kimataifa. Lengo letu ni kuongeza ajira, kuinua vipato vya wananchi na kuhakikisha utajiri wa mazao haya unabaki hapa nchini,” amesema.

Akiwa njiani kuelekea Tarakea, mgombea huyo amekosoa uongozi uliopo madarakani kwa kushindwa kulinda na kuinua thamani ya mazao ya kilimo yanayozalishwa hapa nchini.
Amesema ni jambo la kushangaza kuona bidhaa kama parachichi na ndizi kutoka Tanzania zikiuzwa kwa majina ya mataifa mengine kutokana na ukosefu wa sera makini.
“Haiwezekani ndizi na parachichi zilizozalishwa hapa Tanzania zisafirishwe kufungashwa nje ya nchi na kuuzwa kama bidhaa kutoka mataifa mengine. Chaumma hatutakubali hali hiyo iendelee. Tutahakikisha tunajenga miundombinu ya kisasa.
“Ikiwemo viwanja vya ndege vya kusafirisha mazao hayo moja kwa moja kutoka mikoa kama Kilimanjaro kwa kutumia nembo ya Tanzania,” ameongeza Mwalimu anayeendelea na mikutano ya kumwaga kampeni za kuomba kura.
Mgombea huyo pia ameeleza kuwa ilani ya Chaumma imeweka kilimo kama nguzo kuu ya maendeleo ya uchumi wa nchi, akisisitiza kuwa ni jambo lisilokubalika kuona Serikali ikikopa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mikubwa wakati fursa za maendeleo zipo katika ardhi yenye rutuba ambayo haijatumika ipasavyo.
“Tuna ardhi nzuri, tuna vijana wenye nguvu tusubiri nini? Tuamue sasa. Chaumma ikipewa nchi ndani ya miaka mitano, reli ya kisasa itafika Kaskazini kuongeza utalii, kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuongeza ajira kwa vijana wa mikoa kama Kilimanjaro,” amesema.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Rombo kupitia chama hicho, Andrea Oisso, ameeleza kuwa wananchi wa eneo hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu duni, jambo linalosababisha usumbufu mkubwa katika kusafirisha mazao ya kilimo.

“Wakulima wetu wanalima ndizi na maparachichi kwa wingi, lakini kutokana na ubovu wa barabara, bidhaa hizo husafirishwa kwa shida kwenda Dar es Salaam na hata nje ya nchi kwa kutumia malori,” amesema Oisso.
Ameeleza kusikitishwa na hali ya mazao hayo kuuzwa nje ya nchi huku wakulima wa Rombo wakibaki bila kunufaika ipasavyo.
“Tunazalisha parachichi na zinaenda nchi jirani bila sisi kunufaika tunabaki mikono mitupu,” amesema