Morogoro. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja amewaomba wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kukichagua chama hicho ili mabadiliko ya sheria za uchaguzi ‘reforms’ ambazo wanazipigania wakaziharakishe.
Devotha amesema hata wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanapaswa kuichagua Chaumma ili ikabadili mifumo ya kodi ambayo sio rafiki kwa wananchi.
Mgombea mwenza huyo ameowaomba kura wananchi hao leo Septemba 3,2025 kupitia mkutano wa hadhara alioufanya Jimbo la Morogoro mjini, akinadi sera za chama hicho ili wananchi wakiamini na kukichagua kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu.

“Sisi tunasema daktari ni daktari, kama kule tulipokuwepo tulikuwa madaktari tumekuja na udaktari wetu, uwezo wetu upo vilevile kuna vyama havishiriki uchaguzi visione aibu, adui yetu ni CCM, mwaka 2015 tuliwahi kuwa na Umoja wa Katiba wa Wananchi (Ukawa) palipokuwa na nguvu CUF tuliunga mkono kama ACT Wazalendo tunawaunga mkono.
Kama Chadema hawapo mtuunge mkono kwasababu adui yetu ni CCM tunazitaka ‘reforms’ tukiingia bungeni ni reforms, reforms, reforms ndiyo itakuwa kipaumbele kwa Chaumma, lakini unazipataje ‘reforms’ lazima uwe na wawakilishi bungeni wakabadili katiba,” amesema.
Devotha amesema, ni ngumu kupata mabadiliko kama wawakilishi wa wanaotaka mabadiliko hawapo bungeni, akisisitiza dhamira ya Chaumma kupambana hadi kushika dola katika sanduku la kura.
Mbali na hayo mgombea mwenza huyo amesema Chaumma imejipanga kuboresha sekta ya kilimo ili kiwe cha tija kwa wakulima kulima kwa kutumia trekta badala ya jembe la mkono.

“Tukiingia madarakani cha kwanza tutahakkisha tunawekeza kwenye chakula, mashamba mazuri na mabonde tutasimamia yalimwe tutapunguza gharama za uzalishaji,
“Kama mkulima analima tukampa mbolea bure, tukapunguza gharama za mafuta watu waache kutumia jembe la mkono watumie trekta, mafuta yakiwa chini badala ya mtu kulima kwa trekta kwa Sh100,000 kwa hekari atakilima kwa Sh20,000, watu wanapandisha vyakula sababu ya gharama za uzalishaji”amesema.
Pia amesisitiza kuwa eneo la bandari ili kutengeneza mazingira bora ya biashara mlolongo wa kodi ambazo zinazofanya bidhaa zinazopita bandarini kuwa ghali huku mataifa yasiyo na bandari yakineemeka zitafutwa na Chaumma ili Watanzania wafurahie huduma za bandari nchini.
Kwa kero ya maji na barabara,Devotha amesema Chaumma imejipanga mkoa wa Morogoro wenye maeneo mengi ambayo barabara ni vumbi kujengwa kwa kiwango cha lami na maji masafi bili kwa wananchi kwa mwezi isizidi Sh1,000.
Mgombea Ubunge Jimbo la Morogoro mjini Elizeus Rwegasira ameahidi kuwasaidia vijana wanaondesha pikipiki maarufu bodaboda kupata mafunzo na kupewa vyeti ili kuepukana na ajali za barabarani.
Mgombea huyo amesema mkoa wa Morogoro una matukio ya mara kwa mara ya ajali za pikipiki akiahidi mafunzo yatakayotolewa ndio suluhisho.

Mbali na hayo amesema kundi hilo halina uongozi kwa muda mrefu hivyo atawezesha uchaguzi huku kwa kundi la wanafunzi wa Sekondari na vyuo vikuu akiahidi kuwapatia kompyuta ili waendane na teknolojia.
Awali, Mgombea udiwani Kata ya Mjimpya, Mgeni Misoti, amesema ameamua kuwania nafasi hiyo ili kuleta maendeleo yanayokosekana sasa.
“Mjimpya inastahili kuitwa mji mkongwe, lakini inakabiliwa na changamoto za barabara mbovu, vumbi, kukosa taa na giza kutawala,hayo ndiyo nitakayoyapigania nikichaguliwa,” amesema.
Mwenyekiti wa Chaumma wilaya ya Morogoro mjini, Ismail Rashid, amesema tangu uhuru Morogoro haijawahi kupata mgombea mwenza wa rais, hivyo wananchi wa mkoa huo wana kila sababu ya kukiunga mkono chama hicho.
“Devotha Minja ni mtoto wetu. Amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu na ni mtetezi wa wanawake,ni mama mwenye dira, sasa ni wakati wake kuingia Ikulu,” amesema.
Mgombea mwenza huyo amehitimisha ziara yake ya kampeni mkoani Morogoro na sasa anaelekea mkoani Dodoma.