KUMEKUWA na mijadala mbalimbali juu ya kiwango cha kiungo mkabaji mpya wa Yanga, Balla Mousa Conte aliyetua klabuni hapo kutoka CS Sfaxien ya Tunisia, lakini kumbe mwenyewe amesikia kila kitu kinachoendelea na kuamua kutoa kauli ya kibabe akituma salama mapema.
Kiungo huyo amesema licha ya presha kubwa ndani ya kikosi hicho hasa eneo analocheza hana wasiwasi kutokana na ubora alionao na ule wa kikosi cha timu hiyo kwa ujumla na kutaka mashabiki wasubiri msimu mpya utakapoanza rasmi kuanzia Septemba 16 waone mambo.
Conte amejiunga na Yanga akipishana na Khalid Aucho aliyetua Singida Black Stars baada ya kumaliza mkataba Jangwani alipotumika kwa mafanikio kwa misimu minne na mijadala imezuka baada ya kucheza katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda ikielezwa kwamba ameonekana mzito uwanjani.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa ya Guinea, inayojiandaa kucheza mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Somalia na Algeria, Conte amesema alifanya uamuzi sahihi kuichagua timu hiyo na hana presha kabisa.
“Natambua Yanga ni timu kubwa na nafasi ninayocheza wamepita wachezaji wengi wakubwa na bora hilo halinipi presha, kwani mpira ni mchezo wa wazi Yanga imekamilika kila eneo ni muda wangu na mimi kuonyesha kile nilichonacho,” alisema Conte na kuongeza;
“Sichezi peke yangu, tunakutana wachezaji 11 uwanjani ambao kila mmoja ana nafasi ya kufanya vizuri, naamini tutafanya kitu kikubwa ambacho kinatarajiwa na mashabiki ambao wana ndoto kubwa kwetu wachezaji. Najua namna gani ya kuwapa raha.”
Conte alisema anaamini Yanga ina malengo makubwa na kama wachezaji watapambana kuendana na mipango na mikakati ya uongozi ili waweze kufikia malengo, suala la presha kwake halina nafasi, ana imani kubwa na nyota waliopo akiwamo yeye mwenyewe ni watu watakaoibeba timu hiyo.
“Ni muda mchache nimekaa na timu nimeona ubora mkubwa na kila mchezaji ameonyesha kuwa na kiu ya kufanya vizuri, hivyo kwa pamoja bila ya kujitazama mimi mwenyewe kutokana na presha kubwa iliyopo naona kabisa nina nafasi ya kufanya vizuri,” alisema Conte aliyeitumikia Sfaxien katika mechi 23 za Ligi Kuu bila kufunga bao wala kuasisti na kulimwa kadi saba za njano mbali na mechi nyingine za michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.
“Unajua katika timu ni ngumu kama wewe pekee ndiye unaona una nafasi ya kuaminiwa, ndani ya Yanga kila mchezaji ni bora na kila mmoja anataka kuthibitisha hilo, hivyo ni kikosi ambacho kina wachezaji wenye vipaji vikubwa nami najipanga kuhakikisha nafanya makubwa.”
Conte alisema anacheza ndani ya timu hiyo bila kuumiza kichwa na badala yake anacheza akiwa katika hali ya kawaida, kwa vile tayari amekutana na wachezaji wengine bora na uzuri ni kwamba yeye hatazamwi kama mchezaji mkubwa kwa kuwa tayari kuna wakubwa kutokana na walichokifanya msimu uliopita, hivyo anaingia akijiweka tayari katika mazingira mazuri ya kuipambania timu.
Alisema anawapenda wachezaji wote ndani ya timu hiyo na hana chaguo kutokana na kubaini kuna vipaji vikubwa na anaamini kwa pamoja watakuwa na msimu bora na wa ushindabni kwa timu pinzani.
Conte ni kati ya wachezaji 11 wa Yanga walioitwa katika timu tofauti za taifa kwa ajili ya mechi hizo za kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia 2026 akiwamo kipa Diarra Djigui (Mali), Lassane Kouma na Ecua Celestin (Chad), Balla Mousa Conte (Guinea) na Dube Abuya (Kenya) na sita waliopo Taifa Stars.