Daraja dogo la mbao chakavu lawatesa wanakijiji Hai

Hai. Wananchi wa Kijiji cha Kyuu, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kujenga daraja dogo katika eneo la Mto Kishenge, Kitongoji cha Maiputa, ili kuwawezesha kuendelea na shughuli mbalimbali za kijamii na kimaendeleo bila vikwazo.

Ombi hilo limetolewa wakati wa ziara ya Ofisa Tarafa wa Masama, Nswajigwa Ndagile, alipotembelea eneo hilo na kujionea hali mbaya ya daraja hilo ambalo lilijengwa kwa miti miaka mingi iliyopita na kwa sasa limeoza, hali inayowalazimu wananchi kutumia daraja hilo kwa tahadhari kubwa kutokana na hatari iliyopo.

Wakizungumza mara baada ya ziara hiyo, wananchi wamesisitiza umuhimu wa Serikali kuingilia kati kwa haraka ili kuokoa maisha yao na kuhakikisha shughuli za kijamii, kiuchumi na maendeleo zinaendelea bila vikwazo.

Afisa Tarafa Masama Nswajigwa Ndagile katika, akiangalia Daraja dogo lilijengwa kwa mbao na miti lilianza kuharibika katika kijiji cha Kyuu Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro



“Ni kweli kwa muda huu ili daraja sio salama kwa wananchi kulitumia, miundombinu yake imeoza kwani imejengwa kwa miti,” ni kauli ya wananchi.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kyuu, Anna Munisi, amesema daraja  katika Mto Kishenge ni kiungo muhimu kwa wakazi wa eneo hilo, hasa katika kusafirisha mazao ya kilimo kama mahindi kipindi hiki cha mavuno, pamoja na mboga mboga zinazokwenda sokoni, ikiwemo Soko la Sadala.

Ameeleza kuwa kutokana na daraja hilo kujengwa kwa miti ambayo kwa sasa imeoza, wakazi wengi wameanza kuogopa kulitumia, hasa kwa vyombo vya moto, jambo ambalo limesababisha walazimike kutumia njia mbadala ambazo ni ndefu na zenye kuongeza gharama za usafiri.

Afisa Tarafa Masama Nswajigwa Ndagile katika, akiangalia Daraja dogo lilijengwa kwa mbao na miti lilianza kuharibika katika kijiji cha Kyuu Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro



Kutokana na hali hiyo, ameomba Serikali kuchukua hatua za haraka kuondoa kero hiyo inayozuia maendeleo ya wananchi.

Mwenyekiti wa Kijiji, Benson Ndos amesema baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi alitoa taarifa kwa Ofisa Tarafa, ambaye alifika kijijini hapo kujionea hali halisi ya daraja hilo.

Ndos amesema kutokana na ukaribu wa daraja hilo na eneo la mwekezaji wa Kampuni ya Mijiru, Meneja wa kampuni hiyo pia alihudhuria ili kushiriki katika kutafuta suluhisho.

Baada ya mazungumzo, Meneja wa Kampuni ya Mijiru alieleza kuwa wako tayari kusaidia katika ujenzi wa daraja hilo.

Afisa Tarafa Masama Nswajigwa Ndagile katika, akiangalia Daraja dogo lilijengwa kwa mbao na miti lilianza kuharibika katika kijiji cha Kyuu Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro



Hata hivyo, alibainisha kuwa kwa kuwa barabara hiyo ipo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), watatoa taarifa na kuomba mwongozo kutoka kwao ili kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.

“Ni kweli tulishaona tatizo hili na Tarura, tunaomba  muongozo, kutoka Tarura ili kufanikidha suala hili kwa sababu Ofisa Tarafa upo hapo, nadhani utawahimiza wafike wafanye ili  tathimini ya ujenzi uweze kuanza,” amesema meneja huyo.

Ofisa Tarafa Nswajigwa Ndagile amesema  atawasiliana na Tarura wilayani humo, kufika na kutoa mwongozo wa pamoja na ushauri wa kitaalamu juu ya namna ya kujenga daraja hilo.