KUJIAMINI kulikofanywa na timu ya Tausi Royals, katika Ligi ya Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (WBDL) ndiko kulikoifanya timu hiyo ishindwe kucheza nusu fainali ya Ligi hiyo.
Timu ya Tausi Royals ilifungwa na DB Troncatti katika michezo 2-1.
Sababu iliyofanya ijiamini hivyo, ilionyesha ni kutokana na uwezo wa wachezaji walionao, na huku timu ya DB Troncatti ikijipanga kuiadhiri timu hiyo katika robo fainali.
Kushindwa kwa timu hiyo, pia kulitokana na kukosa mipango mizuri ya uchezaji wa timu hiyo, itakayofanya ifunge pointi.
Tofauti na timu ya DB Troncatti mipango iliyokuwa nayo, ni kucheza kwa malengo ya kufunga pointi muda wote.
Ikiongozwa na Jesca Lenga, nyota huyo aliiongoza timu hiyo icheze kwa mipango, hali iliyofanya ishinde .
Mchezaji huyo anayecheza namba moja (point guard), aliiwezesha timu yake kushinda katika robo fainali.
Uwezo aliyoonyesha katika robo fainali hiyo, ni jinsi alivyokuwa anamiliki mpira, na utoaji wa pasi kwa mfungaji.
Katika robo fainali hiyo, Jesca alifunga pointi 15 katika robo fainali ya kwanza na alitoa asisti 14, huku robo fainali ya pili alifunga pointi 20 na kutoa asisti 10 wakati robo fainali ya tatu alifunga pointi 18 na asisti 10.
Katika robo fainali ya kwanza Tausi Royals ilishinda kwa pointi 68-60, huku robo fainali ya pili na ya tatu, DB Troncatti ikishinda kwa pointi 61-58 na 56-46.
Kwa ushindi huo, timu ya DB Troncatti itacheza na JKT Stars katika mchezo wa nusu fainali, ambayo nayo ilitinga hatua hiyo baada ya kuifunga Vijana Queens katika michezo 2-0.