DK Biteko awataka Watanzania kuacha alama katika utumishi wao

Moshi. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ibada ya mazishi ya Askofu mstaafu Dk Martin Shao aliyefariki dunia Agosti 25, mwaka huu.

Akizungumza baada ya Ibada ya maziko leo Alhamisi Septemba 4, 2025 yaliyofanyika katika Kijiji cha Lole, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Dk Biteko amesema marehemu Askofu Shao wakati wa uhai wake alifanya mambo mengi mazuri ya kukumbukwa hata baada ya kifo chake.

“Mzee wetu, Hayati Askofu Shao ameanza kazi za kanisa akiwa kijana na amefanya kazi kubwa ambayo kila mmoja anaishuhudia leo, ameacha alama inayotokana na kazi aliyoifanya,” amesema kiongozi na kuongeza;

“Mheshimiwa Rais amenituma niwaletee salamu zake za pole nyingi sana wanafamilia, viongozi wote wa Kanisa KKKT pamoja na ndugu jamaa na marafiki wote kwa na msiba.”

Amesema Serikali itakumbuka mchango wa Askofu Shao ambaye ametumikia Kanisa katika maisha yake tangu ujana wake na hata baada ya kustaafu ameendelea kuwa mshauri.

Amewahimiza waombolezaji kuendelea kuwa karibu na kushirikiana na wafiwa katika kipindi hiki cha majonzi huku akiwahakikishia kuwa Serikali iko pamoja nao hasa katika kipindi hiki cha majonzi.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa amewataka waumini kutumia msiba huo kumshukuru Mungu kwa ajili ya mtu kama hayati Askofu Shao ambaye alikuwa kielelezo cha maisha bora kwa wanadamu.

Ameongeza kuwa Askofu Shao alikuwa mnyenyekevu na msikivu hali ambayo amesema imeanza kutoweka miongoni mwa wanajamii

“Wanyenyekevu kama Dk Shao wameanza kuwa adimu katika jamii na Viongozi waliomtengeneza Dk Shao walifaulu sana… amefanya mambo mengi ndani na nje ya usharika,” amesema Askofu Dk Malasusa.

Amefafanua kuwa Askofu Shao enzi za uhai wake alifanya kazi kubwa ya uinjilishaji ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa umahiri mkubwa.

“ Tusizoee misiba, kila msiba utupe nafasi ya kutafakari maisha yetu,” amesema Askofu Malasusa.

Ibada ya mazishi imehudhuriwa na maelfu ya waombolezaji na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, Mkuu wa Mkoa wa Kilimajaro, Nurdin Babu na Mgombea wa urais kwa tiketi ya Chaumma, Salum Mwalimu.