Dk Biteko kuongoza waombolezaji maziko ya Askofu Shao

Moshi. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amewasili katika  Usharika wa Lole Mwika, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kuungana na mamia ya waombolezaji katika ibada ya  Maziko ya  Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao (86).

Maziko ya Askofu Shao yanafanyika leo, Septemba 4, 2025, katika eneo la Usharika wa Lole, ambapo yamehudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo maaskofu kutoka makanisa yanayounda CCT, viongozi wa dini mbalimbali na viongozi wengine wa  Serikali.

Ibada hiyo ambayo inaongozwa na Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa, pia imehudhuriwa na viongozi wa kisiasa akiwemo mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu na wafanyabiashara.

Dk Shao ambaye  alihudumu kama Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini kuanzia mwaka 2004 hadi 2014 alipostaafu, alifariki dunia asubuhi ya Agosti, 25,2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC, Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Katika historia inaonyesha mwaka 1966-1974 Dk Shao alikuwa mchungaji wa Dayosisi ya Kaskazini, 1974-1976 alikuwa Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki, 1976-2004 alikuwa Msaidizi wa Askofu Dayosisi ya Kaskazini na mwaka 2004-2014 alikuwa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini.

Askofu Dk Shao ambaye alikuwa askofu wa Tatu wa Dayosisi ya Kaskazini, alikuwa kiungo muhimu katika umoja wa kanisa, jumuiya za kanisa na taasisi za ndani na nje ya nchi.

Ametajwa kama kiongozi aliyetumikia kanisa na jamii kwa uaminifu, Askofu aliyejali mambo ya kiroho, mtetezi wa haki na usawa.

Kwa mujibu wa historia ya marehemu iliyosomwa jana na Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Zebadiah Moshi wakati wa ibada maalumu ya kuagwa mwili wake iliyofanyika usharika wa Moshi Mjini, Askofu Dk Martin Shao (Mstaafu) alikuwa akisumbuliwa na maradhi  ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kisukari ambao umemsumbua kwa muda mrefu.