Dk Mwinyi aonya biashara pembezoni mwabarabara akizindua soko la Chuini

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema hakuna tena sababu kwa wananchi kuendelea kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi au pembezoni mwa barabara, kwa kuwa Serikali imeboresha miundombinu na kujenga masoko yenye viwango vya kimataifa.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Septemba 4, 2025, wakati akizindua Kituo cha Mabasi na Soko la Chuini Kwanyanya, lililopo Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo pia alitoa maagizo matano ya kusimamia na kuimarisha matumizi ya miundombinu hiyo kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya miji.

“Hakuna sababu tena ya kuwakuta wafanyabiashara na wajasiriamali wakifanya biashara zao pembezoni mwa barabara na maeneo mengine yasiyorasmi,” amesema Dk Mwinyi.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wasimamizi ambao ni Baraza la mji kuhakikisha wanatoza kodi ndogo kwa wafanyabiashara watakaotaka kufanya biashara ndani ya soko hilo.


Pamoja na hilo, Dk Mwinyi ameagiza wafanyabiashara waingizwe haraka ili waanze kufanya biashara kwani likikaa muda mrefu itakosa maana na lengo la kuwasaidia kuendesha biashara katika mazingira bora.

Pia, ameagiza uendeshaji na kuzingatia usafi uendeshwe na kampuni zenye uwezo na kufanya usafi ili kuepuka kuchakaa.

“Naagiza barabara zote zinazozunguka soko hili zitiwe lami haraka, kuwe na mandhari nzuri na kituo cha mabasi kianze kutumika mara moja ili wanachi wapate kuendesha shughuli zao bila vikwazo,” amesema Dk Mwinyi.

Baada ya kukamilika soko hilo, sasa Unguja imekuwa na masoko makubwa yenye uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 4,000 kila moja likiwemo la Mwanakwerekwe na Jumbi.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi msingi wa ujenzi wa masoko hayo, wakati wa kampeni za mwaka 2020 aliuliza wafanyabiashara kwamba kitu gani anataka awafanyie wakamwambia wanataka mazingira mazuri ya kufanyiabiashara na kupewa mikopo ya biashara.

“Leo nashukuru ahadi hiyo nimeitekeleza tumejenga masoko mazuri sana kwa ajili ya biashara, nimeridhika sana soko hili ni kubwa kama tulivyotaka, iwapo wafanyabiashara wakipangwa vizuri wataingia wengi sana,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema bado kuna masoko mengine mengi yanajengwa likiwemo soko la Mombasa na Malindi.

Dk Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kuwa wamoja na kujiepusha na mifarakano hususani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Awali, akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Issa Mahfoudh Haji amesema mradi huo una maeneo mawili ya kituo cha basi na soko ambapo eneo la soko lina ukubwa wa mita za mraba 43,293 jengo likiwa na milango 98 na vizimba 481 ikiwa na migahawa, ofisi na eneo maalumu la wanawake kunyonyesha.

Pia, amesema eneo hilo linauwezo wa kuchukua magari 200 kwa wakati mmoja.

Kwa upande wa kituo cha mabasi, Katibu Mkuu amesema lina ukubwa wa mita za mraba 28,625 likiwa na  uwezo wa kuingiza mabasi 110 kwa wakati mmoja.

Mradi huo ulioanza kujenga Novemba 15, 2022, na kukamilika Machi 31, 2025 umegharimu Sh43 bilioni ambapo wafanyabiashara na wajasiriamali 4000 watapata fursa za ajira katika soko na kituo hicho cha daladala.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema ndani ya miaka mitano amewapa furaha Wazanzibari na wanahitaji maendeleo zaidi badala ya maneno matupu.

“Asiyeyaona haya, asiyeyasikia haya huyo atakuwa sio wa kuona wala kusikia hata pepo hawezi kusikia wala kuona,” amesema Abdulla.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohamed amesema wananchi hawahitaji dharau, kebei na chuki, badala yake wanahitaji maendeleo na maendeleo hayo hayana dini, chama wa kabila.

“Tusipandikize chuki kwa wananchi wetu, kinachohitajika ni maendeleo na haya ndio maendeleo yenyewe” amesema.

Nao baadhi ya wafanyabiashara katika eneo hilo wamesema awali walikuwa wakiendesha biashara zao katika matope, lakini baada ya kukamilika soko hilo wanaimani biashara zao zitakuwa katika mazingira mazuri.

“Tunaamini biashara zetu zitakuwa katika mazingira mazuri na kuvutia wateja wengi zaidi, hatua tunayoamini itatuongezea vipato,” amesema Hassan Haji Ame mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo.