Dk Nchimbi aahidi wazawa kushiriki uchimbaji madini, miradi ya maendeleo Kahama

Kahama. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho kikitapata ridhaa ya kushika dola katika uchaguzi mkuu, kitahakikisha madini yote ya kimkakati yanachimbwa na Watanzania.

Amesema, kama si wazawa kuchimba wao moja kwa moja basi ubia utakaoingiwa na wawekezaji utakuwa sawia ili rasilimali hiyo iwanufaishe zaidi wananchi.

Dk Nchimbi amesema hayo leo Alhamisi, Septemba 4, 2025 katika mkutano wa kampeni wa kumwombea kura, mgombea urais wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan uliofanyikia stendi ya malori, Kahama Mjini, Mkoa wa Shinyanga.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali ya CCM chini ya Rais Samia itahakikisha thamani ya madini yanayochimbwa mjini yanachenjuliwa hapahapa nchini kwa kujenga viwanda vyetu wenyewe.

“Miaka mitano ijayo, tunakwenda kushughulika na madini ya kimkakati. Tutahakikisha tunachimba madini yetu wenyewe au kwa kushirikiana na wabia. Kama ina hisa ni hisa kweli, kama mapato ni nusu ni nusu kweli, kama ni robo ni robo kweli, CCM inasema haitakubali tena Watanzania kunyonywa,” amesema Dk Nchimbi.

Miongoni mwa madini hayo mkakati ni Graphite, Nickel, Cobalt, na Heavy Mineral Sands.


Katika mkutano huo mkubwa, Dk Nchimbi amesema mambo mengine wanayokwenda kuyafanya ni kusukuma kasi ya mradi wa maji wa ziwa Viktoria ili kupunguza adha ya maji Kahama na maeneo mbalimbali.

Ameahidi, katika kupunguza adha ya ajira, mashamba darasa 60 yataanzishwa ili kuwezesha kuchagiza shughuli za maendeleo ya wananchi wa Kahama.

Dk Nchimbi amesema, katika kipindi hicho cha miaka mitano ijayo, watajenga soko Kahama ambalo litakuwa na maduka 184, vizimba 200:”Hii ni kuhakikisha watu wanakuwa na shughuli za kufanya. Kwa sababu watani zangu Wasukuma msipokuwa na kazi, mnashinda mnaimba tu.”

Amesema mashamba hayo ni kwa ajili ya kuwafundisha wakulima na wafugaji mbinu bora za kilimo na ufugaji wa ng’ombe wa kisasa endapo chama hicho kitaaminiwa tena kushika dola.

Amesema mashamba darasa hayo yatakuwa chachu ya kuongeza tija kwenye kilimo, kuimarisha mifugo na kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja hususani vijana wa Kahama.

“Endapo kama CCM itapewa ridhaa ya kuongoza tena, itaanzisha mashamba darasa 60 katika Wilaya ya Kahama, kwa ajili ya kufundisha watu ufugaji wa kisasa wa mazao kukuza uchumi wa wananchi wetu.”

Sambamba na mashamba hayo, Dk Nchimbi ameeleza kuwa serikali ya CCM itaanzisha skimu nne za umwagiliaji wilayani humo.

Amesema skimu hizo ni pamoja na skimu ya umwagiliaji Lowa katika kata ya Nyandekwa, Iyenze kata ya Iyenze, Kahanga katika kata ya Wendele na Malenge katika kata ya Isagehe, ili kusaidia katika kuinua kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa Taifa.

Awali, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa amekihakikishia chama hicho ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Amesema mkoa huo ulishika nafasi ya pili kwa kura nyingi za CCM katika uchaguzi mkuu wa 2020 na kwamba uchaguzi huu wamejipanga kuhakikisha wanashika nafasi ya kwanza.

“Utekelezaji wa ilani iliyopita ya CCM kwenye mkoa wetu wa Shinyanga ni mkubwa sana na sisi tutahakikisha kura za mwaka huu zinatosha kwa CCM. Oktoba 29 tunaenda kushinda kwa kura nyingi ambazo haziwahi kutokea.”

Mlolwa amesema:”Na hii tumeshakubaliana kwa pamoja, uchaguzi uliopita tulishika nafasi ya pili kwenye kura za CCM, uchaguzi huu tunaenda kushika nafasi ya kwanza, iwe mvua iwe jua, tunaenda kulipa deni la mama Samia kwa wema aliotutendea kwa kumpa kura nyingi.”