Equity kushirikiana na TALEPPA kufufua sekta ya ngozi

Dar es Salaam. Benki ya Equity Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chama cha Watengenezaji wa Bidhaa za Ngozi Tanzania (TALEPPA), hatua inayolenga kufungua minyororo ya thamani katika sekta ya ngozi na kuchochea mapinduzi ya kiuchumi kupitia uzalishaji wa viatu vya shule.

Makubaliano hayo yameambatana na uzinduzi wa Mradi wa Viatu vya Ngozi vya Shule Tanzania (TALSSI), mradi unaotarajiwa kuongeza ajira kwa maelfu ya Watanzania na kuongeza mchango wa sekta ya ngozi katika pato la taifa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Sempeho Manongi, aliyekuwa mgeni rasmi, aliipongeza Equity kwa kuonyesha mfano katika kufadhili sekta ambayo kwa muda mrefu imechukuliwa kuwa “haikopesheki.”

“Kwa muda mrefu sekta ya ngozi imeonekana kama haikopesheki. Equity wameonyesha njia, sasa ni wakati wa taasisi nyingine za fedha kuwekeza katika viwanda vidogo na vya kati,” alisema Manongi.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Kilimo Biashara wa Benki ya Equity, Teofora Madilu, alisema benki imejipanga kubadilisha mtazamo wa sekta ya mifugo kwa kuhakikisha thamani inayopatikana kwenye ngozi inanufaisha pia wafugaji.

“Tumetenga mikopo mahsusi kwa wafugaji, wauzaji wa ngozi mbichi na viwanda vidogo ili kutatua changamoto ya mitaji. Tukishirikiana na TALEPPA tunaweza kufanikisha mapinduzi makubwa ya viwanda vya ngozi nchini,” alisema Madilu.

Naye Katibu wa TALEPPA, Timoth Funto, alisema chama hicho kimeandaa mpango wa kuzalisha jozi milioni 10 za viatu vya shule kwa mwaka vyenye thamani ya takribani Sh300 bilioni.

Funto alisema hatua hiyo, inaweza kuajiri watu zaidi ya milioni mbili na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye uchumi.

Hata hivyo, Funto alibainisha changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwamo miundombinu duni, ukosefu wa teknolojia ya kisasa na sera zisizo rafiki, ambazo zimefanya bidhaa za ndani kushindwa kushindana.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa, Tanzania huagiza zaidi ya jozi milioni 54 za viatu kila mwaka, huku uzalishaji wa ndani ukibaki chini ya milioni tano, hali inayodhihirisha nafasi kubwa ya sekta ya ngozi katika kupunguza uagizaji na kuongeza thamani ndani ya nchi.