Gombo amwaga sera Shinyanga amtaja Mpina, Lissu

Shinyanga. Mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo, ameahidi kufuta gharama za matibabu, elimu hadi chuo kikuu, pamoja na mikopo ya watumishi wa umma mara tu atakapochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza leo, Septemba 4, 2025, wakati wa kampeni za kuomba kura kwa wananchi zilizofanyika katika Stendi ya zamani, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, Gombo amesema kuwa taifa lina rasilimali nyingi zinazotosha kutoa huduma bora kwa wananchi bila kuwatoza fedha zao.

“Tutatumia utajiri wa taifa letu  madini, kilimo, na ufugaji  kugharamia huduma muhimu kama afya, elimu na ustawi wa watumishi wa umma. Sio sahihi kwa wananchi kulipia huduma hizi wakati rasilimali hizi zinatosha kabisa kuiendesha nchi,” amesema Gombo.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali yake itahakikisha kuwa kila Mtanzania anafaidika moja kwa moja na rasilimali za nchi, badala ya utajiri huo kunufaisha watu wachache.

 “Mkinichagua mimi nitafuta gharama za matibabu, elimu bure kuanzia chekechekea hadi chuo kikuu, kufuta vikokotoo sambamba na mikopo ya majeshi yote ya Tanzania na watumishi wa umma wanaodaiwa na benki” amesema Gombo.

Pia, ameongeza kuwa, “Mpina (Luhaga) ana kesi inaendelea mahakamani mara tu nikishika kiti cha urais nitafungua milango ya magereza na kumwachia huru Lissu (Tundu),” ameongeza Gombo.

Naye mgombea mwenza Husna Mohammed Abdallah akiomba kura kwa wananchi wa Shinyanga ameeleza juu ya utajiri wa madini uliopo mkoani Shinyanga huku akigusia maisha duni wanayoishi wananchi.

“Utajiri uliopo mkoani Shinyanga na maisha mnayoishi havifanani elimu duni, maisha duni, mimi siijui Shinyanga ila nilipoingia hapa nikaambiwa hii ndio mjini nikajuiliza sasa huko vijijini pana hali gani, chagueni viongozi wa CUF tupate haki sawa kwa wote,” amesema Husna.

Hata hivyo, mwenyekiti wa CUF ngazi ya Wilaya ya Shinyanga,  Maarufu Hassan Maarufu katika kuwaombea kura viongozi wa CUF ameeleza kuwa wakulima watapanga bei mazao na kugusia mshahara wa wahudumu wa afya,

“Mkitupa kura za ndio CUF tutahakikisha bei ya mazao mfano pamba inapangwa na wakulima wenyewe kwa sababu ndio wanajua machungu wanayopitia hadi kuzalisha, pia madaktari na wahudumu wa afya watalipwa kutokana na utendaji wao wa kazi,” amesema Maarufu.