Hatari iliyopo watumiaji ‘system charge’ za simu

Shinyanga. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi duniani, takribani nchi 144 zimepitisha sheria zinazolenga kulinda data binafsi za raia wao.

Sheria hizi zinawahusu watu takribani bilioni 6.64, sawa na asilimia 82 ya watu wote duniani. Hii ina maana kuwa karibu asilimia 83 ya watu duniani wapo chini ya sheria za ulinzi wa taarifa binafsi.

Mtaalamu wa masuala ya usalama wa mtandaoni kutoka shirika la Jamii Afrika, Emmanuel Mkojera, akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, ameonya juu ya hatari zinazoweza kumpata mtu anayetumia mfumo wa kuchaji simu kwa kutumia USB pekee (bila kutumia kichwa cha chaja).

Ameeleza kuwa njia hiyo inaweza kusababisha udukuzi wa taarifa binafsi, jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa mtumiaji wa simu.

 “Kama hamna ulazima sana wa mtu kuchaji simu maeneo ya uma kwa kutumia waya wa USB pekee ni bora asichaji kwa sababu tofauti na kuchaji USB hutumika kuhamisha mafaili ya mtu kutoka kwenye kifaa kimoja hadi kingine mfano simu, kompyuta mpakato,” ameeleza Mkojera.

Pia, ameongeza kuwa; “Mara nyingi taarifa za watu binafsi husambaa kwa namna huyo mtu anachukua taarifa zako bila kujua na kuzitumia kwa namna isiyofaa kama kulaghai watu wengine sawa na udukuzi wa taarifa binafsi,” ameongeza Mkojera.

Baadhi ya watumiaji wa mfumo wa kuchagia simu katika maeneo ya umma wamekuwa na uelewa tofauti juu ya matumiazi ya mfumo huo, huku wengi wao kukosa elimu juu ya athari zinazoweza kuwakumba hasa za kimtandao,

“Sioni madhara kwa sababu mfumo huu unarahisishia watu wanaosafiri safari za mbali kuchaji simu zao kwa sababu unaweza kuta wengine hawana au hata mtu kasahau kuchaji simu akifika kwenye basi inakuwa rahisi kwake kuchaji na kurahisisha mawasiliano,” amesema Juma Abdallah.

Katika kuchangia hoja hiyo, Aneth Chamba ameeleza; “Binafsi sijui kama kuna madhara ninachokiona ni faida kwa watumiaji wa mabasi, treni au wanaosafiri kwa ndege huwa hii suluhisho bora katika dharura, pengine mtu anapokwenda ni mgeni halafu simu imezima mfumo huu unakuwa msaada mkubwa kwetu.”

Kwa upande wake Lightness Anania ameongeza kuwa uwepo wa huu mfumo katika maeneo ya umma unapunguza wasiwasi wa simu kuzima kwa sababu wengi wanatumia sana mtandao na simu zinaisha sana chaji, lakini mfumo unapunguza wasiwasi wa kuwaza mahali pa kuchaji.

Katika mtazamo wa kuishi kidigitali, Moses Joseph amesema kuwa mfumo huu ni muhimu kwa sababu unachangia katika kukuza teknolojia inayojali mahitaji ya kila siku kwa sababu tunaishi katika dunia ya kidigitali japo hakuna chenye faida kikakosa hasara.

“Kwa uelewa nilionao mfumo huu unachangia kutokuwa na usalama wa taarifa binafsi, kwa sababu unapochaji pale hujui nyuma yake wameunganisha nini japo sijui wanafanyeje wabobezi wananjua,” amesema Robert Nnko.

Jambo muhimu kwa watumiaji

Mkojera ameeleza kuwa kitu pekee mtu anatakiwa kufanya ni kukagua mpangilio wa mfumo wa simu yake anapotumia USB hasa katika maeneo ya umma kwa sababu haitakiwa kuamini chochote unachotumia kwenye kifaa chako.

“Kama mtu anatumia waya wa USB pekee katika kuchaji anatakiwa kuangalia simu kama inaruhusu kuchaji tu au pia kuhamisha mafaili kuepuka kupekuliwa taarifa binafsi, pia tunashauri ni vizuri mtu akatumia kichwa cha chaji wakati wa kuchaji ili kuwa salama zaidi” ameeleza Mkojera.