SIKU chache baada ya kocha Denis Kitambi kutua Fountain Gate, amemuongeza kwenye benchi lake la ufundi kiungo wa zamani wa Simba, Henry Joseph.
Joseph ambaye msimu uliopita alikuwa akiinoa Moro Kids inayoshiriki First League, ametua Fountain Gate kwa kazi mbili.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zinabainisha kuwa kazi ya kwanza, Joseph amekabidhiwa majukumu ya kusimamia utimamu wa mwili kwa wachezaji wa kikosi hicho.
“Mbali na hilo, pia atakuwa kocha msaidizi namba mbili baada ya Mohamed Ismail ‘Laizer’, wote wakimsaidia kocha mkuu Denis Kitambi,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilifichua kuwa, Joseph ambaye enzi zake mbali na Simba amecheza Kongsvinger ya Norway na Mtibwa Sugar, alifika kambini Septemba 2 mwaka huu kuanza majukumu yake rasmi.
Mwanaspoti lilipomtafuta Ofisa Habari wa Fountain Gate, Issa Liponda ‘Mbuzi’, kuzungumzia hilo alisema: “Ni kweli Henry Joseph yupo mazoezini akiendelea na majukumu aliyopewa. Tunaboresha benchi letu la ufundi na muda maalum wa kuwatambulisha wote ukifika kila kitu kitakuwa wazi.”
Sababu Mganda kuitosa Mtibwa Sugar
ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mganda Peter Lwasa, amekamilisha usajili wa kujiunga na Pamba Jiji cha jijini Mwanza, huku akiitosa ofa ya Mtibwa Sugar iliyokuwa ya kwanza kufanya mazungumzo na waajiri wake.
Iko hivi. Kagera iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu kwenda Championship, ilifikia makubaliano ya kumtoa kwa mkopo wa msimu mzima nyota huyo kujiunga na Mtibwa, lakini dili hilo lilikufa baada ya mwenyewe kutokuwa tayari.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza sababu ya Lwasa kuichagua Pamba badala ya Mtibwa ni kutokana na kuvutiwa na ‘project’ (mradi) wa kikosi hicho, kinachofundishwa kwa sasa na kocha mkuu raia wa Kenya, Francis Baraza.
“Kagera ilikubaliana kufanya biashara na Mtibwa kwa sababu ya uhusiano uliopo baina ya pande hizo mbili, ingawa mchezaji aligoma na kuomba uongozi umruhusu aende sehemu nyingine, au ikishindikana avunje mkataba wake,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, kiungo huyo aliyejiunga na timu hiyo Agosti 15, 2024 akitokea KCCA ya Uganda, alisaini mkataba wa miaka miwili, ingawa aliwataarifu viongozi mwaka mmoja uliobakia umevunjika kwa sababu ya Kagera Sugar kushuka daraja.
Mtoa taarifa huyo alisema uamuzi uliokuwa unataka kufanywa na Kagera iliyodai bado ana mkataba wa mwaka mmoja sio kweli, kwani makubaliano ya mwanzo yalikuwa endapo kikosi hicho kitashuka daraja utavunjika rasmi na ndicho kitu kilichotokea.
Nyota huyo aliyefunga mabao manane ya Ligi Kuu msimu uliopita, amechezea URA na KCCA zote za Uganda, Sofapaka, Kariobangi Sharks na Gor Mahia za Kenya, huku akiitumikia pia timu ya Lubumbashi Sports ya DR Congo.