TANZANIA imeshinda mechi yake ya pili ya michuano ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia kwa Kriketi ya mizunguko 20 (T20) baada ya kuifunga Kenya kwa mikimbio 30 katika mchezo uliopigwa mwanzoni mwa juma mjini Windhoek, Namibia.
Tanzania ndio walioanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 125 ikiwa imepoteza wiketi 8 baada ya kumaliza mizunguko yote 20.
Ulikuwa mlima mkubwa kwa Wakenya kwani juhudi zao ziligota kwenye mikimbio 95 baada ya wote kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 19 na hivyo kupoteza kwa mikimbio 30. Saum Mtae ndiye aliongoza kwa kutengeneza mikimbio akiwa amepiga mikimbio 30 kutokana mipira 19 akifuatiwa na Nasra Mohamed aliyepiga mikimbio 26 wakati Hudaa Omary na Neema Pius walitengeneza mikimbio 24 kila mmoja.
Aliyecheza vizuri kwa upande wa Kenya ni Kwes Lavendah Idambo aliyepiga mikimbio 18 na Veronica Abuga aliyetengeneza mikimbio 17.
Huu ulikuwa ushindi wa pili mfululizo kwa Tanzania baada na kuanza kampeni na ushindi kiduchu wa mkimbio 1 dhidi ya Uganda.