Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania sasa iko tayari kuanza usikilizaji wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, baada ya kuipangia tarehe ya usikilizwaji wa awali na jaji atakayeisikiliza.
Mmoja wa mawakili wa Lissu, Hekima Mwasipu, amelieleza Mwananchi leo Alhamisi, Septemba 4, 2025 kuwa kesi hiyo iliyosajiliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imepangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali ((preliminary hearing – PH) Jumatatu, Septemba 8, 2025 mbele ya Jaji Dunstan Ndunguru.
Jaji Ndunguru anakuja kusikiliza kesi hiyo akitokea Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, kwenye kituo chake cha kazi kwa sasa, akiwa ndiye Jaji Mfawidhi.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.
Anadaiwa kwamba akiwa na nia ya uchochezi, aliushawishi umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 na kusomewa shtaka hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu.
Kesi hiyo ilifunguliwa katika mahakama hiyo kwa ajili ya maandalizi ya awali, ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa upelelezi, kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu itakakosikilizwa katika hatua ya ushahidi na kuamuliwa.
Baada ya upelelezi kukamilika na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuridhika na ushahidi uliopatikana, aliwasilisha hati ya mashtaka Mahakama Kuu ambako ilisajiliwa na kuwa kesi rasmi iliyofunguliwa hapo kwa ajili ya hatua kuanza usikilizwaji na hatimaye kutolewa uamuzi.
Hivyo, Agosti 18, 2025, Mahakama ya Kisutu iliendesha mwenendo kabidhi (committal proceedings) na mshtakiwa alisomewa maelezo ya mashahidi wa Jamhuri ambao inatarajiwa kuwaita kutoa ushahidi mahakamani pamoja na vielelezo vya ushahidi vitakavyotumika.
Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, aliieleza Mahakama hiyo kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo Mahakama Kuu, Jamhuri inatarajia kuwaita mashahidi 30 na kuwasilisha vielelezo tisa.
Lissu alipopewa nafasi ya kueleza jambo lolote kama alikuwa nalo kabla ya amri ya Mahakama kuihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu, alitoa maelezo marefu ya utetezi wake dhidi ya shtaka hilo aliyokuwa ameyaandika katika kurasa 140.
Hata hivyo, wakati akiwa katikati, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, aliyeiendesha katika hatua hiyo ya uchunguzi wa awali, alimwelekeza aishie hapo na kwamba maelezo yake yote atayatoa Mahakama Kuu kesi hiyo itakaposikilizwa.
Pia, Lissu alitaja majina ya mashahidi wake anaotarajia kuwaita, lakini Hakimu Kiswaga alimkatisha na kumweleza kuwa hayo atayatoa Mahakama Kuu.
Baada ya kukamilisha hatua hizo, Hakimu Kiswaga alitangaza kufunga jalada la kesi hiyo mahakamani hapo na kuamuru kuwa sasa imehamishiwa Mahakama Kuu.
Jaji Ndunguru alikuwa mmoja kati ya majaji watatu waliounda jopo lililosikiliza kesi maarufu ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA) katika eneo la Bandari.
Kesi hiyo maarufu kama kesi ya Mkataba wa Bandari ilifunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mbeya na Alphonce Lusako na wenzake watatu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake mwaka 2023.
Walikuwa wakipinga kampuni ya Dubai Ports World (DP World) kukabidhiwa uendeshaji wa Bandari, wakidai mkataba huo ulikuwa unakiuka Katiba kwa kupora rasilimali hiyo ya Taifa.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilitupilia mbali kesi hiyo ikieleza kuwa madai ya wadai hao hayakuwa na mashiko, huku ikibainisha kuwa walishindwa kuthibitisha madai yao.