Jela miaka 15 kwa kumuua mkewe kwa mchi bila kukusudia

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mtwara, imemhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela, Shaibu Mtavira, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua bila kukusudia mkewe, Aziza Mtelia, kwa kumpiga na mchi kisha kumzika kwenye shamba lao.

Shaibu alikiri kumuua mkewe baada ya kutokea kutokuelewana  katika mazungumzo yao na kusababisha mapigano kati yao ambapo mke wake alianza kwa kumpiga na mwanzi ubavuni, yeye (Shaibu) akapata hasira akachukua mchi akampiga nao kichwani, akafariki dunia kisha akachimba shimo na kumzika.

Mwili wa Aziza (marehemu kwa sasa), uligunduliwa Aprili Mosi, 2024 ukiwa umezikwa kwenye shamba ambapo baada ya Shaibu kukamatwa alikiri kumuua mkewe.

Aidha, katika maelezo yake ya onyo pamoja na maelezo ya ziada, Shaibu alikiri kusababisha kifo cha mke wake huku mbele ya Mahakama hiyo akikiri mbele ya Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya mauaji kuwa ni kweli amemuua mke wake ila anaomba msamaha kwani hakufanya hivyo kwa makusudi, ilitokana na hasira.

Shaibu alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shtaka la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Hukumu hiyo imetolewa Septemba 3, 2025 na Jaji Martha Mpaze, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya mauaji na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jaji Mpaze amesema mahakama imeona upande wa mashtaka haujathibitisha pasipo shaka yoyote kuwa mshtakiwa alimuua mkewe kwa nia mbaya, hivyo kumtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia na kumhukumu kifungo cha miaka 15 jela.

Katika utetezi wake, Shaibu alidai kuwa alitenda kosa hilo bila kuwa na nia ya kuua na kuwa tukio hilo lilitokea kutokana na hasira kufuatia mzozo baina yao.

Alieleza kuwa siku ya tukio kulitokea kutokuelewana baina yao kuhusu unywaji wa pombe na kukiri kumpiga mke wake hali iliyosababisha kuanguka na kufariki dunia.

Aidha, alikana kuukata mwili huo, akidai kuwa alimzika tu ambapo alionyesha majuto, akaomba msamaha.

Jaji Mpaze amesema katika kesi za namna hii, hata bila kutaja mamlaka yoyote, upande wa mashtaka una wajibu wa kuthibitisha pasipo shaka yoyote kwamba marehemu amekufa kifo kisicho cha asili na kwamba kilisababishwa na mshitakiwa.

Amesema katika kesi hiyo, Aziza (marehemu kwa sasa) kifo chake kilithibitishwa na matokeo ya uchunguzi wa daktari ambaye alithibitisha kifo hicho hakikuwa cha asili.

Kuhusu utambulisho wa mtu aliyesababisha kifo chake, mshtakiwa mwenyewe alikiri mbele ya mahakama hii kuwa alihusika. Kwa maneno yake mwenyewe, amenukuliwa akisema;

“Madam Jaji, ni kweli nimemuua mke wangu. Ninaomba msamaha wako kwa dhati, sikufanya kitendo hiki kwa makusudi; ilitokana na hasira. Ninaomba kwa unyenyekevu, Madam Jaji, kwamba nimejifunza somo langu na sitarudia tena.”

Shaibu hata alipohojiwa na Wakili wa Serikali, alithibitisha yeye ndiye aliyemuua mke wake na ndiye alimzika kwenye shimo alilokutwa.

Jaji Mpaze amesema ingawa mshtakiwa amekiri kusababisha kifo cha mkewe, kwa sasa suala kuu la kuamuliwa na mahakama hiyo ni kama kifo hicho kilifanywa kwa makusudi.

Jaji amesema kuwa ni wazi kuwa uovu uliofikiriwa kabla unaweza kuthibitishwa na kuwa katika kudhihirisha mazingira ambayo uovu uliotangulia unaweza kutolewa, akinukuu kesi mbalimbali za mahakama ya rufaa.

Ameeleza kuwa katika kesi hiyo hakuna shahidi hata mmoja aliyemwona mshitakiwa akimwua marehemu na kuwa upande wa mashtaka, hasa kupitia kwa shahidi wa kwanza, SSP Christopher Msonsa na shahidi wa sita, G7988 Sajenti Fanuel, walitaka kubaini nia mbaya kutokana na maneno ya mshtakiwa mwenyewe.

Kwa mujibu wao, mshtakiwa alieleza kuwa alimpiga marehemu kwa ‘mwichi’ (mchi), kisha kuchukua panga, kuukata mwili huo, kuuzika, na kisha kukaa kimya kwa miezi kadhaa.

Kwa upande mwingine, mshitakiwa huyo anakiri kuwaeleza mashahidi hao mambo mengi waliyoyasema, isipokuwa tuhuma ya kuukata mwili huo, jambo ambalo alilikanusha na kusisitiza kuwa alimzika marehemu.

Jaji Mpaze amesema maelezo ya onyo ya mshtakiwa na maelezo ya ziada ambayo yalikubaliwa mahakamani hapo, yanawiana na kile alichokieleza mahakama katika utetezzi wake na kuwa maelezo ya onyo yana madai ya ziada kuwa aliukata mwili huo, jambo ambalo alilikanusha vikali katika utetezi wake.

“Hata hivyo, kwa kutumia kanuni kwamba kutokwenda lazima kutatuliwe kwa niaba ya mshtakiwa, ninaona taarifa ya ziada ya mahakama, ambayo inaambatana na ushuhuda wa kiapo wa mshtakiwa, kuwa ya kuaminika zaidi,”amesema Jaji

Jaji alinukuu sehemu ya maelezo hayo yaliyoandikwa mbele ya Jaji wa Amani, Ediwni Lutalemba, ambapo mshtakiwa alisema akiwa amekaa nje ya nyumba yake akisubiri chakula mke wake alipeleka chakula akawa anakula peke yake.

“Na yeye akamega matonge mawili akawa anatema ovyo kwa kulewa, mara akaingia ndani na akatoka nje akaenda kuchukua pombe aliyokuja nayo akaificha kwa nje akaanza kumimina kwenye kikombe nikaenda nikamyang’anya ile chupa nikaitupa, nikiwa nimekaa mke wangu alichukua mwanzi akaja akanipiga nao ubavuni.

“Ndipo kwa hasira nikachukua mwichi nikampiga nao kichwani akapoteza maisha yake, asubuhi yake kutokana na woga niliokuwa nao, kwani sikuwahi kufanya kitendo kile ndipo nilichukua jembe nikachimba shimo nikafukia mwili wa marehemu ili kupoteza ushahidi, nikarudi nyumbani kupumzika,” ni sehemu ya maelezo hayo.

Jaji amesema katika utetezi wake mbele ya mahakama, mshtakiwa alitoa maelezo yanayofanana kwa kiasi kikubwa, ambapo amenukuliwa akisema;

“Alipotoka tena akaja na ‘mwanzi’, akanipiga na mbavu nilimuuliza kwa nini ananipiga, akasema wewe ni mwanaume wa aina gani, fyoko utanifanya nini?

“Nilikasirika, nikamchukua mchi na kumpiga. Alishuka chini, nikamuacha pale na kuingia ndani kulala nikiamini ataamka, kumbe nilikuwa naangalia hakuamka. Asubuhi, ilibidi nichimbe shimo ili kumzika.”

Jaji alihitimisha kuwa kosa la mauaji bila kukusudia limethibitishwa siyo na kuwa mahakama inaona kuwa upande wa mashtaka haujathibitisha pasipo shaka yoyote kuwa mshtakiwa alimuua marehemu kwa nia mbaya.

“Mahakama inampata  mshtakiwa na hatia na kumtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia chini ya kifungu cha 195 na 198 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,”

Jaji amehimitisha kwa kumpunguzia mshtakiwa adhabu kutoka miaka 20 hadi kumhukumu miaka 15, kutokana na muda aliokaa mahabusu, kwa kuzingatia umri wake na kwa kutambua ushirikiano alioutoa polisi na mahakamani.