Jeshini kuna vita ya majirani CECAFA Kagame Cup

MIAMBA miwili ya soka la Sudan na Somalia, Al-Hilal Omdurman na Mogadishu City, itakuwa vitani leo Alhamisi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, kutupa karata zao za kwanza katika mashindano ya Kombe la Kagame.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana kwenye michuano hiyo mikongwe ya klabu za Afrika Mashariki na Kati, huku kila moja ikitazamia kuanza vizuri dhidi ya mwenzake.

Bingwa mtetezi wa michuano hii ni Red Arrows kutoka Zambia ambayo hata hivyo haijaalikwa kushiriki msimu huu. Al-Hilal Omdurman, moja ya klabu kongwe na zenye mafanikio makubwa huko Sudan, itashuka dimbani ikiwa na kikosi chenye nyota wapya ambao wamesajiliwa siku chache zilizopita.

Miongoni mwao ni mshambuliaji Sunday Adetunji, aliyejiunga akitokea Ballkani ya Kosovo, pia yupo Mohamed Al-Mustafa kutoka Azam FC ya Tanzania, pamoja na kiungo Issouf Kabore kutoka Majestic FC ya Burkina Faso.

Kama ilivyo kwa Singida BS, Al Hilal nayo inatumia michuano hii kama sehemu ya kujiandaa na michuano ya kimataifa.

Kwa upande mwingine, Mogadishu City, ambayo inahistoria ya kipekee katika soka la Somalia, itashuka dimbani ikiwa na ari kubwa ya kuonyesha kuwa mabingwa wa Somalia wanaweza pia kutikisa ukanda huu. Mogadishu City ilianzishwa miaka 62 iliyopita na imekuwa nembo ya michezo nchini humo. Klabu hiyo ilitwaa ubingwa wa 11 wa Ligi Kuu Somalia msimu uliopita, rekodi inayodhihirisha ubora wao.

Mbali ya soka, Mogadishu City inajivunia kuwa kati ya klabu chache zenye muundo mpana wa michezo Afrika Mashariki, ikimiliki timu za mpira wa kikapu, mpira wa mikono, tenisi ya meza, tenisi ya kawaida, mpira wa wavu, kuogelea, riadha na baiskeli.

Uwepo wa timu hizo mbalimbali umekuwa chachu ya kuinua vipaji vipya na kuimarisha nafasi ya klabu hiyo kuwa kielelezo cha michezo ya ushindani huko Somalia.