Mbeya. Jeshi la Magereza Mkoa wa Mbeya limesema tangu kuanza matumizi ya nishati safi, limepata unafuu wa kupunguza gharama, kuokoa muda na kutoa mwanga katika uhifadhi na utunzaji mazingira, huku likieleza mkakati wa kuwafikia wananchi kuondokana na nishati chafu ya kupikia.
Mkuu wa Gereza la Ruanda Mbeya, Christopher Fungo anasema tangu mwaka jana, gereza hilo limeshaachana na matumizi ya kuni badala yake wanatumia makaa ya mawe na gesi.
Anasema kwa sasa jeshi hilo ni sehemu ya balozi katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, akibainisha kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi walio karibu na gereza hilo kuachana na nishati chafu.
“Tunaelimisha jamii iliyotuzunguka kuhusu umuhimu na faida ya matumizi ya nishati safi kwa kila kaya, kwa upande wetu magerezani tumeshasahau matumizi ya kuni tangu Desemba mwaka jana na mafanikio ni makubwa sana.
“Tangu kuanza matumizi nishati safi, tumeokoa gharama na muda katika shughuli, kwa sasa ni mabalozi kwenye kampeni hii na tunaihamasisha jamii iliyotuzunguka kutumia nishati hii,” anasema Fungo.
Kamishna huyo msaidizi, anabainisha kuwa kwa kipindi cha nyuma, taasisi hiyo ilitegemea kukata miti ilikutumia kama nishati, lakini kwa sasa wanajitahidi kufanya utunzaji na uhifadhi mazingira.
Anasema katika kufikia malengo, jeshi kwa Mkoa wa Mbeya limejiwekea mkakati wa kupanda miti kila mwaka ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye kuhamasisha utunzaji mazingira.
“Tunaishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuwa wamekuwa karibu na sisi na hivi karibuni, tumepokea mitungi ya gesi 250 kwa ajili ya watumishi ikiwa ni njia ya kila kaya kuachana na kuni,” anasema Kamanda huyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya Vijijini, Erica Yegella, anasema kwa sasa mkakati wa mkoa huo ni kila mwananchi kuachana na nishati chafu.
Erica aliyezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa anasema matumizi ya nishati safi yanaokoa maisha kwa watumiaji na kuwaweka sawa kiafya, akieleza kuwa mkoa huo ni wa kilimo, hivyo wananchi wanapaswa kuzingatia utunzaji mazingira.
“Nishati safi inatusaidia kuondoa hewa ukaa, hivyo tuzingatie matumizi bora ya nishati safi, mkoa wetu ni wa kilimo zaidi, tujitahidi sana kutokata miti hovyo ili kutunza mazingira,” anasema Erica.
Amewataka wananchi katika mkoa huo kuondokana na matumizi ya nishati chafu hasa mkaa na kuni, kwa kuwa huzalisha hewa ukaa, akibainisha kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri kila mmoja kufikia malengo.
Pia, aliomba wadau mbalimbali wanaosaidia kuhamasisha juu ya matumizi ya nishati safi kutoa elimu kwa jamii na kuwafikia maeneo yote ili kuweza kufikia malengo ya Serikali.
“Tuwapongeze wadau mbalimbali wanaojitolea kwenye matumizi ya nishati safi kufika maeneo yote yakiwamo ya vijijini, lengo ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na kampeni hii,” anasema Erica.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda anasema Serikali imeweka mkakati bora kwa askari wa Magereza kwa kuwagawia majiko ya gesi na tayari Gereza la Ruanda limeshapokea.
Anasema Serikali imeendelea kuhimiza na kusapoti Magereza zote za Mbeya kuhakikisha wanatumia nishati safi ya kupikia akieleza kuwa,hatua hiyo inaenda kusaidia kufikia malengo.
“Matumizi ya nishati safi si ya mtu mmoja, zile taasisi binafsi na za umma zenye mtu kuanzia mmoja, zinatumia nishati safi, hali hii itasaidia kupunguza gharama na kuokoa muda,” anasema Itunda.
Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Women Empowerment Network (Tawen), Frolence Masunga anasema katika kuunga mkono Serikali kwenye nishati safi, wameamua kutembea Mkoa wa Mbeya hasa vijijini kutoa elimu kwa jamii, lakini changamoto inayojitokeza ni bei na upatikanaji wa nishati hizo.
Anasema kuhusu bei ya mkaa mbadala kupungua, ni jambo linalowezekana akibainisha kuwa wazalishaji wamekuwa na ubora wa bidhaa katika kumsaidia mwananchi kuweza kutumia kwa ubora.
Anasema matarajio ya shirika hilo kupitia makongamano ni kukutana na wabunifu wa mikaa hiyo wakiwamo Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuhakikisha bei inakuwa ya chini na kuwafikia wananchi wote maeneo ya vijijini.
“Tunaendelea kuhamasisha wananchi kuondokana na nishati chafu kwa ustawi wa afya yao, vijijini huku ndio wanatumia zaidi kuni, hivyo Tawen tumeamua kufika maeneo hayo kutoa elimu na kuhamasisha nishati safi.
“Tunalenga hadi kufikia 2034 asilimia 80 ya jamii itumie nishati safi kama Serikali ilivyoahidi kwenye Mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya Kupikia, tumelibeba hili kwa nguvu zote kuhakikisha malengo yanafikia na watu wanafanya shughuli zao za uchumi kwa maisha bora,” anasema Frolence.
Anasema kuwa, mkakati ni kuhakikisha taasisi zote zenye watu kuanzia 120 wanatumia nishati safi, akibainisha kuwa hali hiyo itasaidia utunzaji mazingira na kuchochea maendeleo kwa jamii.
Mhandisi Collins Mwapwele kutoka Stamico ambao ni wazalishaji wa mkaa wa mawe, anasema mkaa wanaozalisha ni wa kiwango na kwa bei nafuu ikilinganishwa na wa kuni.
Anasema mkaa huo unaweza kutumika kwa mahitaji yoyote na unakaa kwa muda mrefu na hauna moshi wowote akibainisha kuwa, kwa watumiaji wanaweza kuutumia muda wowote bila athari.
Anasema katika kuunga mkono kampeni ya nishati safi, Stamico inalenga kuzalisha mkaa wa mawe kwa wingi akiwaomba wananchi kuzingatia matumizi sahihi ili kuondokana na changamoto zozote kwa kutumia kuni.
“Kwanza bei yake ni nafuu ukilinganisha na mkaa wa kuni, unaweza kukaa zaidi ya masaa matano na hauna moshi, Stamico imejipanga kuendelea kuzalisha mkaa wa mawe wenye ubora kwa jamii.
“Niwaombe wananchi kufuata ushauri na kuondokana na nishati chafu ambayo imekuwa na madhara mengi, inapoteza muda na kugharimu zaidi, tumejipanga mkaa huu kuwafikia wananchi wote hadi vijijini” anasema Mhandisi huyo.
Baadhi ya waannchi mkoani Mbeya wanasema ili kufikia malengo, Serikali inapaswa kuweka sheria na adhabu kwa wanaoendelea kutumia kuni katika kupika na katazo la ukataji miti.
Pia, wanashauri uwapo wa uhakika wa mkaa mbadala katika maeneo yote yakiwamo ya vijijini na elimu badala ya huduma hizo kuishia sehemu za mijini, wakieleza kuwa bila juhudi binafsi utekelezaji unaweza kutofikia.
Magdalena Mwampamba mkazi wa Mbalizi anasema zipo kaya zenye watu zaidi ya 10, lakini matumizi yao ni kuni, hali ambayo ni ngumu kuhamia katika nishati safi bila kupewa katazo na elimu.
“Hadi sasa wapo ambao hawajui maana ya nishati safi hasa maeneo ya vijijini, Serikali kama imeamua kutupeleka kwenye teknolojia hiyo, isione kupoteza gharama au muda kutufikia kutuelimisha.
“Zipo familia zenye watu zaidi ya 10 wanatumia kuni, sasa bila kufika huko na kuweka sheria na katazo tunaweza kuishia kuzungumza bila kutenda, tunajua asili ya wengi wamekua kwa kupikia kuni,” anasema Magdalena.
Christopher Temu anasema iwapo Serikali imeamua wananchi watumie mkaa wa mawe na nishati mbadala, ihakikishe wazalishaji na wabunifu wanasambaza huduma hizo maeneo yote na kwa bei nafuu.
Anasema hadi sasa mitungi ya gesi bado bei yake ni kubwa ikilinganishwa na kipato cha mtu mmoja mmoja, hivyo ili kurahisisha na kumsaidia mwananchi wa kawaida, iwepo huduma ya uhakika na yenye bei elekezi na inayowezekana.
“Mfano mitungi ile midogo inauzwa kwa Sh24,000 sasa kwa mtu wa kawaida anayetegemea kilimo huko vijijini unamwambia anunue gesi hiyo, haitoshi mkaa mbadala haupatikani, Serikali ilitazame hili,” anasema Temu.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.