Masache aomba kuunganishwa barabara Makongorosi-Tabora akiomba kura za Urais

Mbeya. Mgombea pekee ubunge Jimbo la Lupa, Wilaya ya Chunya Masache Kasaka ameomba mgombea Urais atakapoapishwa na kuunda Serikali, kuboresha miundombinu barabara kutoka Makongorosi ili kuunganisha shughuli za kiuchumi baina ya Mkoa wa Mbeya ya Tabora.

Mbali na Ombi hilo pia Masache ameomba maeneo ya wachimbaji wadogo kufikishiwa nishati ya umeme kufuatia wananchi wake kujikita kwenye shughuli hizo ili kuchochea shughuli  za kiuchumi.

Masache amewasilisha ombi hilo Septemba 4, 2025 baada ya kupewa fursa ya kutoa  kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za kumuombea kura mgombea wa  kiti cha  Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Uwanja wa Ndege jijini hapa.


Masache amesema serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi hususani  katika sekta ya afya na  kupandisha hadhi kituo cha afya cha halmashauri  ya Chunya kuwa Hospitali ya Wilaya.

“Mwenyekiti wa CCM na Mgombea Urais  Rais Samia Suluhu tunaona mambo mengi umeyafanya katika Serikali  ya awamu ya sita, lakini kuna changamoto  ya nishati  ya umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo  Wilaya ya Chunya,”amesema Masache.

Masache amesema katika maeneo ya vijijini Serikali imefika nishati hilo kwa kiwango  kikubwa changamoto ni baadhi ya maeneo ya wachimbaji  wadogo  wa madini ya dhahabu.


“Mh Rais neno  letu ni  moja nimetumwa na wananchi  wa Lupa ni  kukushukuru ila ombi lao kuomba ujenzi wa barabara kwa kiwango cha rami kutoka Makongorosi mpaka Kijiji cha Mkiwa ili kuunganisha  mawasiliano ya Mkoa wa Mbeya na Tabora na kuchochea shughuli za kiuchumi,”amesema.

Kwa upande wake Mgombea  wa jimbo la Mbarali ,Bahati Ndingo ameomba kuharakishwa ujenzi wa barabara njia nne kutoka Igawa mpaka Songwe mkoani hapa.

“Sisi Mbarali tunakuhaidi kura za kishindo na kesho unakuja katika Wilaya yetu kwenye mkutano wa kampeni tunakuhaidi kura za kishindo Oktoba 29,2025, “amesema Ndingo.