Mbeya. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameombwa atakapoingia madarakani kupandisha hadhi mamlaka ya Mji wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya ili kuboresha shuguli za kiuchumi.
Ombi hilo limetolewa leo Alhamisi Septemba 4, 2025 na mteule wa ugombea ubunge wa Jimbo la Mbeya Vijiji, Patali Shida ambayo pia iliungwa mkono na aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Rungwe, Sophia Mwakagenda.
Awali, mgombea Jimbo la Mbeya, Patali amesema Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka minne imefanya mambo makubwa hususani kutenga zaidi ya Sh6 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali hususani katika sekta ya afya.

Amesema Jimbo la Mbeya Vijijini tangu kuanzishwa kwake mwaka 1980 haikuwahi kupata Hospitali ,lakini kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia wamepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya sita na zahanati 10.
“Mgombea urais tumepata zahanati 10 vituo vya afya sita jambo ambalo limeboresha upatikanaji wa huduma bora za afya zikiwepo za mama na mtoto wakati wa kujifungua,” amesema.
Katika hatua nyingine Patali amesema asilimia 85 ya wananchi Mbeya Vijijini wanajihusisha na shughuli za kilimo huku jumla ya wananchi 110,000 wamesajiliwa kwenye mfumo wa mbolea na mbegu za ruzuku.
“Wilaya ya Mbeya mahitaji ya chakula ni tani 200,000, lakini uzalishaji wetu mpaka sasa hivi ni tani 600,000 haya yote ni uwekezaji wa Serikali ya awamu ya sita na utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi 2020/25,” amesema.
Patali amesema mbali na mafanikio hayo wanashukuru kwa maelekezo ya ujenzi wa barabara njia nne hali ambayo itaokoa maisha ya watanzania yaliyokuwa yanakatishwa katika mteremeko wa mlima Iwambi na kupunguza foleni.
Patali amesema kufuatia mamlaka hiyo kuwa ndogo amemuomba Rais Samia kama ikimpendeza wakati michakato ikiendelea ya kupitia halmashauri zitakazo pandishwa hadhi Mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi ipewe kipaumbele.
“Mh Rais ukitazama mji wa Mbalizi na maendeleo yaliyopo,unatuletea barabara njia nne na Uwanja wa Ndege wa Songwe na viwanda vidogo, tunaomba ikikupendeza pandisha hadhi mji huu ili tukutendea haki,”amesema.
Ombi hilo limeungwa mkono na aliyekuwa mgombea jimbo la Rungwe, Sophia Mwakagenda ameomba mji huo uwe kamili kutokana na kuwa na Mamlaka ya kubariki ombi lao.
“Wanambalizi Oktoba 29, 2025 tukampatia kura za kishindo Rais Samia Suluhu Hassan, lakini ninaamini umebakisha kuapishwa mengine unafanya kama taratibu za kiuchaguzi,”amesema.

Mfanyabiashara wa viazi mviringo amesema endapo Serikali ikaridhia kupandisha hadhi mamlaka hiyo shughuli za kiuchumi zitatanuka na kuchochea mapato ya Serikali.
“Tunaona Mji wa Mbalizi unatanuka kila wakati hususani shughuli za kiuchumi na kilimo nasi tunaunga mkono kauli ya mgombea ubunge wetu mwenye maono ya kuleta maendeleo ya kweli,”amesema.
Katika hatua nyingine wameomba kuboresha miundombinu ya barabara za pembezoni ili kurahisisha kusafirisha mazao kutoka sehemu mija kwenda nyingine, “amesema.
Akihutubia wananchi wa Mamlaka ya Mji wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya, mgombea urais Samia Suluhu Hassan amesema suala hilo liko kwenye mchakato litapita Tamisemi na wakipika serikalini wataangalia la kufanya.