MGOMBEA URAIS CCM RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AENDELEA KUCHANJA MBUGA… AHUTUBIA MAELFU YA WANANCHI MBALIZI

*Atoa maelekezo kwa wakulima kuendelea kujisajili katika mfumo wa kupata Mbolea ya ruzuku,pembejeo.

*Aahidi mambo makubwa katika miaka mitano ijayo …agusia kuendelea kuboresha huduma za kijamii

 Na Said Mwishehe,Michzuzi TV-Mbalizi

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuchanja mbuga ambapo leo Septemba 4,2025 amehutubia maelfu ya wananchi Mji Mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya huku ahadi yake kubwa ikiwa ni kuendelea kufanya mambo makubwa zaidi katika miaka mitano ijayo.

Aidha Mgombea Urais ,Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwahakikishia Watanzania kuwa inatambua mchango wa wakulima nchini na hivyo ameahidi kuwa Serikali itaendelea na mpango wake wa kutoa Mbolea na pembejezo za ruzuku huku akiwataka wakulima kuendelea kujisajili katika mfumo wa mbolea na pembejeo za ruzuku kwani Mbolea ya ruzuku bado ipo na itaendelea kutolewa kwa wakulima.

Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi and w Mbalizi mkoani Mbeya , Mgombea Urais Dk.Samia Suluhu Hassan ameeleza Serikali itaendelea kuboresha huduma mbalimbali ili kugusa makundi yote katika jamii kwa kuwawezesha kupata maji,huduma za afya, miundombinu ya barabara na huduma nyingine zote muhimu katika jamii 

Kuhusu sekta ya kilimo Rais Dk.Samia amesema kumekuwa na hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwq na Serikali katika kuboresha mazingira ya sekta hiyo ambapo pia ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wakulima kuendelea kujisajiri kwa wingi katika mfumo wa ruzuku za mbegu na pembejeo za kilimo.

“Serikali bado inauwezo wa kutoa ruzuku hiyo kwa wakulima wengi zaidi nchini.Hadi sasa mbolea na mbegu za ruzuku zinagawiwa kwa wakulima nchi nzima. Kuna kila aina ya mbolea za kupandia na kukuzia,” amesema na kusisitiza umuhimu kwa wakulima kujisajili lakini akiwataka kutojihusisha na kuuza Mbolea au pembejeo inayotolewa na Serikali kwa mfumo wa ruzuku.

Amesema baadhi ya mazao ambayo mbolea na mbegu za ruzuku zinatolewa ni mahindi, mpunga, tumbaku na parachichi huku akieleza lengo la Serikali ni kuona tunazalisha mazao kwa wingi na kisha kuuza nje ya nchi. 

“Wakulima endeleeni kujisajili kwani serikali bado ina uwezo kutoa ruzuku. Tunzeni namba zenu za siri na msishirikiane na waovu kuuza pembejeo za ruzuku,” alisisitiza Dk. Samia.

Kuhusu wafugaji Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameahidi Serikali inakwenda kukamilisha ujenzi wa machinjio ya mifugo ya kisasa Utengule mkoani Mbeya huku akisisitiza pia serikali kuendelea na kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo lengo ni  kuongeza hadhi ya mifugo kutoka Tanzania  kwani nyama ya Tanzania inasoko kubwa katika soko la kimataifa.

“Kabla ya kampeni hiyo, mifugo ya Tanzania ilikuwa haina soko la uhakika kwa sababu ya kukosa rekodi za chanjo.”