KIUNGO mpya wa APR ya Rwanda, Dao Rouaf Memel ameanza na moto kwenye mashindano ya Kombe la Cecafa Kagame baada ya kuibuka mchezaji bora wa mechi dhidi ya Bumamuru wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0, juzi, Jumatano kwenye Uwanja wa KMC.
Licha ya mabao ya APR kufungwa na Ouattara Dj dakika ya saba na Togui dakika ya 75, fundi huyo alikuwa mwiba kwa Warundi hao kutokana na namna alivyokuwa akiunganisha kikosi hicho.
Memel aliyesajiliwa kutoka Sonabel ya nyumbani kwao Burkina Faso, alitunukiwa laki tano kama zawadi ya mchezaji bora wa mechi katika mashindano hayo ya klabu ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Ilikuwa mechi ngumu, nadhani kilichotubeba ni kucheza kwetu kama timu, ninafuraha mchezaji bora wa mechi naamini, hii inanifanya kujiona nina kazi kubwa zaidi ya kufanya katika michezo ijayo ili kuendelea kuisaidia timu yangu kufanya vizuri katika mashindano haya,” alisema.
APR ni miongoni mwa timu ambazo zimewahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mikongwe zaidi ukanda huu na msimu uliopita ilicheza fainali na kupoteza mbele ya Red Arrows ya Zambia kwa mikwaju ya penalti.
Mara ya mwisho kwa APR kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ilikuwa 2010 kwa kuichapa St. George ya Ethiopia mabao 2-0.