Dar es Salaam. Wakati mikopo inayotolewa na benki nchini ikiongezeka kwa asilimia 73.83 katika kipindi cha miaka minne, wakazi wa Dar es Salaam ndio wanufaika wakuu.
Dar es Salaam kuwa kinara wa uchukuaji mikopo katika kipindi hicho kunatajwa kuchangiwa na uwepo wa shughuli nyingi za kibiashara, ufikiaji huduma na mazingira mazuri yaliyopo.
Ripoti ya hali ya uchumi wa kanda iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha mikopo inayotolewa na benki nchini imeongezeka kutoka Sh20.39 trilioni mwaka ulioishia Machi 2022 hadi kufikia Sh35.45 trilioni kipindi kama hicho mwaka 2025.
Ukuaji huo umeshuhudiwa mfululizo kwani kabla ya mwaka 2025 ulitoka Sh24.51 trilioni mwaka 2023 hadi Sh30.03 Machi 2024.
Akizungumzia ukuaji huo, mchambuzi wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka amesema Dar es salaam inaongoza kwa sababu kwa miongo mingi imekuwa ikitambulika kama Jiji la kibiashara.
Hali hiyo imefanya huduma na mambo mengi yanayotaka kutekelezwa kuanzia ndani ya jiji hilo kabla ya kupelekwa maeneo mengine, akitoa mfano wa kampeni kama vile ya nishati safi.
“Hii inalifanya jiji hili kuwa sehemu yenye mzunguko mkubwa wa fedha na kufanya miji mingine kushindwa kukua kwa kasi. Inakua lakini si kwa kasi inayoweza kushawishi watoaji mikopo kwenda,” amesema.
Amesema licha ya mikopo mingi kuonekana inachukuliwa na wakazi wa Dar es Salaam, upo uwezekano wa fedha hizo kufanya kazi mikoa mingine nchini tofauti na Dar es Salaam.
“Kimatumizi unakopea Dar es Salaam lakini matumizi yanaelekezwa mikoa mingine, mtu anaweza kuwa na makao makuu Dar es Salaam lakini shughuli zake zinafanyika nchi nzima. Inaonekana kama ni kapu moja linapokea kingi lakini katika mgawanyo fedha zinatumika katika maeneo mbalimbali ila inaonekana hivyo kwa sababu tu makao makuu yao yapo Dar es Salaam,” amesema.
Ripoti hiyo ya BoT inaonyesha katika mikopo ya Sh35.45 trilioni iliyotolewa mwaka ulioshia Machi 2025, asilimia 53 yote ilibaki Dar es Salaam, ikiwa na maana kuwa, Sh18.781 trilioni za thamani ya mikopo yote iliwanufaisha wakazi wa Dar es Salaam na viunga vyake.
Kanda ya Kati inafuata ambako Sh5.68 trilioni zilichukuliwa na wakazi wa maeneo hayo ikiwa ni sawa na asilimia 16 ya thamani ya mikopo yote.
Kanda ya Ziwa ilifuata kwa kuchukua Sh4.611 trlioni, Kanda ya Kaskazini ikiwa nafasi ya nne kwa kuchukua mikopo ya Sh3.569 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 10.1 ya mikopo yote.
Nyanda za Juu Kusini walichukua Sh1.199 trilioni, huku Kusini Mashariki wakiwa na Sh1.603 trilioni.
“Hii inatokana pia na watu kushindwa kufikia huduma za fedha kwa urahisi kutokana na masharti yaliyowekwa na benki hali inayofanya watu wengi kuangalia njia mbadala,” amesema Deus Marwa, ambaye ni mfanyabiashara.
Amesema kiwango cha mikopo kilichotolewa na benki za biashara bado ni kidogo hali inayofanya baadhi ya watu kutafuta njia mbadala za kupata fedha ikiwamo kupitia kampuni zinazoitoa kwa masharti magumu.
Pia wengine huchukua kutoka kutoka kampuni za simu ambazo hazihitaji masharti magumu, ikiwamo dhamana.
Kumekuwa na ongezeko la asilimia 91.49 la mikopo ya kidijitali mwaka 2024. Mikopo iliyotolewa ikifikia Sh4.22 trilioni kutoka Sh2.20 trilioni mwaka 2023, huku idadi ya miamala pia ikiongezeka kwa asilimia 64.77, ikipanda kutoka milioni 163.42 hadi milioni 269.30, kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya Mfumo wa Malipo wa Taifa iliyotolewa na BoT mwaka 2024.
Ongezeko hilo linaonyesha kukua kwa mahitaji ya mikopo kwa njia ya simu ambayo imekuwa nyenzo muhimu ya kifedha kwa Watanzania wengi.